ICC yaombwa kufanya uchunguzi dhidi ya Venezuela
27 Septemba 2018Hotuba ya Maduro katika mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa imekuja ikiwa ni saa kadhaa
baada ya Argentina, Chile, Colombia, Peru, Paraguayi na Canada kutoa mwito kwa mahakama ya ICC kuifanyia uchunguzi Venezuela kuhusiana na tuhuma dhidi ya nchi hiyo za mauaji pamoja na ukatili mwingine dhidi ya ubinadamu.
Kuendelea kusalia na minon'gono kuhusiana na tuhuma hizi inaweza ikatafsiriwa kama ni sawa na kuidhinisha tuhuma za uhalifu dhidi ya utawala wa Venezuela, alisema waziri wa mamabo ya nje wa Paraguayi Andres Rodriguez Pedotti.
Nchi hizo sita zina matumaini kuwa hatua hiyo inaongeza mbinyo kwa Maduro ili akomeshe ghasia na mgogoro ambao umesababisha zaidi ya watu milioni mbili kulazimika kuikimbia nchi hiyo na kusababisha pia mfumuko wa bei nchini humo kuongezeka kwa kiwango cha juu.
Hata hivyo maafisa wa Venezuela wamekua wakipinga ukosoaji wa kimataifa wakisema wakosoaji wanachochewa na mabepari wanaoongozwa na Marekani ili kuhalalisha uvamizi dhidi ya taifa hilo.
Akizungumza katika hadhara hiyo ya Umoja wa Mataifa Maduro amelalamika kuwa Marekani inaishambulia Venezuela kupitia vikwazo pamoja na njia nyingine huku pia ikiyashawishi mataifa mengine kuwa na mahusiano mabovu ya kidiplomasia na Venezuela.
Maduro alisema Marekani inataka kuendelea kutoa amri kwa ulimwengu kama vile dunia ni mali yake lakini hata hivyo Venezuela haita salimu amri.
Maduro yuko tayari kuzungmza na Trump
Ama kwa upande mwingine kiongozi huyo wa Venezuela amesema yuko tayari kuzungumza na rais wa Marekani Donald Trump.Canada ni miongoni mwa nchi ambazo zimetoa mwito Venezuela ichunguzwe na mahakama ya ICC mnamo wakati mwendesha mashitaka mkuu wa mahakama hiyo , Fatou Bensouda akiwa tayari ameanzisha uchunguzi wa awali kuhusiana na madai kuwa vikosi vya serikali ya Venezuela tangu mwaka 2017 mara kadhaa vilitumia nguvu ya ziada kuwatawanya na kuwadhibiti waandamanaji na pia kuwadhalilisha baadhi ya wafuasi wa upinzani waliotiwa mbaroni.
Ni juu sasa ya mwendesha mashitaka kuamua la kufanya kuhusiana na wito uliotolewa na mataifa hayo sita licha ya mwendesha mashitaka kutotoa ufafanuzi mara moja juu ya pendekezo hilo.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch ni moja ya mashirika yaliyopongeza hatua iliyopendekezwa na mataifa hayo sita ambayo imejikita katika ripoti mbili ikiwa ni pamoja na ripoti ya tume ya shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na haki za binadamu iliyofichua tuhuma kadhaa zikiwemo za mauaji na ukiukaji mwingine wa haki za binadamu.
Mwandishi : Isaac Gamba/APE
Mhariri: Bruce Amani