Hali nchini Kenya bado ni ya wasiwasi kufuatia maandamano
3 Julai 2024Polisi waliwarushia mabomu ya kutoa machozi waandamanaji jijini Nairobi huku biashara nyingi zikiendelea kufungwa kwa hofu ya kuporwa.
Barabara kuu ya kuelekea mji wa pili kwa ukubwa nchini Kenya, Mombasa, ilifungwa huku waandamanaji wakiwasha moto. Mjini Mombasa, magari matano yalichomwa na waandamanaji nje ya hoteli ambayo mmiliki wake anadaiwa kuwafyatulia risasi waandamanaji waliokuwa wakifanya uporaji.
Soma pia: KNCHR: Watu 39 wameuawa katika maandamano ya Kenya
Licha ya Rais William Ruto kubadili msimamo na kusema kuwa hatotia saini mswada wa fedha, baadhi ya waandamanaji sasa wanamtaka kiongozi huyo kujiuzulu na kumshutumu kwa utawala mbovu.
Lakini baadhi ya washiriki wa maandamano hayo yanayoongozwa na vijana wameelezea wasiwasi wao kwamba baadhi ya Wakenya wanatumia maandamano kufanya vurugu.