ICJ kujadili ukaliaji wa Israel kwenye maeneo ya Palestina
19 Februari 2024Kwa muda wa siku 6, majaji 15 wa Mahakama hiyo wataujadili mzozo huo wa miongo kadhaa, na vikao hivyo vinatarajiwa kuhudhuriwa na mataifa mbalimbali. Wawakilishi wa Palestina wamewasilisha hoja zao kuhusu uharamu wa ukaliaji huo.
Licha ya kuwa vita vinaendelea katika Ukanda wa Gaza, vikao vya Mahakama hiyo vinajikita zaidi kuhusu ukaliaji wa kimabavu wa Israel katika maeneo ya Ukingo wa Magharibi, Gaza na Jerusalem Mashariki.
Soma pia:Mahakama ya ICJ yaitupilia mbali kwa sehemu kubwa kesi ya Ukraine dhidi ya Urusi
Hayo yanajiri wakati Misri ikisema imewasilisha shauri lake ICJ, ikiishutumu Israel kwa matendo haramu katika maeneo ya Palestina na kwamba itatetea hoja yake mbele ya Mahakama hiyo ifikapo Februari 21.
Diaa Rashwan, mkuu wa kitaifa wa sekta ya habari nchini Misri amesema shauri hilo linapinga vikali sera za Israel za mateso, ubaguzi wa rangi na matendo mengine ambayo yanakiuka waziwazi kanuni na sheria za kimataifa za kibinadamu.