Israel yaendeleza mashambulizi Gaza
23 Oktoba 2023Israel imeendeleza mashambulizi katika Ukanda wa Gaza ambako kumeshuhudiwa uharibifu na maafa makubwa, na viongozi mbalimbali ulimwenguni wakiendelea kujadili namna ya kuutafutia suluhu mzozo huo. Ndege za kivita za Israel zimeshambulia maeneo mbalimbali huko Gaza kabla ya mashambulizi ya ardhini yanayotarajiwa katika eneo hilo lililozingirwa na linaloongozwa na Hamas.
Hofu ya kuenea kwa vita hivyo imeongezeka wakati ambapo vikosi vya Tel Aviv vimefanya pia mashambulizi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu na Israel, lakini pia huko Syria na Lebanon ambako walipambana na kundi la wanamgambo wa Hezbollah.
Maafisa wa Palestina wanasema mji wa kati wa Deir al-Balah ulikuwa umeathirika vibaya kufuatia mashambulizi ya Jumamosi na Jumapili.
Hayo yanakuja wakati tawi la kijeshi la kundi la Hamas, Izz el-Deen al-Qassam, likisema kuwa limewashambulia wanajeshi wa Israel na kuwarejesha nyuma, walipokuwa wakijaribu kuingia katika Ukanda wa Gaza eneo la kusini la Khan Younis.
Soma pia: Mawaziri wa EU kujadili ufadhili wa Ukraine na mzozo wa Gaza
Wapiganaji hao wamedai kuharibu baadhi ya zana za kijeshi pamoja na vifaru vya Israel kabla ya kurejea salama katika kambi yao.
Jeshi la Israel ambalo limekuwa likidhamiria kuanzisha mashambulizi ya ardhini huko Gaza, halijaelezea chochote juu ya taarifa hii, ingawa lilisema kuwa lilifanya operesheni ya kiwango cha chini ndani ya Gaza usiku wa jana.
Kwa upande mwengine, misafara miwili ya misaada imewasili katika Ukanda wa Gaza mwishoni mwa juma kupitia kivuko cha Rafah kutokea Misri.
Israel imesema malori hayo yalibeba chakula, maji na vifaa vya matibabu, lakini hadi sasa haijaruhusu kupelekwa kwa mafuta, ambayo yanahitajika mno katika uendeshaji wa mifumo ya maji na hospitali.
Wakaazi wa Gaza wametaja kuteseka na hali hii:
" Sisi ni binaadamu. Na tunataka kuishi kwa utu. Na kuwa na uwezo wa kuwalisha watoto wetu. Kufanya kazi, kula na kunywa. Na hatuvitaki vita hivi. Je, haya ndiyo maisha? Hapana! sio maisha."
Wito wa Umoja wa Ulaya
Hapa UIaya, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, amehimiza hii leo uwasilishaji haraka wa misaada huko Gaza, na kusema umoja huo unajadili wito wa "usitishwaji mapigano kwa sababu za kiutu" katika mzozo kati ya Israel na Hamas.
Soma pia: Vita vya Israel vyahofiwa kusambaa maeneo mengine
Kabla ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya unaofanyika leo huko Luxemburg, Borrell amesema kilicho muhimu zaidi ni kuchukua hatua za haraka zitakazopelekea kurejeshwa kwa huduma za msingi kama usambazaji wa maji safi na umeme.
Borrell amesema kuwa malori kadhaa ya misaada ya kibinaadamu ambayo yameruhusiwa kuingia Gaza kutoka Misri hayatoshi na kwamba mafuta yanayozalisha umeme na kuwezesha usambazaji wa maji ya kunywa yanahitajika mno huko Gaza.
Umoja wa Ulaya wenye jumla ya mataifa 27 umegawanyika kwa muda mrefu katika sera zake kuhusu suala la Israel na Palestina, na umekuwa ukitatizika kwa kutoa kauli zinazokinzana tangu kuongezeka kwa ghasia kufuatia shambulio la Oktoba 7 la Hamas na mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel katika Ukanda wa Gaza.
Soma pia: Papa Francis ataka vita visitishwe Gaza
Israel na mshirika wake mkuu Marekani hadi sasa wamekaidi wito wowote wa kusitishwa kwa operesheni ya kijeshi dhidi ya kundi la Hamas ambalo linazingatiwa na Umoja wa Ulaya, Ujerumani ikiwemo na mataifa mengine kadhaa kuwa kundi la kigaidi.
Uvamizi wa wanamgambo wa Hamas huko Israel mnamo Oktoba 7 uliwaua takriban watu 1,400 na kuwachukua mateka wengine zaidi ya 200 katika shambulio baya kuwahi kutokea katika historia ya Israel, ambayo imejibu kwa mashambulizi makubwa ambayo pia hadi sasa yameua zaidi ya Wapalestina 4,600.