Guterres: Tuchukue hatua za pamoja ama tuangamie sote
7 Novemba 2022Takribani wakuu 100 wa nchi na serikali wanashiriki mkutano wa kilele wa mazingira unaofanyika katika mji wa kifahari wa Sharm al-Sheikh nchini Misri, wakikabiliwa na shinikizo la kupunguza zaidi uzalishaji wa hewa chafu pamoja na kuyafadhili mataifa yanayoendelea ambayo tayari yameathirika na ongezeko la joto duniani. Wakuu wa nchi wapatao 50 watatoa hotuba zao hii leo katika siku ya kwanza ya mkutano huo wa kilele.
Guterres kwa mara nyingine ameueleza mkutano wa COP27 kwamba "ubinadamu una machaguo mawili ya kuchukua hatua za pamoja au kuangamia".
"Tunakaribia kwa hatari sana kufikia hatua ya mwisho na ili kuepuka hatima hiyo mbaya, nchi zote za G20 lazima ziharakishe sasa hatua za mpito katika muongo huu. Ubinadamu una machaguo mawili: kushirikiana au kuangamia. Ama ni mkataba wa mshikamano wa mazingira au makubaliano ya pamoja ya kujiua."
Katibu huyo mkuu amehimiza "mkataba wa kihistoria baina ya nchi tajiri na zile zinazochipukia utakaolenga kupunguza uzalishaji wa gesi na kupunguza ongezeko la joto duniani kulingana na matarajio ya mkataba wa Paris. Kiongozi wa China Xi Jinping ambaye nchi yake inaongoza katika uzalishaji wa gesi chafu hahudhurii mkutano huo wakati Rais Joe Biden wa Marekani, ambaye nchi yake inashikilia nafasi ya pili katika orodha ya uchafuzi, atajiunga na mkutano huo baadae wiki hii.
Mara tu baada ya hotuba ya Guterres, rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu Sheikh Mohammed bin Zayed al-Nahya, alisema kuwa nchi yake ambayo ni mwanachama wa shirika la nchi zinazouza nje petroli, itaendelea kuzalisha mafuta ya kuchimbwa kwa kadri yatakavyohitajika.
Umoja wa Falme za Kiarabu utakuwa ndio mwenyeji wa mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira mwaka ujao, ambao utajaribu kukamilisha makubaliano yaliyofikiwa mwaka jana nchini Uingereza na mwaka huu huko Misri.Mkutano wa COP27 kufungua pazia nchini Misri
Makamu wa zamani wa rais wa Marekani Al Gore amesema licha ya kufanyika mazungumzo ya mara kwa mara bado kuna tatizo la uaminifu na hatua zinazochukuliwa hazitoshi.
Na Ubelgiji imekuwa nchi ya tatu tu duniani kuahidi ufadhili wa kuyasaidia mataifa yanayoendelea kukabiliana na hali zisizoepukika zinazosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi, ikitoa ufadhili wa euro milioni 2 na nusu kuisaidia Msumbiji.