Israel yashambulia Gaza na kuamuru watu zaidi kuondoka Rafah
11 Mei 2024Israel pia imetoa amri ya watu kuhamia maeneo salama licha ya tahadhari ya Umoja wa Mataifa dhidi ya kushambulia eneo mji huo wa Rafah uliofurika watu.
Shirika la habari la Ufaransa AFP, madaktari na wengine walioshuhudia, wameripoti kutokea kwa mashambulizi katika eneo la pwani, ambapo Umoja wa Mataifa unasema misaada ya kibinadamu imezuiwa.
Hii ni baada ya wanajeshi hao wa Israel kukaidi wito wa kimataifa wa kutoishambulia Rafah na wiki hii kuingia katika eneo la mashariki mwa mji huo, hatua iliyosababisha kufungwa kwa kivuko kimoja muhimu cha msaada.
Taarifa ya hospitali ya Al-Aqsa Martyrs mjini Deir al-Balah, imesema kuwa takriban watu 21 waliuawa wakati wa mashambulizi katikakati mwa Gaza na kupelekwa hospitalini humo.
Mjini Rafah, mashuhuda wameripoti kuwepo kwa mashambulizi makali ya anga karibu na kivuko kinachopakana na Misri.
Mashambulizi mengine yanaripotiwa Kaskazini mwa Gaza.